25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Nape atoa ushauri Simba, Yanga

nape-nnauyeNa ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, amezishauri klabu za Simba na Yanga, kushirikiana na Serikali katika kufanya tathmini za mali zao kabla ya kuingia kwenye mapinduzi ya  mifumo ya uendeshaji wa klabu hizo kwa kutumia mfumo wa hisa na kampuni.

Nnauye aliyasema hayo huku klabu ya Simba ikiwa katika mchakato wa kumilikiwa na mfanyabiashara, Mohammed Dewji ‘Mo’, kwa asilimia  51 kwa Sh bilioni 20, wakati  Mwenyekiti wa Yanga akitaka kukodisha nembo ya  klabu ya Yanga  kwa miaka 10, akitaka majengo yabaki kuwa mali ya klabu, asilimia 25 ya faida itaingia kwa klabu lakini gharama za uendeshwaji zitakuwa chini yake.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Nnauye alisema Serikali inaunga mkono uwepo wa mifumo hiyo na itakuwa tayari kushirikiana na klabu hizo kufanya tathmini ya mali zao, huku ikizitaka kuwa makini  kabla ya kufanya uamuzi wa matumizi ya mifumo hiyo.

“Wanatakiwa kuwa makini kabla ya kuingia katika mifumo hiyo, kwani tayari tumeshuhudia wakinyoosheana vidole hivyo tunashauri michakato iwe ya wazi kwa  kila hatua kwa kuwa klabu hizo ni mali za wananchi.

“Wakati wakiwa katika michakato hiyo ni vizuri kuzingatia historia ya klabu hizo, pia ni lazima mikataba hiyo iridhiwe kwa dhati si kwa ushawishi wa fedha,” alisema Nnauye.

Nnauye alizitaka klabu hizo kufuata sheria za nchi na zinazosimamia michakato hiyo, huku akisisitiza kuwa Serikali haitasita kuingilia kati iwapo kutakuwa na uvunjwaji wa sheria hizo.

“Kama michakato ikiendeshwa vizuri kwa kuzingatia sheria na mambo mengine niliyoyaeleza, jambo hili litakuwa lenye tija hata hivyo hatutasita kuingilia kati kama hakutakuwa na utaratibu wenye kufuata sheria,” alisema Nnauye.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles