Na RAMADHAN HASSAN – DODOMA
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, Nape Nnauye amesema wanasiasa wanatakiwa kuweka akiba ya maneno.
Juzi, Nape alitangaza kujiuzulu nafasi hiyo ingawa hadi sasa haijaelezwa sababu za uamuzi wake huo.
Alikuwa akizungumza bungeni jana jioni wakati akichangia taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kipindi cha Januari 2018 hadi Januari 2019.
Nape alisema wakati mwingine watu wanasema mambo mengi na wanatakiwa kuangalia maneno wanayotakiwa kusema kwa wababu wanatakiwa kuweka akiba ya maneno.
“Kwa hiyo wakati mwingine tunapolishwa maneno na kuanza kusema, wekeni akiba ya maneno juu ya nani anapinga nini na nani anasema nini, itatusaidia sana wanasiasa, ni vizuri tukiweka akiba ya maneno.
“Kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Mtama, naomba nimshukuru Mheshimiwa Rais na hapa nataka tujifunze kidogo kuweka akiba ya maneno hasa tunaposhutumiana bila sababu.
“Mheshimiwa Rais (John Magufuli) wakati wa uchaguzi, sisi wa Jimbo la Mtama tulipeleka maombi ya kufuta baadhi ya mashamba makubwa yaliyotelekezwa. Namshukuru Rais, namshukuru Waziri wa Ardhi (Lukuvi), moja ya shamba lililofutwa ni shamba namba 37 liko Mahumbika, Mtama Mkoa wa Lindi.
“Aliyelipeleka kuomba lifutwe ni mimi Mbunge, nilimpelekea Waziri, Waziri akapeleka kwa Rais, Rais akafuta.
“Nataka niwaombe wenzangu, kwanza nimshukuru Waziri na nimshukuru Rais kwa kulifuta hili shamba kwa niaba ya wakulima, sasa tutakwenda kuligawana vizuri,” alisema Nape.