Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waajiri nchini wametakiwa kuwa na programu endelevu za mazoezi kwenye maeneo yao ya kazi kwa lengo la kuwalinda wafanyakazi dhidi magonjwa yasiyoambukiza ambayo kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni yamekuwa chanzo kikubwa cha vifo.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Prof. Joyce Ndalichako, alipokuwa akizungumza na mamia ya waajiri na wafanyakazi walioshiriki katika bonanza la michezo lililoandaliwa na Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE).
Bonanza hilo lilowashirikisha waajiri zaidi ya 100 limefanyika katika viwanja vya Leadres Club vilivyopo Kinondoni jijini Dar es Salaam ambapo timu za waajiri zilishindana katika michezo mbali mbali ikiwemo mpira wa miguu, mpira wa pete, mbio fupi, kuvuta Kamba, kufukuza kuku na kukimbia kwenye magunia.
Aidha, Waziri Ndalichako amewakumbusha waajiri kuweka mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi ili kuwakinga wafanyakazi na vihatarishi vya magonjwa na ajali ambazo zimekuwa zikigharimu maisha ya watu au kuwasababishia ulemavu.
“Ninawapongeza sana waajiri wote ambao wameitikia wito wa ATE na kujitokeza kwenye bonanza hili kwa wingi kwani mwitikio umekuwa mkubwa sana hivyo nawasisitiza kwamba programu kama hizi kuwa endelevu,” amesema Waziri Ndalichako, nakuongeza:
“Kwa upande wa OSHA ninawashukuru kwa kuona umuhimu wa kuwahamasisha masuala ya mazoezi kwasababu natambua kwamba wameshiriki kwa kufadhili bonanza hili ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa na ningependa kuona kwamba linakuwa endelevu,” amesema Prof. Ndalichako.
Mkurugenzi Mtendaji wa ATE, Suzanne Ndomba, amesema lengo la kuandaa bonanza hilo ni kuwahamasisha waajiri kuona umuhimu wa kuwekeza katika afya za wafanyakazi kwa ajili ya maendeleo ya biashara na uwekezaji nchini.
“Tunashukuru waajiri kwa kuitikia wito wetu wa kushiriki kwenye bonanza hili kwani mwitikio umekuwa mzuri. Jumla ya waajiri 129 wameshiriki pamoja na kwamba bonanza hili tumelifanya kwa mara ya kwanza. Hivyo, tunawakumbusha waajiri kuwekeza katika afya za wafanyakazi kupitia programu za mazoezi kwenye maeneo yao ya kazi,” amesema Ndomba.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, amesema Taasisi yake imefadhili bonanza hilo baada ya kubaini ongezeko kubwa la wafanyakazi wanaopata magonjwa yasiyoambukizwa katika sehemu za kazi.
“Katika shughuli zetu za ukaguzi pamoja na uchunguzi wa afya za wafanyakazi kwenye maeneo ya kazi tumebaini kwamba wafanyakazi wengi wanapata magonjwa yasiyoambukiza kama vile kisukari, presha na uzito uliokithiri kutokana na mtindo wa maisha. Hivyo, tumeshiriki katika bonanza ili kuwahasisha waajiri kuchukua hatua za kudhibiti ongezeko la magonjwa hayo kwenye maeneo yao ya kazi kupitia michezo,” amesema Mwenda.
Aidha, Kiongozi huyo Mkuu wa OSHA, amesema michezo ina mchango mkubwa katika kuondoa kihatarishi cha kisaikolojia kwenye maeneo ya kazi ambacho ni chanzo kikubwa cha ajali na hivyo ni vema waajiri wakawekeza katika programu endelevu za michezo kama namna mojawapo ya kupunguza ajali mahali pa kazi.