27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

NAPE: NITAWASILISHA RIPOTI KWA RAIS

Na Waandishi Wetu – Dar es Salaam

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amesema atawasilisha ripoti ya kamati hiyo kwa Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais kwa hatua zaidi.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa ripoti hiyo, Nape alisema Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais ndiyo mamlaka yake ya juu hivyo kama kutakuwa na lolote wao ndio wenye uamuzi.

 “Nimeipokea ripoti, kazi hii si rahisi ina gharama kubwa, hasa katika kusimamia haki na ukweli, juu yangu kuna Waziri Mkuu, Makamu wa Rais na Rais, ndio wakubwa zangu.

“Nitakabidhi taarifa kwao wataisoma, kama kuna maeneo ya kutoa ushauri ama maelekezo watafanya wao,” alisema Nape.

Alisema Serikali inathamini uhuru wa vyombo vya habari kwa sababu wanaamini Tanzania yenye mafanikio inahusisha pia wanahabari.

“Ninyi (wanahabari) ni sehemu muhimu katika kujenga Tanzania ya viwanda, ujenzi wa Tanzania yenye uchumi wa kati na mafanikio ya sera zote alizonazo rais, hivyo tumuunge mkono katika nia yake njema kuhakikisha Tanzania inaendelea kuwa eneo jema kwa kila mtu. 

“Rais ana nia njema na tasnia ya habari na Watanzania wote, nina imani wanahabari na dunia kwa ujumla itakuwa imetuelewa. Madhaifu yakitokea kwa mtu mmoja hayawi tope kwa Serikali nzima,” alisema Nape.

Waziri huyo pia alisema ni vizuri viongozi wakajenga utaratibu wa kuwasilikiza wananchi na kuacha kiburi kwani wanalipwa kwa kodi za wananchi.

“Sisi wengine tuliopewa dhamana ya kuwatumikia watu ni vizuri kuwa wanyenyekevu, tunalipwa kwa fedha za walipakodi na hawa wavuja jasho wa kawaida, tutapata baraka kwa Mwenyezi Mungu na tutakuwa tunawatendea haki Watanzania waliotuchagua.

“Wanasiasa tujifunze kuwa na ngozi ngumu wakati mwingine na kuheshimu mipaka ya kazi zetu. Mwalimu Nyerere alisema kujikosoa na kujisahihisha si ishara ya udhaifu bali ishara ya uimara na kujirekebisha na kusonga mbele,” alisema Nape.

Waziri huyo aliipongeza kamati hiyo kwa kufanya kazi hiyo kwa ufanisi licha ya kushtukizwa, huku wakiifanya kwa kujitolea.

“Jambo hili lilikuwa na presha kubwa na mimi nilipata presha, sikuwa najua kwamba lingekuwa na presha kubwa kiasi hiki… kazi hii haikuwa ndogo kwa sababu imehusisha jambo ambalo halijawahi kutokea katika historia ya nchi yetu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles