30.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NCHI ILIVYOLIWA KWENYE MADINI

Rais Dk. John Magufuli akipokea taarifa ya uchunguzi wa kiasi cha madini kilichopo katika mchanga (makinikia) uliokuwa ukisafirishwa nje ya nchi kutoka kwenye machimbo ya madini nchini, kutoka kwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Profesa Abdulkarim Hamis Mruma Ikulu, Dar es Salaam jana.PICHA: IKULU

 

 

Na NORA DAMIAN -DAR ES SALAAM

KAMATI Maalumu iliyoundwa na Rais Dk. John Magufuli kuchunguza kiwango cha madini yaliyopo katika mchanga wa dhahabu (makinikia) unaosafirishwa kwenda nje ya nchi, imeanika namna nchi inavyotafunwa bila huruma kwenye sekta ya madini.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyokabidhiwa jana kwa Rais Magufuli, kamati hiyo imebaini kontena 277 za mchanga huo zilizokuwa Bandari ya Dar es Salaam na maeneo mengine ya nchi, zina dhahabu na madini mengine yenye thamani ya takribani Sh trilioni 1.441.

Wakati kamati hiyo ikibaini hayo, taarifa za Wakala wa Serikali wa Ukaguzi Madini (TMAA) na nyingine za kusafirisha mchanga huo zilizokaguliwa na kamati, zinaonyesha mchanga huo una madini yenye thamani ya Sh bilioni 112.1.

Mwenyekiti wa kamati hiyo, Profesa Abdulkarim Mruma, akizungumza kabla ya kumkabidhi rais ripoti hiyo, alisema walifanya uchunguzi wa kimaabara kubainisha aina, kiasi na viwango vya madini yatakayoonekana katika makinikia kisha kubainisha thamani ya madini hayo kwa kuzingatia bei katika soko la dunia.

“Tulifuata taratibu za kisayansi katika kufanya uchunguzi wetu, katika baadhi ya makontena tuliyapakua yote na kukagua na mengine tulichimba mashimo sehemu ya chini, katikati na juu.

“Tulichunguza utendaji wa TMAA na utaratibu mzima wa ufungaji sealed (lakiri) kabla ya kutoa vibali vya kusafirisha makontena,” alisema Profesa Mruma.

MATOKEO YA UCHUNGUZI

Kwa upande wa dhahabu, kamati hiyo ilibaini kuwapo kwa viwango vya juu ndani ya mchanga (makinikia) yaliyofanyiwa uchunguzi. 

Katika makontena yote 277, madini ya dhahabu yalikuwa na uzito wa kati ya tani 7.8 na 13.16 zenye thamani ya kati ya Sh bilioni 676 na trilioni 1.147.

“Taarifa tulizopata kutoka kwa wazalishaji pamoja na TMAA, zinaonyesha kuwa makinikia yana wastani wa tani 1.2 za dhahabu zenye thamani ya Sh bilioni 97.5.

“Kutokana na tofauti hii kubwa kati ya viwango vya dhahabu vilivyopo kwenye taarifa za usafirishaji na vile ambavyo kamati imevibaini, ni dhahiri kuwa taifa linaibiwa sana kupitia usafirishaji wa makinikia nje ya nchi,” alisema Profesa Mruma.

Alisema madini ya fedha yaliyopatikana katika makinikia hayo ni kati ya tani 1.7 na 1.9 ambazo zina thamani kati ya Sh bilioni 2.1 na bilioni 2.4.  Wazalishaji na TMAA walisema madini yaliyopo ni kilogramu 831 yenye thamani ya Sh bilioni 1.0.  

Katika uchunguzi huo, madini ya shaba yalikuwa kati ya tani 1,440.4 na 1,871.4 ambayo yana thamani kati ya Sh bilioni 17.9 na bilioni 23.3.

Nyaraka za usafirishaji zilizopatikana bandarini zilionyesha kuna tani 1,108 tu za shaba zenye thamani ya Sh bilioni 13.6.

 Kamati pia ilichunguza shehena ya mbale za shaba ndani ya makontena matano yaliyozuiliwa bandarini na kubaini kulikuwa na viwango vya dhahabu hadi kufikia gramu 38.3 kwa tani viwango ambavyo havikuonyeshwa kwenye ripoti ya upimaji wa kimaabara wa TMAA.

Profesa Mruma alisema kamati haikuonyeshwa mahala popote yanakopelekwa makinikia hayo na kubaini kuwa wanauziwa watu wengine na makampuni.

MADINI MENGINE

Katika uchunguzi huo, kamati hiyo ilibaini kuwapo kwa madini mengine ambayo thamani yake inakaribiana na dhahabu, lakini hayakuorodheshwa wala kujumuishwa kwenye ukokotoaji wa mrabaha.

“Uchunguzi pia umeonesha kuwepo kwa madini mkakati (strategic metals) ambayo kwa sasa hivi yanahitajika sana duniani na yana thamani kubwa sambamba na thamani ya dhahabu. 

