30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

NASA YARUHUSIWA KUKAGUA MITAMBO YA UCHAGUZI

Nairobi, KENYA

MAHAKAMA Kuu nchini Kenya imekubali muungano wa upinzani National Super Alliance (NASA) kukagua mitambo ya kompyuta iliyotumika na  Tume ya Uchaguzi (IEBC) wakati wa uchaguzi Agost 8 mwaka huu.

Pia imeruhusu NASA kusoma data kwenye kompyuta hizo chini ya uangalizi ili kuhakikisha usalama wa mitambo ya IEBC haihujumiwi.

Hatua hiyo imekuja baada ya NASA kufungua kesi ya kupinga matokeo ya ushindi wa Rais Uhuru Kenyatta wa chama cha Jubilee.

Muungano huo unaoongozwa na Raila Odinga, ulipinga matokeo ya kura za urais nchini humo kutokana na kile wanachodai kuwa kulikuwemo vitendo vya udanganyifu katika mchakato nzima wa uchaguzi.

Baada ya kuanza kusikiliza kesi hiyo jana, mahakama hiyo ilitoa ruhusa kwa Nasa kukagua mitambo ya kompyuta iliyotumika na Tume ya Uchaguzi (IEBC) wakati wa uchaguzi Agost 8 mwaka huu.

Wanasheria wa Odinga wameruhusiwa na mahakama hiyo kusoma data kutoka kwenye mitambo ya kompyuta hizo kwa kufanya uchunguzi wa uchaguzi uliofanyika wiki mbili zilizopita.

Jaji wa Mahakama hiyo,¸Isaac Lenaola alisema NASA itapata utambulisho wa mitambo ya kompyuta zilizotumiwa wakati wa uchaguzi pamoja na nywila zilizotumiwa kuingia katika mitambo hiyo.

Aidha, upinzani utaweza kupata taarifa kuhusu yaliyojiri katika mitambo hiyo ya uchaguzi kuanzia Agosti 5 hadi kufikia jana. Pia wataruhusiwa kusoma nakala za fomu za matokeo katika vituo vya kupigia kura na ngazi ya maeneo bunge (Fomu 34A na 34B) ambazo zilitumiwa kutangazia matokeo.

Taarifa kuhusu mchakato wa upinzani kupekua mitambo hiyo ya IEBC itawasilishwa kwa mahakama hiyo leo jioni.

Majaji saba wa mahakama hiyo ya juu wameanza kusikiliza kesi hiyo iliyowasilishwa na Raila Odinga (mgombea urais wa NASA).

Utofauti wa fomu

Mwanasheria wa NASA, Otiende Amollo ameishutumu  IEBC kwa kuchezea Fomu namba 34A na B akisema kwamba baadhi ya fomu zilisainiwa na maafisa wa uchaguzi ambao sio wahusika.

“Katika majimbo 13 jumla ya kura 598,476,  fomu zake zilisainiwa na maafisa ambao si wahusika. Fomu nyingine hazikuwa na Barcodes (feki) na nyingine zilionyesha zinatoka nje ya Kenya.

“Pia fomu nyingine zilikuwa na mpangilio tofauti unaoonesha kuwa haukuchapishwa na Kampuni ya Al Ghurair ya Dubai, ambayo ilipewa zabuni ya kuchapisha karatasi za kura,” alisema Amollo.

Amollo alisema matokeo ya vituo vyote vya kupigia kura  ambavyo vilisainiwa na maafisa ambao hawahusiki matokeo yake yanapaswa kufutwa.

Pia anasema kulikuwa na makosa katika kuonesha matokeo ambapo makosa hayo yalifanywa kwa makusudi. IEBC ilitangazaje mshindi wakati hawakuwa na fomu zote namba 34A?” alihoji.

“Kwa hiyo matokeo hayakuwa kulingana na fomu namba 34A wala fomu 34B, fomu hii ilikuwa imeandikwa kura milioni 7 ,” alisema.

Awali IEBC ilitupilia mbali madai ya NASA, ambapo mfumo wa ukusanyaji matokeo wa IEBC ulidukuliwa kubadili matokeo.

Tume hiyo ilikanusha kuwa mfumo uliotumiwa na IEBC kukusanya matokeo na kuyatangaza haukudukuliwa kama ilivyodaiwa na upinzani na kwamba baada ya uchunguzi wao wa ndani wamejiridhisha kuwa mfumo wao haukuingiliwa.

kura zilizoharibika

Amollo alibainisha kuwa upo uwezekano mgombea urais wa Jubilee alipewa kura zilizoharibika, kwani wakati Mwenyekiti wa IEBC anatangaza matokeo, hakuwaambia Wakenya idadi ya kura zilizoharibika katika majimbo ya Murang’a, Samburu West, Soi, Narok North, Nyali, Roysambu, Ruaraka na Embakasi.

Karatasi za kura

Mwanasheria anayeongoza jopo la mawakili wa NASA, James Orengo anadai kuwa karatasi za kupigia kura zilizotumiwa katika uchaguzi wa rais wa Agosti 8 hazikuchapishwa na Kampuni ya Dubai kama IEBC inavyodai.

Orengo alisema uchambuzi wa karatasi za kura zilizotumiwa katika uchaguzi ulionesha kwamba karatasi hizo zilikuwa na upungufu wa usalama wa kisheria, wakidai kuwa zilichapishwa nchini Kenya.

Kwa upande wa serikali wakili kiongozi wa IEBC, Paul Muite aliiambia mahakama hiyo kuwa Wakenya walifanya maamuzi yao na uchaguzi ulizingatia Katiba.

“Ni vigumu kuiba kura vituoni na wasimamizi wa uchaguzi waliridhika na uchaguzi ulivyofanyika,” alisema Muite.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles