26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

NCHI HAIWEZI KUJENGWA NA VIJANA WALEVI WA VIROBA

SERIKALI inafanya vizuri na imeendelea na operesheni ya kukagua pombe zinazofungwa katika vifungashio vya plastiki (viroba).

Alhamisi wiki hii katika manispaa za Temeke na Kinondoni mkoani Dar es Salaam ilifunga viwanda vya maghala kutoendelea na uzalishaji, kuuza wala kusambaza pombe hizo.

Kwa upande wa Temeke, kiwanda cha Global Distillers Limited ambacho ni watengenezaji wa pombe kali aina ya viroba kwa jina la Premium Vodka na Ginja, ilifanikiwa kukamata katoni 1,500 na ghala ambalo lilikutwa na katoni 650.

Kwa upande wa Wilaya ya Kinondoni na Ubungo kiwanda cha Kibo Spirit na True Bell navyo vilizuiwa uzalishaji baada ya kukuta pombe hiyo ya viroba ikiwa imesheheni aina ya Kitoko na Rivella.

Tunasema hilo lilikuwa zoezi endelevu lengo likiwa kuhakikisha kuwa agizo la Serikali kutozalisha viroba linatekelezeka kwa wafanyabiashara hao.

Kwamba viwanda hivi vifungwe na kusitisha uzalishaji huo hadi hapo utaratibu mwingine utakapofuatwa, ikiwa ni pamoja na kutumia teknolojia mpya.

Katika Manispaa ya Kinondoni pia ukaguzi ulifanyika katika maghala mbalimbali, ikiwamo Triple S Investment Company Ltd walikokuta vifungashio aina ya Signal true Vodka vyenye ujazo asilimia 100.

Tunasisitiza kuwa viwanda hivi vimechangia katika majanga ya afya kwa sababu vijana wengi, wakiwamo waendesha magari na bodaboda, wanatumia viroba tangu asubuhi kwa sababu ya unafuu wake wa bei na kusababisha ajali nyingi, mbali na kudhuru afya zao.

Si muda mrefu uliopita tuliripoti kuwa kiwanda feki cha kutengeneza pia konyagi feki na bidhaa zake kilikuwa kumegundulika Dar es Salaam baada ya Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla, kuvamia kiwanda hicho.

Kwamba hii ilitokea baada ya Dk. Kigwangalla kwa kushirikiana na Maofisa wa Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Tume ya Ushindani pamoja na Jeshi la Polisi kunasa kiwanda hicho bubu.

Kiwanda hicho kilinaswa kwenye nyumba ya mwanamke anayejulika kwa jina moja la Koku maarufu kwa ‘Mama Kareem’ eneo la Sinza Kijiweni, Dar es Salaam kikitengeneza pombe feki ya konyagi, viroba na pombe kali ya smirnoff.

Katika kiwanda hicho pia kulikutwa mali ghafi mbalimbali zinazotumika kutengenezea bidhaa hizo. Vingine ni dumu la spirit lita 20, chupa tupu na zilizojazwa kwa ajili ya kusambazwa, vizibo vya chupa za konyagi na smirnof pamoja na vifungashio vya aina mbalimbali.

Hivi karibuni mkulima wa Kijiji cha Kingo, Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi alikutwa amefariki dunia ndani ya nyumba yake baada ya kunywa viroba vya konyagi.

Mkulima huyo anadaiwa kunywa pombe hiyo alipokuwa kwenye sherehe kijijini hapo. Tunashauri Serikali ifanye misako mingi nchi nzima kama msako uliofanywa Sinza Kijiweni na kuwakamata wenye viwanda hivi feki.

Tunadhani pia msako ulioanza na unaoshika kasi wa operesheni ya kukagua pombe zinazofungwa kwenye vifungashio vya plastiki (viroba) uendelee hadi viwanda vinavyotengeneza viroba vifikiwe vyote.

Viwanda hivi vinavyotengeneza viroba vinasababisha majanga kwa Taifa. Tunadhani viwanda hivi vifunge vinywaji hivi kwenye chupa kubwa kuliko viroba vyenye bei nafuu kiasi cha kuwavuta vijana wengi kunywa ovyo pombe hizi wakati wowote. Tunasema nchi haiwezi kujengwa na vijana walevi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles