24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Nasari: Nimehamia CCM kwa sababu Magufuli amerudisha mashamba

JANETH MUSHI -ARUSHA

ALIYEWAHI kuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari na Willy Qambalo aliyekuwa Mbunge wa Karatu, kwa tiketi ya Chadema, wametangaza kuhamia Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wakidai kuvutiwa na miradi ya maendeleo iliyofanywa na Rais Dk. John Magufuli na kuwa amefanikiwa kurudisha ardhi iliyokuwa mikononi mwa wawekezaji.

Nassari akizungumza mara baada ya kupokewa na Mwenyekiti wa UVCCM, Henry James, alisema hakuwahi kuwaza iko siku atasema “CCM hoyeee” na kuwa baada ya kutafakari kwa muda ameamua kuhamia chama hicho.

Alisema yako mengi ya kusema na kuwa wenye shauku ya kumsikia ni wengi ila huu ni mwanzo wa safari na mengi zaidi ataendelea kuyasema siku za mbeleni.

Nassari alisema moja ya sababu iliyomfanya kuhama upinzani ni baada ya kuona Rais Magufuli ametekeleza yote aliyokuwa akiyapigania ikiwemo kurudisha ardhi kwa watu wa Meru aliyokuwa akiipigania kwa muda mrefu.

Alisema mbali na hilo, Rais Magufuli amekuwa kiongozi wa mfano wa kuigwa barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Nassari alisema nafsi imemwambia ajiunge CCM, marafiki waliomchangia, ndugu na jamaa wote wamemshauri jambo hilo na ameamua kujiunga mchana kweupe.

 “Leo nimekuja rasmi mchana kweupe na niliwaambia siku naenda CCM sitaenda usiku wala alfajiri, kwa sababu  moja tu, ninachokifanya ni suala ambalo liko wazi na lina mwanga, siyo bahati mbaya.

“Sijaja hapa kuongea nanyi kwa sababu kuna kitu nataka, ni kwa sababu naipenda nchi yangu, nimekuwa na mzigo wa kuchangia jamii yangu. Wengi wanawaza ubunge, sijatangaza nia mahali popote, sijaja kutangaza nia,” alisema Nassari.

Aiishukuru Chadema kwa kumlea na kumsaidia kuwa mbunge akiwa katika umri mdogo.

“Nimekuja mchana kweupe kushukuru kwa moyo wa dhati chama changu kwa kunilea na kunifikisha hapa nilipo, nawaambia asante sana, lakini roho yangu inakataa kuendelea kubaki huko na kupinga yanayofanywa na Rais wangu.

 “Kuna kitu kilikuwa kinanihukumu ndani yangu, kinaniambia nilipo sitafika na ninawashukuru watu wa Meru na Watanzania wengine.

“Pengine wako ambao wamekwazwa na hatua yangu hii ya kuondoka, ila nimebishana na nafsi yangu kwa muda mrefu nimeshindwa.

“Wameru wana usemi kuwa unapokunywa maziwa huangalii yametoka kwa ng’ombe mwenye rangi gani, nimekaa Meru na nyie ni mashahidi sikuwa mbunge lelemama, nilipambana kuhakikisha watu wangu wanarudishiwa ardhi yao.

“Kuna mashamba kama kule Valeska niliyopigania turudishiwe toka mikononi mwa wawekezaji waliojitwalia ardhi yetu, Rais amerudisha na sasa ni ardhi ya wananchi wa Meru, sasa nampinga ili iweje?” alisema.

Alisema tangu akiwa kijana mdogo alikuwa na kiu ya kusaidia jamii ya Meru ambapo akiwa chuo mwaka 2008 alisaidia upatikanaji wa ‘laptop’ katika jimbo lake, hivyo ameona ni vema kuungana na CCM ili kusaidiana kwa karibu kuendeleza taifa la Tanzania.

“Naamini baada ya kuungana nanyi, Watanzania wataendelea kunywa maziwa bila kujali yametoka kwa ng’ombe wa rangi gani, lakini kweli hata kuendelea kupingana  na Rais Magufuli ni kukosa la kupinga sababu kila nilichopigania amekifanya,” aliongeza Nassari.

 Kwa mujibu wa Nassari, Rais Magufuli anastahili kupongezwa jimboni huko kwani mbali na miradi ya maendeleo, ameweza kuipandisha hadhi Shule ya Kata ya Kisimiri Juu kuwa ya kipaji maalumu na kuboreshwa.

Alisisitiza kuwa kuingia kwake katika siasa haikuwa kwa bahati mbaya au kuwa mwanasiasa  pekee, bali kutaka kuona taifa linasonga mbele kwa maendeleo na kupiga hatua  zaidi.

“Haijalishi ukinywa maziwa ni ya ng’ombe gani au wa rangi gani, cha msingi unakunywa maziwa, leo itoshe kusema haya ila wakati ukifika nitasema, yapo mengi ya kusema, yale yote mnayoyataka kusikia toka kwangu mtaendelea kusikia na kuyaona,” alisema Nassari.

 Aliongeza kuwa ameshaandika barua kwa chama chake ya kutangaza uamuzi wa kuhama na kuwa ameambatanisha na kadi yake.

Kwa upande wake, Qambalo alisema  wamekutana na Nassari katika eneo hilo na kwamba hawakupeana taarifa na kila mtu anaona kilichofanywa na Rais Magufuli.

“Wengine wanaweza kusema tulipanga hili na Nassari, hapana. Tumekutana hapa na nilipomuona nimemuuliza hata wewe? Nimefanya uamuzi huu bila kushawishiwa na mtu yeyote, nimeangalia sera za CCM ni za kuwaletea wananchi maendeleo,” alisema Qambalo.

Alisema mwenye macho yanaona, pua zinanusa na ngozi inapata hisia, hivyo naye amenusa amepata hisia, bila kushawishiwa na mtu yeyote ameamua kuja CCM, ili akienda bungeni akakae upande wa kushangilia na siyo ule upande wa upinzani wa kununa na kuguna.

MWENYEKITI UVCCM

Awali Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Kheri alisema vijana wa jumuiya hiyo nchi nzima wamejipanga vema kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ikiwa ni pamoja na kumuunga mkono Rais  Magufuli.

Kheri alisema mwaka huu wa uchaguzi CCM ikiwemo na jumuiya zake imejiandaa kuhakikisha wanaeleza ubora wa chama chao na wako tayari kukabiliana na chama chochote na mgombea kutoka chama chochote.

Alisema katika uchaguzi wa mwaka huu hawajaona mtu wa kushindana naye na kuwa yeyote atakayeteuliwa na chama wao kama vijana watamuunga mkono, kumpigania hadi ashinde na kuwa utayari wa vijana wameuonyesha kupitia kumdhamini mgombea urais,  Dk. Magufuli.

Kheri alisema suala la kuhama chama ni haki ya kila mtu huku akitolea mfano wa baadhi ya makada wa CCM waliowahi kuhama chama hicho na kwenda upinzani, akiwemo aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles