Na Waandishi Wetu, Dar es Salaam
VIONGOZI wastaafu na wasomi nchini wamesema hivi sasa taifa linakabiliwa na viashiria vya uvunjivu wa amani hali inayosababisha nchi kuyumba.
Kutokana na hali hiyo wamesema ni muhimu kudhibiti amani hasa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25 mwaka huu.
Walikuwa wakizungumza Dar es Salaam jana katika mkutano uliandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere unaojadili amani na umoja wa nchi.
Jaji Warioba
Akizungumzia hali ya amani, Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba, alisema hivi sasa nchi imekuwa na viashiria vingi vya uvunjifu wa amani jambo ambalo linaweza kuhatarisha maisha ya wananchi.
Alisema kuibuka migogoro baina ya wananchi na Serikali ni miongoni mwa sababu za dalili ya uvunjifu wa amani.
Jaji Warioba ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema viongozi wanapaswa kukaa pamoja na kujadili suala hilo.
“Hivi sasa kuna baadhi ya watu wanapenda kujitambulisha kwa ukanda, ukabila, udini na uongozi jambo ambalo ni hatari kwa wananchi kwa sababu linaweza kuleta ubaguzi.
“Hali hii ilikuwapo kabla ya uhuru ambako Serikali ya Mkoloni ya Uingereza iliweza kuwabagua wananchi jambo lililosababisha viongozi waasisi na wananchi waliokuwapo kipindi hicho kupigania uhuru.
“…baada ya kupata uhuru, Serikali ya awamu ya kwanza ilitunga sheria ya uraia ambayo iliweza kuondoa ubaguzi wa rangi, ukabila na ukanda na kuwaunganisha wananchi, kutafuta viongozi na kutumia lugha moja ya kiswahili,” alisema Jaji Warioba.
Alisema kuwapo vitendo hivyo ni lazima Watanzania wajue kwamba amani iliyokuwapo ilitafutwa hivyo wanapaswa kuienzi na kuidumisha iweze kudumu.
“Amani ikitoweka kuirudisha ni kazi, hivyo basi tunapaswa kuienzi na kuhakikisha inadumu vizazi kwa vizazi,”alisema.
Dk. Salim
Waziri Mkuu Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Dk. Salim Ahmed Salim, alisema Watanzania wengi wana hofu kuhusu uvunjifu wa amani hivyo ni lazima hatua zichukuliwe nchi isipoteze sifa ya kuwa kisiwa cha amani, umoja na utulivu.
“Uvunjifu wa amani unatokana na migogoro ya siasa, hali ya uchumi, tofauti za dini na kabila na hata kutotenda haki kwa wote pamoja na kupuuza msingi mkuu wa usawa wa binadamu.
“Hivyo tumeona umuhimu wa kufanya mkutano huu kwa sababu ya wasiwasi walionao Watanzania kuwa tusipochukua hatua zinazostahili sasa taifa letu litapoteza sifa za msingi ambazo zinaifanya Tanzania iwe kisiwa cha amani,” alisema Dk. Salim.
Akitoa mfano wa nchi za Afrika zilizopoteza sifa ya kuwa na amani kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kondo (DRC), Libya, Sudan Kusini, Misri, Somalia, Burkina Faso na Burundi, alisema mifano hiyo inatosha kuwa funzo kwa Tanzania juu ya athari za uvunjifu wa amani.
“Tujifunze kutokana na matatizo yanayowakumba wenzetu. Haya yanaweza kutokea Tanzania kama hatutakuwa makini, viashiria vya uvunjifu wa amani vikiachwa viendelee taifa litaangamia na hakuna atakayepona,” alisema Salim.
Askofu Ngalalekumtwa
Akizungumza katika mkutano huo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, alisema amani ya nchi ni ya kila mtu endapo itavunjika kila mmoja atawajibika kwa nafasi yake.
“Kila mmoja kwa nafasi yake anapaswa kudumisha amani ya nchi, ikiwa tutaruhusu ivunjike hakuna atakayepona, hivyo basi kila mmoja ana wajibu wa kuhakikisha tunailinda na kuidumisha amani iliyopo,”alisema.
Alisema kutokana na viashiria vinavyoonekana hivi sasa ndani ya nchi ni ukweli usiopingika kwamba wananchi wasipokuwa makini nchi inaweza kwenda kubaya.
Alisema kutokana na hali hiyo, wanapaswa kutoruhusu viashiria hivyo viendelee katika jamii bali ni kuikemea na wananchi kuendelea kudumisha amani.
PROFESA SHIVJI
Akizungumzia suala hilo, Mwenyekiti wa Kavazi la Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, alisema imefika wakati kama taifa, watu wajiulize viashiria vya kutoweka kwa amani vimefikaje?
“Tujiulize kama nchi ina viashiria vya kutoweka kwa amani tujiulize tumefikaje hapa na kama tukibaini kuna tatizo ni lazima tuanze kufikiria namna ya kupambana navyo kabla havijatufikisha kubaya.
“Hatuwezi kujifariji kuwa sisi ni kisiwa cha amani wakati leo kuna viashiria vya kuvunjika kwa amani nchini. Ni jukumu letu kama taifa kusimama wote kwa pamoja na kusema hapana kwa wale wanaoweza kutugawa na kuiharibu amani yetu,” alisema Profesa Shivji.
Profesa Lipumba
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema uvunjifu wa amani unatokana na vitendo vya Serikali kutotenda haki kwa wananchi jambo ambalo limesababisha kutoaminika kwa wananchi.
Alisema hadi sasa hakuna uwazi katika uwajibikaji wala utekelezaji wa mambo mbalimbali yanayohusu jamii na taifa kwa ujumla, jambo ambalo limechangia kujitokeza migogoro baina yake na wananchi.
“Serikali imeshindwa kutenda haki kwa wananchi jambo ambalo limesababisha kujitokeza kwa migogoro. Kutokana na hali hiyo serikali inapaswa kuwa wazi na kuhakikisha kuwa inawashirikisha wananchi katika mambo mbalimbali ya taifa na jamii,”alisema.
Profesa Baregu
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Profesa Mwesigwa Baregu, alisema mchakato wa kutafuta Katiba mpya ulikuwa ni fursa ya kuweka mambo sawa lakini umekwama kutokana na matumizi ya ubabe badala ya maridhiano.
“Viashiria vya uvunjifu wa amani vimekuwa ni vingi na tunatakiwa kuangalia tumefikaje hapa tulipo na tunatokaje. Kutafuta Katiba Mpya ilikuwa ni fursa ya kuweka mambo sawa lakini mchakato huo umeenda kwa ubabe badala ya maridhiano na ubabe ni chanzo cha mtafaruko,” alisema.
Mbatia
Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema dhana ya amani imebaki kuwa ni mtaji wa siasa kwa wanasiasa ambao wameishiwa sera huku wanasiasa hao hao wakishiriki kwa njia moja au nyingine katika uvunjifu wa amani.
Alisema amani ya Tanzania haitaweza kudumu endapo hapatakuwapo usawa katika nyanja zote za utoaji wa haki hasa kwa mahakama, polisi, utawala wa sheria na mgawanyo ulio sawa wa rasilimali za nchi.
Butiku
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, alisema lengo la mkutano huo ni kukusanya wadau mbalimbali kujadili viashiria vya uvunjifu wa amani vinavyojitokeza katika jamii.
Alisema mkutano huo unaweza kutoka na mapendekezo ya kuitaka serikali na wananchi nini kifanyike kuhakikisha amani inadumu.
“Katika kipindi hiki kuna viashiria vingi vya uvunjifu wa amani, jambo ambalo linaweza kuwatia hofu wananchi, kutokana na hali hiyo, tumewaalika wadau mbalimbali wakiwamo viongozi wakuu wastaafu, waliopo madarakani, wanasiasa na wadau mbalimbali,”alisema Butiku.
Habari hii imeandaliwa na Patricia Kimelemeta, Michael Sarungi na Jonas Mushi