24.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, October 8, 2024

Contact us: [email protected]

Nape: Nayajua maumivu Bunge kutorushwa live

TUNU NASOR-DAR ES SALAAM

ALIYEKUWA Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa, Michezo na Wasanii, Nape Nnauye, amesema anatambua maumivu wanayoyapata wananchi kutokana na Bunge kutokuoneshwa mubashara (live).  

Nape ambaye ni Mbunge wa Mtama (CCM), alisema hayo alipokuwa akizungumza katika kipindi cha 360 kilichorushwa na Clouds Tv jana.

Alisema anajua kuwa wananchi wanaona jambo hilo halikuwatendea haki, lakini ni kutokana na kuwa mchakato haukukamilika ipasavyo.

Nape alisema utungaji wa kanuni za kusimamia na kuendesha studio za Bunge haukushirikisha wadau ndiyo sababu ya Bunge kutokurushwa mubashara.

“Hata ushiriki wa wananchi katika shughuli za Bunge umepungua sana kwa kuwa wanaona vipindi vichache tu, hivyo tungetengeneza kanuni ambazo zitasaidia watu wote kuona zingesaidia kurejesha hali kawaida,” alisema Nape.

Alisema hata hivyo sheria za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), haziruhusu kuweka matangazo ya biashara wakati wa kuonesha vipindi vya Bunge jambo ambalo linaviumiza vituo vya televisheni na kushindwa kumudu kurusha mubashara.

“Kama Bunge ni la umma, linaendeshwa na fedha zetu za walipakodi, turuhusu kuweka matangazo katikati, lakini turuhusiwe kurusha ‘live’, jambo hili ni la kukaa mezani na kujadili tu,” alisema Nape. 

Alisema wakati anachaguliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, Michezo na Wasanii alikuta uongozi wa Bunge walikubaliana kuanzishwa kwa studio hiyo na tayari walikuwa wametenga fedha kuianzisha.

“Nilikuta TV pekee inayorusha Bunge ilikuwa ni TBC ambayo ilikuwa haitengewi fedha kwa shughuli hiyo, huku ikitumia Sh bilioni nne kwa mwaka kufanya kazi hiyo,” alisema Nape.

Alisema aliamua kuiondoa TBC kurusha matangazo hayo na kama Bunge lingehitaji kufanya kazi hiyo wangetakiwa kuilipa gharama inazotumia.

“Serikali ya awamu ya tano ilikuja na mkakati wa kupunguza matumizi na kila waziri alitakiwa kuangalia eneo lake, nami nikaona hapa tunaweza kupunguza matumizi,” alisema Nape.

Aliongeza kuwa hata hivyo Bunge tayari lilikuwa limeanza ujenzi wa studio zake kama ilivyo kwa nchi za Jumuiya ya Madola ambao hutumia utaratibu huo kulinda heshima za Bunge.

“Bunge liliamua kuviondoa vituo vingine vya televisheni ili waweze kuchukua taarifa kutoka studio za Bunge, lakini mzigo wote nilibebeshwa mimi kama waziri.

“Kama ‘screen’ zote bungeni zinaonesha kila kinachoendelea, kinachokosekana ni namna ya kwenda kuzichukua taarifa hizo na kuzirusha japo kwa kuchelewa dakika kadhaa ili mradi ziwafikie wananchi,” alisema Nape.

UNUNUZI KOROSHO

Akizungumzia suala la ununuzi wa zao la korosho, Nape aliwataka viongozi kujihadhari kutoa kauli ambazo hazijafanyiwa utafiti wa kutosha ili kauli ya serikali iwe thabiti.

Alisema Rais Dk. John Magufuli na Serikali ilikuwa na nia njema ya kuwasaidia wakulima, lakini changamoto ni kuwa vyombo ambavyo vinatekeleza suala hilo havikujiandaa.

“Sina uhakika kama Serikali ilikuwa imefanya maandalizi ya fedha za kununua korosho na kama ujuavyo fedha ya Serikali ili iweze kutoka ina mlolongo mrefu sana,” alisema Nape.

Alisema hata mfumo uliosimikwa kununua zao hilo baada ya kuiondosha Bodi ya Korosho na kuleta Bodi ya Mazao Mchanganyiko hauna uzoefu na suala la korosho.

“Suala la uhakiki tumekuwa hatufanyi vizuri, kwa mfano uhakiki wa wafanyakazi, wastaafu na madeni ya nyuma umekuwa na ukakasi,” alisema Nape.

KUTOLEWA BASTOLA

Akizungumzia hatua aliyoichukua baada ya kutolewa bastola na mtu katika mkutano wake na waandishi wa habari, Nape alisema anamfahamu mtu huyo na waliopanga kufanya tukio hilo, lakini aliamua kuwasamehe.

“Sikutaka kuripoti polisi kwa kuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa alikuwapo na polisi wenye sare na wasiokuwa na sare, sasa namshtaki nani kwa nani?” alihoji Nape.

MATUMIZI YA TWEETER

Alisema amekuwa akitumia mtandao wa kijamii zaidi wa tweeter kuwasilisha ujumbe kwa jamii inayomzunguka.

“Lengo ni kufikisha ujumbe kwa jamii na ukirusha jiwe gizani ukisikia tu ameguna ujue ndio liliyempiga,” alisema Nape.

MSAADA KWA RUGE

Wakati huohuo Nape amewataka Watanzania ambao ni jamaa wa Mkurugenzi wa vipindi vya Clouds, Ruge Mutahaba kujitolea kwa hali na mali kusaidia matibabu yake huko Afrika Kusini.

“Najua kuwa kuna familia ya Ruge nje ya Mutahaba, wajitokeze kusaidia matibabu yake ambayo yanagharimu kiasi kikubwa cha fedha huko Afrika Kusini,” alisema Nape.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles