NAVY KENZO HAWATAKI MASIHARA LEADERS CLUB JULAI 22

0
880

Na JUMA3TATA RIPOTA

HAINA shaka kabisa ukiliweka kundi la Navy Kenzo kwenye orodha ya makundi bora yaliyofanikiwa kudumu kwa muda mrefu katika tasnia ya Bongo Fleva.

Linaundwa na wapenzi wawili ambao ni Emmanuel Mkono ‘Nareel’ na Aika Mareale ambao muziki umewapa mafanikio ya kifedha na kisanaa, kiasi kwamba wameanzisha lebo yao ya The Industry inayomiliki wasanii Rose Ree na Wildad.

Julai 22 mwaka huu kundi la Navy Kenzo litadondosha bonge la burudani katika tamasha la kampeni ya ‘Castle Lite Unlocks’ litakatalofanyika kwenye viwanja vya Leaders Club jijini Dar es salaam.

Mmoja wa wasanii wanaounda kundi hilo, Aika anasema kama kawaida yao wamepanga kufanya onyesho kubwa na la aina yake ili kukonga nyoyo za wapenzi wa muziki nchini.

Anasema kuwa wanathamini nafasi waliyopewa kutumbuiza kwenye tamasha hilo na kuwaahidi mashabiki pamoja na waandaaji kufanya kile kinachotakiwa.

“Tunaheshimu nafasi hii adimu ambayo inatupa nafasi ya kuwapa watanzania burudani ya hali ya juu na yenye hadhi ya kimataifa kama ilivyo kawaida yetu Navy Kenzo,” anasema.

Navy Kenzo linafahamika kwa kudondosha pini kali kama vile Kamatia Chini, I Just Wanna, Moyoni, Morning na nyinginezo nyingi.

Tamasha hilo pia litapambwa na nyota wa muziki wa kizazi kipya nchini Naseeb Abdul ‘Diamond Planumz’, Cassper Nyovest wa Afrika Kusini, Vanessa Mdee na rapa maarufu duniani Nayvadius Wilburn ‘Future’ kutoka Marekani.

 Hali kadharika Navy Kenzo wanatarajiwa kulitumia jukwaa la tamasha hilo kama fursa ya kuzidi kupaa kimataifa kwa kufanya onyesho kali na la aina lake litakaloweka historia nchini.

Navy Kenzo ni miongoni mwa makundi ya muziki hapa nchini yanayofanya vizuri kwa sasa wakiwa wanafanya muziki wenye ladha ya aina yake, unaochezeka na kuburudisha watu wa lika zote.

Kuhusiana na tamasha hilo, Meneja Masoko wa TBL Idara ya Kuunganisha Wateja Afrika Mashariki, George Kavishe, anasema tamasha hilo litawahusisha wasanii wengine wa hapa nyumbani ili kunogesha zaidi.

Anasema kuwa tamasha hilo limelenga kuhamasisha wateja wake wa bia chapa Castle Lite kuifurahia zaidi na pia kuwaleta pamoja kupitia tukio hilo kubwa la burudani.

“Uzinduzi huu utafikia kilele chake Julai 22, mwaka huu ambapo kutakuwa na tamasha kubwa Dar es Salaam litakalowapa nafasi wateja wetu kushuhudia wanamuziki wakubwa wa ndani na nje ya nchi, hivyo kuwapa wateja burudani itakayokuwa kwenye kumbukumbu zao kwa muda mrefu,” alisema Kavishe.   

 

Kavishe, anasema kuwa kwa kipindi hicho cha kampeni, zawadi kedekede zitatolewa zikiwemo muda wa maongezi wa simu za mkononi wa zaidi ya shilingi milioni 30 na pia tiketi zaidi ya elfu moja kwa washindi wa droo ambazo zitakuwa zinashindanishwa.

 

Anasema kuwa tayari watu sita wameshinda bahati nasibu ya kampeni hiyo ambapo watapatiwa usafiri na malazi kumwezesha kuhudhuria tukio hilo.

Aliwataja washindi hao kuwa ni Allod Uluga wa Iringa Vijijini, Agness Mlugu (Kigamboni, Dar es Salaam),  Alvin Munuo (Sinza, Dar es Salaam), Ansila Erick (Dar es Salaam), Emilius Fussi (Iringa) na Moses Damian (Dar es Salaam).

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa Afrika Mashariki, Thomas Kamphius, anasema kuwa Tamasha hilo litakuwa ni hitimisho la kampeni ya miezi mitatu iliyozinduliwa wiki iliyopita kwenye Club ya Next Door iliyopo Masaki, Dar es Salaam ya 'Castle Lite Extra Cold Unlocks.

“Kampeni ya 'Castle Lite Unlocks' imekuwa kwenye harakati za maandalizi kwa miaka michache sasa, ambapo Castle Lite imebadili mfumo wa kawaida uliozoeleka kwa kuwaleta wasanii wa ngazi ya juu ili kuburudisha  ukanda wa pwani ya Afrika kwa maonesho yaliyo na uzoefu wa ‘Extra Cold’ katika kilele cha tamasha ‘Castle Lite Unlocks’,” anasema Kamphius.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here