27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

NAPE AWAONYA MAOFISA HABARI NCHINI

Na SARAH MOSES, DODOMA


MAOFISA habari na viongozi wa umma nchini, wametakiwa kutekeleza sheria zinazowataka kutoa habari na taarifa kwa vyombo vya habari ili wananchi wajue kinachoendelea nchini.

Rai hiyo ilitolewa juzi mjini Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alipokuwa akifungua kikao kazi cha maofisa mawasiliano serikalini.

Alisema maofisa habari watakaobainika kutotimiza wajibu wao, watachukuliwa hatua kwa sababu moja ya majukumu yao ni kutoa habari kwa vyombo vya habari.

“Hata ikibainika viongozi wao wa juu ndio vikwazo, wizara yangu itasimamia kidete kuhakikisha mamlaka ya nidhamu ya kila mhusika inamchukulia hatua stahiki.

“Nasema hivyo kwa sababu kuunyima umma habari ambazo ziko wazi, si tu ni kuvunja sheria, bali pia ni kukinzana na maono ya rais wetu.

“Katika hili, Idara ya Habari (Maelezo) itaweka mfumo wa kuwapima maofisa habari kila mara kwa vigezo ambavyo ninataka tukubaliane wenyewe kupitia mkutano huu.

“Hivi tunawezaje kuwa na kitengo cha habari kisichotoa taarifa yoyote kwa miezi kadhaa?

“Je, tunaweza kuwa na kitengo cha habari katika zama hizi kwenye ofisi ya umma ambacho hakiandai hata makala kwenye magazeti, redio na kwenye runinga.

“Baada ya mkutano huu, niletewe malengo yanayopimika na tuanze mara moja kupimana kiutendaji,” alisema Nape.

Pamoja na hayo, Nape aliwapongeza wakurugenzi, Dk. Hassan Abasi wa Maelezo na Greyson Msigwa wa Ikulu kwa kuweza kuwa wabunifu na mfano hai wa namna Serikali inavyoweza kutumia teknolojia mbalimbali za mawasiliano.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles