32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 1, 2023

Contact us: [email protected]

Ndalichako: wanafunzi 682 warudishwe UDSM

Na ASHA BANI-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Elimu, Sanyansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ameamuru wanafunzi 682  walioondolewa katika usajili wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)  warudishwe.

Agizo hilo alilitoa   Dar es Salaam jana alipofungua mafunzo ya siku tano ya kuandaa hesabu za fedha za Serikali yaliyofanyika katika Chuo cha Kodi.

Alisema amesikia tangu mwishoni mwa wiki na tayari ameshauagiza uongozi wa TCU na uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kukaa pamoja na kumaliza tofauti hizo.

Alisema chuo kikuu kina nafasi 3000, tatizo lililojitokeza ni la ufundi kutokana na wanafunzi wengi kupenda chuo hicho hivyo ameomba uongozi kumaliza tatizo hilo na watoto waweze kupokelewa.

“Wengi wanapenda UDSM na tatizo lililokuwa linaweza kurekebishika, wote ni idara za serikali TCU na UDSM hawakutakiwa kushindana na ndiyo maana nimewaagiza mpaka Jumamosi wawe wamemaliza tofauti zao.

“Nafikiri mpaka leo saa tisa  (jana) watakuwa wameshawekana sawa,” alisema Prof.Ndalichako.

Habari zilienea kuanzia juzi kuwa takribani wanafunzi 682 wamefutiwa usajili wao   UDSM.

Akizungumzia   wahasibu wabadhirifu  ndani ya idara na taasisi za Wizara ya Elimu, alisema   kiama chao kinakuja.

Alisema kumekuwapo  changamoto nyingi kwa wahasibu mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na kuchakachua nyaraka mbalimbali na hata kushindwa kufunga hesabu   wanapotakiwa kuwasilisha hesabu zao mwishoni mwa mwaka.

“Tayari nafanya kazi na kwa kushirikiana na Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, kuhakikisha dosari ambazo zinatokea kwa wahasibu wa wizara yangu nchini na taasisi zake.

“Wale watakaoonekana kushindwa kufanya vema na hata kugundulika kuwa wameghushi basi  wawajibishwe.

“Lengo ni kuhakikisha mapato na wizi wa fedha za umma na hasa taasisi za elimu kuanzia ngazi za wilaya, mkoa zinadhibitiwa kwa ukamilifu,” alisema.

Aliongeza   ukaguzi mbalimbali unaonyesha wahasibu wamekuwa wakiandaa nyaraka za udanganyifu, wengine kushindwa kuandaa   nyaraka hizo bila sababu za msingi kumbe ni wizi.

“Wengine wana msemo ambao wamekuwa wakiutumia kuwa ‘kila mbuzi anakula kwa urefu wa kamba yake’ sasa kamba inakatika na hizo fedha za serikali katika awamu hii ni sumu ambayo haijaribiwi kwa kuonja,

“Wahasibu wengi wamekuwa wakighushi majina ya watu au kuandika kwa kujirudia hata mara tatu, mfano waliohudhuria semina, mafunzo ili mradi wajilipe mara tatu tatu jambo linaloonyesha  wahasibu wanachezea fedha za serikali, huo ni wizi wa kishamba,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,471FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles