22.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 18, 2021

NAPE,KITWANGA WAGEUKA

Na Mwandishi Wetu,

MAWAZIRI wa zamani, Nape Nnauye na Charles Kitwanga, wamegeuka kuwa mwiba kwa kutoa hoja za kukosoa utendaji wa Serikali ya Rais Dk. John Magufuli.

Mwenendo wa makada hao wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuikosoa Serikali, umeanza kuibuka siku za hivi karibuni baada ya wote kwa nyakati tofauti kuenguliwa katika nafasi zao za uwaziri.

Kwa hatua yao ya sasa, wanasiasa hao wanadhihirisha ukweli kwamba wabunge wengi hushindwa kueleza matatizo ya majimbo yao pindi wanapopewa nyadhifa serikalini na wanapotenguliwa wanadai wanapata nafasi zaidi za kuwatumikia wapigakura wao.

Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wa siasa wanadai kuwa makada hao walikosa ujasiri wa kuikosoa Serikali walipokuwa wanashikilia nyadhifa zao kutokana na kubanwa na hoja ya uwajibikaji wa pamoja.

NAPE

Nape ambaye alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kabla uteuzi wake kutenguliwa Machi, mwaka huu baada ya kupokea ripoti ya tukio la kuvamiwa kwa Kituo cha Televisheni cha Clouds, amesikika mara kadhaa nje na ndani ya Bunge akiikosoa Serikali.

Akiwa jimboni kwake Mtama alikoenda kuzungumza na wapigakura wake baada ya kutenguliwa, alisema kama matukio ya kuteka watu yataachwa yaendelee, basi CCM itakuwa na kazi ngumu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

Nape alitoa kauli hiyo wakati huo kukiwa na tukio la kutekwa kwa msanii wa muziki wa kizazi kipya, Ibrahim Mussa maarufu kwa jina la Roma Mkatoliki.

Wakati akichangia hotuba ya makadirio ya Bajeti ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji wiki iliyopita, Nape alisema kuwa

kama CCM isipotekeleza Ilani ya Uchaguzi ya mwaka 2015 kwa kutowapatia maji wananchi, inaweza kuondoka madarakani.

Kauli nyingine ya Nape aliitoa wiki hii alipokuwa akichangia bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, aliposema kuwa wananchi wa mikoa ya Kusini hawatakubali kuona ujenzi wa kiwanda cha mbolea Lindi unakwama kutokana na kile alichodai vita iliyopo kati ya mataifa makubwa.

Aliitaka Serikali isikubali kuona vita hiyo inaendelea kuwaumiza wananchi hao na kuongeza kuwa kama itashindwa kusimamia, wao hawatakubali.

Pia kupitia kurasa zake za mtandao wa kijamii wa twitter, Nape, amekuwa akiandika baadhi ya kauli zenye mwelekeo wa kuikosoa Serikali

KITWANGA

Kitwanga aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi alianza kuikosoa Serikali baada ya kutenguliwa mwaka jana, kutokana na ununuzi wa ndege mbili mpya aina ya Bombardier kutoka Canada ili kufufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

Alisema ndege hizo, si tu hazina mwendo, lakini pia ilikuwa ni ajabu kununuliwa kwa fedha taslimu wakati duniani kote ndege hununuliwa kwa kulipa kidogo kidogo wakati mteja akiendelea kuzitumia.

Kitwanga aliibuka tena wiki iliyopita wakati akichangia Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Maji na Umwagiliaji Gerson Lwenge kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, akisema atawahamasisha wapigakura wake wakazime mtambo ulioko katika chanzo cha maji cha Iherere.

Alisema jimboni kwake hakuna maji ya uhakika na tangu mwaka 2008 wananchi wamekuwa wakiyasubiri bila mafanikio.

“Kwa hiyo, nitakachokifanya safari hii, sitatoa shilingi kwenye bajeti, bali nitakwenda kuwahamasisha wananchi wa Misungwi wapatao 10,000, twende tukazime mtambo katika kile chanzo cha maji ili wote tukose.

 “Mshukuru nilipokuwa waziri nilikuwa siwezi kusema kitu, sasa nimetoka, tutapambana kwa sababu lazima tuwe na mipango mizuri ya kuwapelekea wananchi wetu maji kama inavyofanyika katika umeme kupitia REA (Wakala wa Umeme Vijijini),” alisema.

Kauli hiyo iliibua hasira za Waziri Lwenge wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/2018, ambaye aliita kuwa ni sawa na uasi.

Kutokana na kauli hiyo, alimtaka ahame chama kama haoni jitihada za kupeleka maji jimboni kwake zinazofanywa na Serikali.

“Kitwanga anaposema atakwenda kuhamasisha wananchi wakabomoe mtambo wa Iherere maana yake analeta uasi au hathamini kazi iliyofanywa na chama chake?

“Kama ni hivyo, sasa ajitoe kwenye chama kwa sababu Serikali imepeleka fedha na kwa maendeleo yaliyofanyika, ni lazima tuwahamasishe wananchi kutunza miundombinu iliyopo badala ya kwenda kuibomoa.’ alisema.

KAGASHEKI

Mbali na kina Kitwanga, baadhi ya waliokuwa mawaziri katika Serikali ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete nao pia wamegeuka kuwa wakosoaji wa Serikali.

Mmojawapo ni aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, anayeikosoa Serikali kupitia akaunti yake ya twitter.

Kagasheki aliyeangushwa katika ubunge wa Bukoba Mjini na mpinzani wake wa siku nyingi, Wilfred Lwakatare (Chadema), aliwahi kusema kuwa kama nguvu ya Ukawa ingemchagua mgombea makini, basi CCM ingekuwa na kazi ngumu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.

Kada huyo wa CCM aliyejiuzulu nafasi yake kutokana na sakata la Operesheni Tokomeza, aliwahi kuandika katika ukurasa wake wa twitter: “Kuikosoa Serikali yoyote ile ni jambo la kawaida. Ni vema kuchagua maneno na kulenga hoja bila matusi.”

MULUGO

Naye Philip Mulugo aliyekuwa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakati wa utawala wa Kikwete, pia amekuwa akiikosoa Serikali ya Magufuli.

Mulugo ambaye kwa sasa ni mbunge wa Songwe, amesikika bungeni wiki iliyopita akiikosoa Serikali alipochangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi.

Akichangia bajeti hiyo, Mulugo aliishangaa Serikali kuruhusu vitabu vyenye makosa vitumike shuleni wakati kuna uwezekano wa kuviondoa.

Katika maelezo yake, Mulugo alivitaja vitabu vya jiografia vya kidato cha tatu na kiingereza kidato cha nne, kuwa vina makosa yanayoweza kuharibu misingi ya wanafunzi.

“Haiwezekani mbili mara mbili mtu aseme ni sita wakati sisi tunajua ni nne. Kwa hiyo, hili suala la vitabu mliangalie vizuri kwa sababu haliko vizuri,” alisema Mulugo.

Pamoja na hayo, Mulugo alizungumzia michango inayotozwa na Serikali katika shule binafsi na kusema ni mingi na kwamba inatakiwa kupunguzwa kwa kuwa inawakatisha tamaa wamiliki wa shule hizo.

WAPINGWA

Kutokana na mwenenedo wa mawaziri hao wa zamani, Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) alionyesha kushangazwa na kuamua kuwalipua bungeni.

Wakati akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Maji, Msukuma alisema: “Nilisikitika sana na nataka niwaulize kwamba, nyinyi mawaziri wa Magufuli hivi vile viapo mnavyokula mnajua maana yake?

“Kama hamjui maana ya hivi viapo, basi sina hakika kama mko sawasawa na kama hamko sawasawa, Ndalichako (Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi), hebu pitisha operesheni ya vyeti feki huenda hapa penyewe kuna feki za kutosha.

“Hivi inawezekana vipi mtu uliyekuwa waziri unasimama hapa na kusema ulipokuwa waziri ulikuwa umebanwa kuzungumza na baada ya kufukuzwa sasa uko huru kuzungumza?”

Naye, aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara wakati wa utawala wa Kikwete, Dk. Cyril Chami, amewafananisha wabunge wa CCM ambao ni vinara wa kuikosoa Serikali kuwa ni kama mke anayetoa siri za ndani ya nyumba yake na mumewe.

Akizungumza na MTANZANIA Jumapili hivi karibuni, Dk. Chami aliyekuwa Mbunge wa Moshi Vijijini, alisema mbunge anapokuwa waziri anakuwa na nafasi nzuri ya kupata fursa na nyenzo za kuwatumikia wapigakura wake.

 “Ukiwa waziri una nafasi ya kuwasiliana na waziri mwenzako anayeshughulikia kwa mfano maji. Inakuwa rahisi zaidi kuliko kupiga kelele bungeni. Unajua kupiga kelele sio lazima kwamba mbunge huyo anafanya kazi na hasa ukiwa mbunge wa chama kinachounda Serikali hutarajiwi kuongea kila kitu hadharani.

 “Sisi tunafuata mtindo wa Westminster (Uingereza). Waziri hatarajiwi kuikosoa Serikali ambayo yeye ni sehemu yake.

“Kama waziri husika ana dukuduku lake kuhusu wapigakura wake jimboni, basi anayo nafasi ya kulisema kwenye Baraza la Mawaziri, kumuona Waziri Mkuu au hata rais mwenyewe.

“Hata ukiwa mbunge una jambo kubwa, basi unayo nafasi ya kulizungumza kwenye mkutano wa wabunge wa CCM,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Chami ambaye alipoteza kiti chake cha ubunge katika uchaguzi wa mwaka juzi, alisema mbunge anaweza kuikosoa Serikali ya chama chake, lakini ajue akivuka mipaka anajipotezea sifa za kuwa mbunge wa CCM.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa CCM (Bara), Rodrick Mpogolo, alisikika hivi karibuni akisema kuwa chama hakina muda na wabunge wanaoikosoa Serikali.

Mpogolo alisema wabunge hao watambue kuwa CCM ni kubwa kuliko wao.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,215FollowersFollow
521,000SubscribersSubscribe

Latest Articles