27.2 C
Dar es Salaam
Friday, September 30, 2022

NAPE: NIMEJITOLEA MAISHA YANGU, KAMA WAKUBWA WATACHUKIA WACHUKIE

Na MWANDISHI WETU,LINDI


MBUNGE wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, amesema amejitoa maisha yake kuwatetea wakulima wa korosho na kwamba yuko tayari jata kama wakubwa wakichukia.

Kauli hiyo ya Nape imekuja ikiwa zimepita wiki mbili tangu kumalizika kwa Bunge la bajeti ambalo mjadala wa korosho ulichukua nafasi kubwa hadi Spika Job Ndugai akasema lilikuwa ni ‘Bunge la korosho’.

Bunge hilo pia lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Sekta ya Korosho, Sura 203 ambayo yamefuta kifungu cha 17A ili ushuru wote wa ‘export levy’ unaokusanywa kwenye korosho ghafi zinazosafirishwa nje ya nchi uingizwe katika Mfuko wa Serikali.

Akizungumza na wananchi wa jimboni kwake mwishoni mwa wiki, Nape alisema yeye na baadhi ya wabunge wenzake walipinga sheria hiyo, lakini wakashindwa kwa kura, hivyo kwa sasa anamwachia Mungu kwa kuwa anajua wanakoelekea.

Kabla ya marekebisho ya sheria hiyo, fedha hizo za kodi ya ‘export levy’, asilimia 65 zilikuwa zikienda katika Mfuko wa Korosho ili kuendeleza zao hilo, huku asilimia 35 ikienda kwa Serikali. Lakini kwa sheria hiyo mpya, sasa asilimia zote 100 zinaenda serikalini.

 ATOA YA MOYONI

Akihutubia wananchi wakati wa mkutano wa hadhara, Nape alisema ameamua kujitoa kwa sababu anaujua ukweli vizuri kuhusu zao hilo la korosho tangu akiwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi aliposhiriki kila hatua tangu ulipoundwa Mfuko wa Korosho.

Pamoja na hilo, aliwataka wananchi hao kuwa wavulimivu kwa kipindi hiki cha mwaka mmoja endapo hatua hiyo ya Serikali itafanikiwa au haitafanikiwa.

“Mimi nimetoa maisha yangu, potelea mbali. Lakini kusema ukweli nitasema daima na chama changu kinasema ‘nitasema kweli daima fitna kwangu mwiko’, nyekundu iwe nyekundu, kama wakubwa wachukie, nyekundu iwe nyekundu na nyeusi iwe nyeusi, si mmenituma wenyewe? Mtanilinda?” alihoji Nape huku akijibiwa kuwa watamlinda.

Alisema Serikali yoyote duniani kazi yake ni kukusanya kodi na kusimamia ugawanyaji wa fedha zilizotokana na kodi, kisha zirudi kwa wananchi kwa ajili ya maendeleo yao.

“Sasa chama cha kwanza kimesema, cha pili kimesema, cha tatu ni hiki cha Serikali, na tusikilizane vizuri hapa, katika kupambana na umasikini wetu nilijua moja ya tatizo kubwa ni bei ya mazao yetu.

“Asilimia kubwa ya wananchi wa Mtama ni wakulima, wanalima ufuta, mbaazi, korosho na mazao mengine madogo madogo.

“Mnakumbuka nilipoanza nilizungumza juu ya mbaazi maana kuna wananchi wangu wameacha mbaazi zinaozea shambani kwa sababu bei imetoka Sh 2,000 mpaka Sh 150.

“Kazi ya Serikali ni pamoja na kutafuta masoko na Serikali hawatakwepa hilo na mimi kwenye suala la kutetea wananchi kwa kweli sitajali hatua yoyote Serikali itachukua kwa sababu ndiyo kazi niliyoomba, ninaomba kuwateteeni.

“Bila korosho maisha yetu taabani, wenzetu wana pamba sisi hatuna, wenzetu wana dhahabu sisi hatuna, wenzetu wana ng’ombe sisi hatuna, wenzetu wana utalii sisi hatuna, kuna kitu kimoja kinaitwa korosho.

“Korosho kwa muda mrefu inakwenda chini, mwaka 2006, rais wa wakati huo, Jakaya Kikwete, alikuja kufanya ziara akasema ‘sasa ninataka nikomboe zao la korosho’, moja ya tatizo lililokuwepo ni madeni kwenye vyama vya ushirika, Serikali ikaamua kuchukua madeni ili vyama vya ushirika viwe na uwezo kwenda kusimamia zao la korosho, vikopesheke, madeni yakachukuliwa na Serikali.

“Vyama vya ushirika vikaanza kukopesheka, tukaanzisha mfumo wa stakabadhi ghalani, mwaka 2010 mimi nikateuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Masasi, nikasimamia mfumo wa stakabali ghalani na ukaanza kupandisha bei ya korosho, tulianza na Sh 250, mwaka jana tumefika Sh 4,000 kwa kilo.

“Sasa katikati pale tukasema kwa kuwa bei imeanza kupanda, tutafute mfumo utakaosaidia zao la korosho, wadau wakakutana Masasi, tukakubaliana tukasema kwa kuwa hatuna viwanda vya kubangua, tupeleke korosho inayopelekwa nje itozwe kodi, ndiyo ikaitwa kizungu ‘export levy’.

“Tukasema sisi hatuwezi kukusanya, tuachie Serikali ikusanye kwa niaba yetu, tuwalipe asilimia fulani ambayo ni 35 tutamlipa Serikali na asilimia 65 iende kwenye mfuko wa pemebejeo, tukaanzisha Mfuko wa Pembejeo Masasi, tukausajili tukapeleka, hela ikaanza kuja.

Kwa habari kamili jipate nakala yako ya gazeti la MTANZANIA hapo juu

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,327FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles