28.1 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

Nchi Nne mbioni kuanza kunufaika na Gesi Asilia ya Tanzania

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limetangaza kuwa limeingia makubaliano na kampuni mbili za kimataifa kwa ajili ya ujenzi wa mitambo ya kisasa ya kusafirisha gesi asilia kwenda nchi za Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Kenya, na Zambia.

Hesehmu ya washiriki wa semina hiyo wakiwa katika pich ya pamoja.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Ahmad Massa, alisema makubaliano hayo yalifikiwa Mei 2024 na kampuni za ROSETTA kutoka Falme za Kiarabu, na KS Energy ya Uturuki. Aliongeza kuwa mkataba mwingine umesainiwa na kampuni ya ESSA kutoka Indonesia kwa ajili ya uzalishaji wa mbolea aina ya urea.

“Tayari TPDC inampango wa kuuza gesi asilia kwa majirani zetu, ambao tumeingia nao makubaliano ya awali. Nchi hizo ni Uganda, Kenya, DRC na Zambia, na gesi hiyo itasafirishwa kwa wateja kupitia njia ya bomba,” alisema Massa wakati akifungua semina ya waandishi wa habari iliyofanyika Septemba 13, 2024, jijini Dar es Salaam.

Kuhusu mkataba wa uzalishaji wa mbolea kupitia gesi asilia, Massa alibainisha kuwa mbolea itakayozalishwa kupitia mpango huo itakuwa mkombozi kwa sekta ya kilimo nchini. “Mbolea hii haitasaidia tu kilimo nchini, bali pia italifanya taifa letu kuwa tegemeo la mbolea katika ukanda wa Kusini mwa Afrika,” aliongeza.

Massa pia alieleza kuwa TPDC, kwa kushirikiana na kampuni ya AR Petroleum, wanatarajia kuanza uzalishaji wa gesi asilia katika eneo la Ntorya. Hapo, futi za ujazo milioni 60 za gesi zitazalishwa kila siku na kupelekwa kwenye kiwanda cha kuchakata gesi cha Madimba, mkoani Mtwara.

“Zaidi ya hayo, TPDC imeanza kuruhusu sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa vituo vya gesi asilia iliyogandamizwa (CNG). Hadi sasa, zaidi ya kampuni binafsi 30 zimeruhusiwa kujenga vituo vya CNG nchini, ili kuwezesha matumizi ya gesi asilia katika maeneo mbalimbali,” alifafanua Massa.

Kwa upande wake, Mjiolojia Mwandamizi kutoka Idara ya Mkondo wa Juu TPDC, Dk. Shaidu Nuru, alisema kuwa uzalishaji wa gesi nchini ulianza rasmi mwaka 2004 katika vitalu vya SongoSongo na Mnazi Bay, huku visima 96 vya utafiti na uzalishaji vikiwa vimechimbwa hadi sasa.

Mhandisi Mwandamizi kutoka Idara ya Mkondo wa Chini TPDC, Anthony Karomba, aliongeza kuwa asilimia 50 ya umeme unaozalishwa nchini hutegemea gesi asilia, na viwanda 56 tayari vimeunganishwa na mfumo huo. Pia, zaidi ya magari na bajaji 5,000, nyumba 1,511, na taasisi 13 zinatumia gesi hiyo.

Akizungumzia mpango wa matumizi ya nishati safi, Karomba alisema, “Kwa kipindi cha miaka 10 ijayo, tunatarajia kuwa asilimia 50 ya wakazi wa Dar es Salaam watakuwa wanatumia nishati safi ya gesi asilia.”

Meneja Mawasiliano wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania(TPDC), Marie Msellemu, akizungumza wakati wa semina hiyo.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles