Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kuwa wizara yake pamoja na wadau wa habari wanaamini kuwa mapendekezo waliyokubaliana ndiyo yaliyopelekwa bungeni.
Waziri Nape ametoa kauli hiyo juzi wakati akifanya mahojiano katika kipindi cha Dakika 45 kinachorushwa na kituo cha ITV ambapo alisema kuwa kwa sasa tasnia ya habari imetulia na watu wana uhuru wa kufanya kazi zao.
“Bahati nzuri mchakato wa kufanya mapendekezo ya Sheria ya Habari tulikaa vikao zaidi ya vitatu na pande zote, tulivutana lakini baadaye tulielewana hivyo tunaamini tulichokipeleka bungeni.
“Hata hivyo, bado kuna nafasi ya wanahabari kusema kuhusu yale tuliyokubaliana kwani bunge litawaita, upande wetu Serikali tutakuwa na wajibu wa kujibu kama kutakuwa na mahali tumetofautiana na mwisho wa siku mtunga sheria ni Bunge, lakini kiujumla mchakato wa mabadiliko ya sheria ya habari umekwenda vizuri.
“Mimi naamini uhuru wa habari upo nchini isipokuwa unapaswa kuendelea kuimarishwa ndiyo maana tunapeleka sheria bungeni ili uhuru unaotolewa tuuimarishe kwa sheria sababu kwa sheria iliyopo vipo vyombo vya habari visingepaswa kuwepo,” amesema Nape.
Aidha, akifafanua zaidi kuhusu mabadiliko hayo Nape amesema kuwa: “Sheria ilisomwa bungeni na tunategemea itasomwa tena kwenye bunge lijalo kwa mara ya pili. Ikisomwa kwa mara ya kwanza inakuwa ni nyaraka ya umma, wanapewa kamati ya Bunge na wadau wanaujadili.
“Tunategemea kwenye Bunge lijalo itajadiliwa na ilisomwa kwa mara ya kwanza baada ya majadiliano na wanahabari,” amesema Nape.