“Pamoja na kuwa na thamani kubwa, lakini hayatumiki katika kukokotoa mrabaha, wanasema hawayahitaji. Lakini tulipoingia kwenye mtandao tuliona yanahitajika na huu ni upotevu wa mapato,” alisema Profesa Mruma.

Aliyataja madini hayo kuwa ni iridium, rhodium, ytterbium, beryllium, tantalum na lithium.

Profesa Mruma alisema thamani ya aina zote za Metali Mkakati katika makontena 277 yaliyoko bandarini, ni kati ya Sh bilioni 129.5 na bilioni 261.5.

Alisema madini ya iridium ni wastani wa kilogramu 1,773 na 3,808.8 zenye thamani kati ya Sh bilioni 108 na 231.

Rhodium ni kati ya kilogramu 9.4 na 21.6 zenye thamani kati ya Sh bilioni 0.7 na bilioni 1.5.

Ytterbium ni kati ya kilogramu 1024.9 na 1,357.3 zenye thamani ya Sh bilioni 12.4 na bilioni 16.4.

Beryllium ni kati ya tani 5.4 na 7.5 zenye thamani kati ya Sh bilioni 6.0 na bilioni 8.3.

Tantalum ni kati ya kilogramu 3240.9 na 4,792 zenye thamani kati ya Sh bilioni 1.9 na bilioni 2.8.

Lithium ni kati ya kilogramu 5,955.5 na 8,254.6 zenye thamani kati ya Sh bilioni 1.0 na bilioni 1.4.

 “Kwa kuwa viwango hivi vya thamani havitumiki kukadiria mapato ya Serikali, ni wazi kuwa kuna upotevu mkubwa sana wa mapato kwa nchi yetu,” alisema Profesa Mruma.

Pia alisema katika makinikia hayo kulikuwa na madini ya sulfur yenye uzito wa kati ya tani 2,161 na 2,825.4 ambayo yana thamani kati ya Sh bilioni 1.4 na bilioni 4.9.

Madini ya chuma ni wastani wa tani 1,496 na 1,695 ambayo yana thamani kati ya Sh bilioni 2.3 na bilioni 2.6.

“Kulikuwa na madini mengine kama Zinc, lakini thamani yake hazikuwa kubwa sana… hata haya madogo nashauri tusiyatupe,” alisema.

UZITO WA MAKONTENA

Profesa Mruma alisema walibaini makontena yalikuwa na uzito mkubwa wa tani 23.1 tofauti na ulioelezwa awali wa tani 20 kwa kila kontena.

Alisema walipima makontena manne yaliyokuwa bandarini na kubaini kuwa yalikuwa na uzito wa ziada kati ya tani 3.1, 2.95, 2.7 na 2.2.

“Hivyo basi, ongezeko hili la uzito linaongeza thamani ya makinikia na hivyo kuongeza upotevu zaidi wa mapato ya Serikali,” alisema Profesa Mruma.

TMAA

Ripoti hiyo ilibainisha kuwa TMAA haifungi utepe wa udhibiti mara baada ya kuchukua sampuli kwenye makontena na badala yake udhibiti hufanyika baada ya siku kadhaa katika hatua za mwisho za usafirishaji wa makontena.
 “Hali hii inatoa mianya ya kufanyika udanganyifu, viwango na thamani ya makinikia baada ya uchukuzi wa sampuli. Mtu anaweza kutempa kwa kuongeza viwango vya makemikia au hata uzito,” alisema Profesa Mruma.

MAPENDEKEZO

Kamati hiyo ilipendekeza Serikali ichukue hatua kwa watendaji wa TMAA na wizara kutokana na kutosimamia vyema tathmini ya viwango halisi vya madini/metali mbalimbali vilivyopo katika makinikia na kuisababishia Serikali upotevu wa mapato.

Pia ilipendekeza Serikali iendelee kusitisha usafirishwaji wa mchanga nje hadi mrabaha stahiki utakapolipwa serikalini kwa kuzingatia thamani halisi ya makinikia kama ilivyoainishwa kwenye uchunguzi huo.

 “Ujenzi wa mashine ya kuchenjulia makinikia nchini ufanyike haraka iwezekanavyo. TMAA ifunge tepe kudhibiti udanganyifu unaoweza kutokea baada ya uchukuaji wa sampuli na ipime madini yote ambayo yamo ndani ya makinikia na kujua thamani yake bila kujali kilichoandikwa na msafirishaji,” alisema Profesa Mruma.

Pia kamati ilipendekeza Serikali iweke mfumo wa kushtukiza kwa lengo la udhibiti na usafirishaji madini nje ya nchi.

Kuhusu uwezo wa scanner inayotumika bandarini kukagua vilivyomo ndani ya makontena, Profesa Mruma alisema haina uwezo kwani inaonyesha umbo tu la shehena ya makinikia.

“Tulichukua vipande vya chuma na kuweka kwenye kontena, lakini scanner haikuona kitu. Hivyo, mtu akiamua kuficha kitu kwenye makinikia scanner haziwezi kuona, Serikali itumie wataalamu wa mionzi kufunga scanner zitakazofanya kazi kwa usahihi,” alisema scanner.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles