23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Ndalichako awashukia watoa takwimu za uongo

Na RAMADHAN HASSAN -DODOMA

WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, amewashukia watu wanaotoa takwimu za uongo wanaodai kwamba wizara yake imekuwa ikipokea asilimia 56 ya fedha za bajeti kutoka serikalini.

Alisema wizara yake imekuwa ikipokea asilimia 86 ya fedha za bajeti kutoka serikalini, huku akishangazwa pia na wanaodai kuwa fedha hizo hazitolewi katika wizara yake.

Kauli hiyo aliitoa jana jijini hapa wakati akifungua mkutano wa wadau wa elimu ambao walikuwa wakifanya tathmini ya hali ya elimu nchini.

Alisema Wizara ya Elimu imekuwa ikipokea fedha za ziada Sh bilioni 8.2 kulipa madeni kutoka serikalini.

“Na tumepewa ziada ya bilioni 8.2 kwa ajili ya kulipa madeni. Ukiangalia unapewa mpaka fedha za ziada, kwa kweli nikimsikia mtu anasema fedha katika Wizara ya Elimu hazitolewi lazima nitamshukia kama mwewe,” alisema Ndalichako.

Pamoja na hali hiyo alitolea ufafanuzi kuhusu takwimu ambazo zimekuwa zikitolewa kwamba Serikali imekuwa ikitoa asilimia 56 ya bajeti katika wizara hiyo.

Alisema jambo hilo si la kweli na kwamba wizara yake  imekuwa ikipokea asilimia 86.5 ya bajeti kutoka serikalini.

“Nitumie nafasi hii kutoa ufafanuzi kuhusiana na takwimu kwamba sekta ya elimu imekuwa ikipata bajeti ambayo inashuka, labda niseme tu kwamba ni vema tunapokuwa tukitoa takwimu tuwe tunaangalia tunazitoa kutoka wapi.

“Kila mmoja wenu anaweza akatafuta katika simu yake ya mkononi kwenye mtandao, ukiangalia bajeti ya mwezi Mei 2018 katika kitabu changu cha hotuba nilisema bayana kwamba hadi kufikia Machi 31, 2018 Wizara yangu ilikuwa imepata jumla ya fedha trilioni 1.5 kati ya shilingi trilioni 1.336 sawa na asilimia 75 na hadi Juni 2018 Serikali ilikuwa imetoa zaidi ya asilimia 86.5. Sijafahamu hizi takwimu kwamba serikali imetoa asilimia 56 ya bajeti zimetoka wapi,” alisema.

Alisema bajeti ya Wizara ya Elimu kwa mwaka 2017/18 ilikuwa ni Sh trilioni 1.336 na mwaka 2018-2019 ilikuwa ni Sh trilioni 1.407 hivyo akawashangaa wale wanaosema bajeti hiyo imekuwa ikishuka.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet), John Kallaghe alisema kuwa wamebaini shule zinapata shida kulipia mahitaji muhimu ambayo mwanzoni walikuwa wanalipa kutokana na michango ya wazazi.

“Hii ilikuwa ni pamoja na ujenzi na ukarabati wa shule, kununua zana za kufundishia, na kuajiri walimu wa ziada. Kwahiyo kuna umuhimu wa kupitia tena kwa undani utekelezaji wa mpango wa elimu bila malipo,” alisema Kallaghe.

Alisema uwiano wa walimu ni muhimu katika kuboresha utoaji wa elimu bora.

“Serikali imefanya mambo mengi ikiwemo elimu bure, muhimu ni kuangalia wanafunzi wanaojiunga na shule wanamaliza bila ya kuishia njiani kwa sababu nyinginezo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles