24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

NATAMANI BALOZI SERGEY KISLYAK ANGEWAKILISHA NCHI YETU-II

Balozi Sergey Kislyak

 

 

Na MARKUS MPANGALA,

JUMAPILI iliyopita nilielezea juu ya sakata linaloendelea katika Serikali ya Donald Trump. Nilisema juu ya kujiuzulu kwa mshauri wa masuala ya usalama wa Serikali ya Trump, Michael Flynn.

Aidha, nilibainisha chanzo ni mwanadiplomasia Sergey Kislyak. Nilisema ni yeye amesababisha malumbano huko White House na kibano kikali alichokutana nacho Flynn kilimfanya akiri kufanya vikao na Kislyak.

Nikaongeza kuwa, anayefuata ni Jeff Sessions, ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Marekani aliyetangaza kujitoa kwenye uchunguzi wa sakata la iwapo timu ya kampeni ya Trump ilisaidiwa na Serikali ya Russia.

Nilitumia mfano huo kuonyesha umahiri wa Sergey kama balozi mwenye uwezo mkubwa. Zaidi anatajwa kuwa jasusi aliyebobea kwenye fani yake, akiwa mvumbuzi wa vipaji vipya vya ujasusi nchini kwao.

Kutokana na sakata linaloendelea nchini Marekani, ndipo nikahuisha na uteuzi wa mabalozi wetu hapa nchini. Nikasema mbali ya Adadi Rajab, ambaye kitaaluma anafahamika kuwa mmoja wa mashushushu wazuri waliopata kutokea, lakini bado tunakabiliwa kuwapata mabalozi wenye haiba kama Sergey, Adad au Bernard Membe.

Kusema hivyo sikusudii kubeza mamlaka ya uteuzi wala wateuliwa, badala yake naamini kunatakiwa kushonwa upya suti ya uteuzi wa mabalozi pamoja na uvumbuzi wa vipaji vya kuitumia Idara ya Usalama hapa nchini (TISS).

Inapofika mahali mtu anayefanya kazi TISS anakuwa mwepesi kujitambulisha kwa wananchi wa kawaida, linakuwa tatizo. Vilevile inapofika mahali tunawachukua ndugu, marafiki au watu wenye uhusiano wa maofisa usalama wetu ili wawe watumishi wa idara hiyo bila kuzingatia uwezo, vipaji na umahiri katika kuzisoma nyakati, mazingira na kadhalika, linakuwa tatizo kubwa zaidi.

Aidha, unapofika mahali tunakuwa na watu kwenye idara nyeti ambao hawawezi hata kumaizi mtaa wanaopita kwa mara ya kwanza, hilo ni tatizo. Binafsi ninaamini kuwa, uteuzi wetu katika balozi mbalimbali kote duniani tunatakiwa kufanya juhudi kubwa kuhakikisha maofisa usalama wetu wanakuwa sehemu au ndio wawakilishi wetu kama walivyo akina Sergey wa Serikali ya Putin.

Ni jambo la kushangaza mtu timamu ashindwe kujiuliza kwanini tangu mwaka 2008 hadi leo Sergey Kislyak amekuwa balozi wa Russia nchini Marekani bila kubadilishwa. Huo ni ujumbe kwetu. Sakata linaloendelea ni matunda ya kazi yake na manufaa kwa wananchi wa Russia kama nilivyoeleza wiki iliyopita.

Kwa muktadha huo, ninakubaliana na mhadhiri mmoja wa Chuo Kikuu (jina nalihifadhi) ambaye nilinukuu mawaidha yake wiki iliyopita kwamba idara na balozi zetu hazina ushindani wa kiuchumi, maendeleo, teknolojia wala ujasusi wa kibiashara ambao ungeliweza kulinufaisha taifa letu.

Yeye alisisitiza kuwa, ujasusi wa kibiashara ni jambo ambalo linatakiwa kuwa ajenda ya msingi katika balozi zote kwa kushirikiana na TISS, ili kuwashinda washindani wetu kokote duniani.

Aidha, katika hoja hiyo nilijadiliana naye juu ya umahiri wa Bernard Membe katika fani hiyo pamoja na ufanisi wake kwenye balozi (angalau kwa kiwango kidogo).

