Ndalichako: Bodi ya Mikopo ijiandae vyuo vikifunguliwa

0
902
WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kujiandaa kulipa wanafunzi wakati wowote vyuo vitakapofunguliwa.

Ametoa maelekezo hayo jana katika ziara yake ya kikazi Dar es Salaam ambako amekutana na menejimenti ya HESLB.

“Katika kipindi hiki ambapo vyuo vya elimu ya juu vimefungwa, HESLB ihakikishe inatumia muda huu kufanyia kazi changamoto zote za wanafunzi ili vyuo vitakapofunguliwa malipo ya mikopo ya wanafunzi yafanyike kwa wakati,” alisema Profesa Ndalichako

Pia alitumia ziara hiyo kuwakumbusha watumishi wa HESLB kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Akizungumza katika kikao kati ya waziri na menejimenti ya HESLB, Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema wapo tayari kuwahudumia wanafunzi muda wowote vyuo vitakapofunguliwa.

“Sisi tupo tayari. Serikali ilishatupa fedha na tutawawezesha wateja wetu mara moja vyuo vikifunguliwa,” alisema Badru.

Aliongeza kuwa taasisi yake inakamilisha mwongozo wa utoaji mikopo kwa mwaka wa masomo 2020/21 kwa kushirikisha wadau, wakiwemo wanafunzi kupitia shirikisho lao la TAHLISO.

Kuhusu urejeshaji wa mikopo iliyoiva, alisema Sh bilioni 160 zimekusanywa katika kipindi cha miezi tisa iliyopita, Julai 2019 hadi Aprili 2020.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here