Rafiki yangu huyo aliniambia: “Nimekusoma unachomaanisha juu ya Bernard Membe, ila cha kushangaza yeye anaijua hiyo kazi, alikuwa ndo bosi wa Balozi zetu kwa miaka 8 kama sikosei. Nashangaa naye aliendelea kuona watu wanakuwa ‘assigned’ tu kwenye balozi zetu. Sijui nini kilikuwa kinamkaba. Akiwa Wizara ya Mambo ya Nje, tena mzoefu wa ujasusi na hasa kwenye balozi, tulitegemea alikuwa na ‘power’ kubwa ya ku-shape aina ya mabalozi na waambata wao kwenye balozi zetu. ‘Let's hope’ mambo yatakuja kubadilika huko mbeleni.

“Japo hata sasa Membe ni ‘experienced spy’. Sijui nafasi yake katika kufanya ‘restructuring’ ya balozi zetu. Na hasa ukaribu wake na DG (mkurugenzi) wa sasa (Modestus Kapilimba) na mtizamo wake juu ya mabadiliko ndani ya hizo balozi”.

Muktadha huo unatuletea mantiki kuwa, mwenendo wa uteuzi wa mabalozi wetu na waambata bado umekuwa wenye mtazamo wa kichama. Mtazamo huo ndio unaathiri ufanisi wetu katika Nyanja hiyo.

Ninaamini licha ya kuwa na matunda tuliyopata, bado kiu yangu haijakatwa na matamanio ya kushinda yamekuwa makubwa sana. Mara kadhaa nimeona kampuni za Kenya zikitupiga dafrao kwenye taasisi zetu na kulazimika kuwakodisha ili waziendeshe.

Sitazitaja taasisi hizo, lakini tumezikodisha kwasababu si kwamba tumeshindwa kuziongoza, bali wao walichofanya ni ujasusi wa kibiashara ambao wamefanikiwa kudhoofisha mizizi iliyotupatia ubora husika.

Chukulia kwa mfano, unaanzisha kampuni fulani ya bia halafu inapiga hatua na kuuza bidhaa zake hadi nchi jirani. Lakini ghafla bia hizo zinapotea kwenye soko na kudidimia kabisa. Kisha kampuni nyingine ya bia iliyokuwa ikishindana na kampuni yako huko ugenini inakuja hapa nchini na kuinunua ili iendeshe biashara ileile.

Kwa mtu timamu anaelewa kuwa kuna kuzidiwa ujasusi wa kibiashara. Chukulia mfano mwingine, unamiliki kampuni ya ndege hapa nchini, halafu unafanya ushindani katika soko la nchi jirani, ikawa imekua kwa kasi sana na kupata faida zaidi kuliko ndege za nchi husika.

Miaka kadhaa baadaye kampuni yako ya ndege inadhoofika kisha kuelekea kufilisika, lakini yule mshindani wako katika biashara ya ndege anakuja na kuikodi kampuni yako hiyo ili aiendeshe.

Jambo la ajabu zaidi, anapokodi hiyo kampuni ya ndege anaididimiza na kusababisha inapoteza soko lake ililojijengea, licha ya ahadi lukuki za kuboresha na kupanua shughuli zake wakati akinunua ili kuwekeza.

Hii ina maana mshindani wako alikuwa akifanya ujasusi wa kibiashara na hila ambazo zilichangia kampuni yako kudhoofika kabisa. Baada ya kuinunua na kuimiliki, maana yake anakuwa na mamlaka ya kuifutilia mbali katika uso wa dunia, na ndivyo inavyotokea.  Hilo si jambo la kawaida na halina tafsiri kibiashara pekee, hata ujasusi wa kibiashara ni biashara pia.

Aidha, kampuni yako ya bia nayo inadhoofishwa nchi jirani na kujikuta inapoteza kabisa soko la bidhaa zako, lakini mshindani wako anapokuja kuomba kuwekeza kwa mlango wa nyuma (kutumia menejimenti nyingine yenye uhusiano nayo) anatoa sharti ni marufuku bia hizo kuuzwa katika nchi anakotoka.

Mambo kama haya yanatakiwa kujulikana kwa balozi zetu na suala zima la ujasusi wa kibiashara na uchumi unaozidi kuota mizizi kila kukicha. Ni matarajio yangu mifano hii michache itawazindua wahusika juu ya ukweli wa udhaifu wa balozi zetu na mwenendo wetu usioridhisha wa idara zetu za usalama.

Baruapepe; [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles