23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NAPE ATABAKI SALAMA NDANI YA CCM?

Na BALINAGWE MWAMBUNGU


NIMESOMA mahali kwamba mwezi Machi una matukio mawili makubwa katika nchi yetu; kwanza ni kifo cha aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Horace Kolimba ambacho kilitokea Machi 13, 1997 na kufutwa kazi Nape Nnauye Machi 23, mwaka huu.

Horace Kolimba

Alishika nyadhifa mbalimbali serikalini ikiwa ni pamoja na kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera. Alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa JUWATA Taifa na kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera. Baada ya hapo aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), 1990-1995.

Ni katika kipindi hicho Kolimba akateuliwa kuwa Mbunge na Waziri wa Mipango ili kumwezesha kujua mambo yaliyokuwa yanaendelea bungeni na kwenye Baraza la Mawaziri.

Alipotamka mbele ya hadhara kupitia wanahabari, kwamba CCM imepoteza dira, chama ambacho alikuwa anakiongoza wenzake wakashituka. Akaitwa Dodoma kujieleza mbele ya Kamati Kuu. Hakurudi. Wataalamu wakasema alikufa kwa presha.

Ikumbukwe kwamba Kolimba hawakuwa wanapatana na Mwalimu Julius Nyerere ambaye tayari alikwisha ng’atuka urais na uenyekiti wa CCM kutokana na viongozi watatu wa juu; Rais Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu, John Samwel Malecela na Katibu Mkuu, Horace Kolimba, kukubali hoja ya Bunge ya kuirejeshea madaraka Serikali ya Tanganyika.

Lakini pia Kolimba, ilisemekana alikuwa na nia ya kugombea urais mwaka 1995, lakini akatambua kwamba angepingwa na Mwalimu Nyerere. Kwa hiyo, aliyatamka maneno ya kushitua kwamba CCM imepoteza dira. Aliwatega wenzake ili wafanye kosa la kumfukuza kwenye chama. Kumbuka wakati huo tayari tulikuwa tumekwishaingia kwenye mfumo wa vyama vingi na hatujui angejiunga na chama kipi. Bahati mbaya alifariki wakati Kamati Kuu haijafanya uamuzi kuhusiana na kauli yake.

Horace alikuwa kaka na rafiki yangu. Tulikuwa majirani kijijini Kwemba yeye alikuwa tayari amejenga na kuhamia, mimi nilikuwa na kipande cha shamba.

Baada ya CCM kumwandikia barua ya kumwita Dodoma, alinipigia simu na akataka tukutane pale Hoteli ya Palm Beach, Dar es Salaam. Tulizungumza mengi na swali langu la mwisho kwake lilikuwa: Ukifukuzwa CCM utakwenda chama gani? Alijibu kwa Kiingereza: “We will cross the river when we get there”maana yake; Tutajua namna ya kuvuka tukishafika mtoni.

Kwa mtazamo wa wengi, Kolimba alikuwa na ujasiri wa kusema kile alichokiamini na akaamua kusema ukweli, bila woga. Kumbuka kwamba kabla ya vyama vingi, CCM kilikuwa na dira, Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, siasa ambayo ilifutwa na Azimio la Zanzibar. Je, CCM ya sasa ina dira?

Nape Nnauye

Aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ameondolewa madarakani kimya kimya Machi 23 mwaka huu. Hakuna anayehoji uamuzi wa Rais kwa kuwa amepewa mamlaka hayo na Katiba. 

Watu wanazungumzia mtifuano, hakuna kitu kama hicho. Nani asiyejua kwamba cheo ni dhamana?  Cheo ni kupokezana kijiti, hakuna mtu atakayedumu na cheo kama sultani. Nape analijua hilo.

Tofauti ya Tanzania na nchi nyingine za Kiafrika, kiongozi wa juu amewekewa mihula miwili tu ya miaka mitano mitano. Lakini kuna baadhi ya nchi ya viongozi, wakishaingia madarakani, wanasahau kwamba wamechaguliwa na wananchi kwa mkataba. Wakiona namna gani vipi, wanabadilisha vifungu vya Katiba ili wandelee kutawala.

Nape Nnauye, kwa mtazamo wangu, ni kama Kolimba. Aliamua kusimama kwenye ukweli. Katika historia ya nchi hii, ni mwaka 1964 tu, ambapo wanajeshi wenye silaha walikamata kituo cha redio TBC na kutangaza amri ya hatari, lilikuwa jaribio la kuipindua Serikali. Tangu hapo, hapajawahi kutokea tukio kama wakati wa Rais Mwinyi, Rais Benjamin Mkapa.

Tukio la Ijumaa ya Machi 17, 2017 lililofanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, akiwa na askari wenye silaha za moto, kuvamia Studio za Clouds, limelitia doa Taifa letu. Na sisi wanahabari ni lazima tuliweke katika kumbukumbu.

Nape Nnauye, kama Waziri wa Habari, mwenye dhamana ya kuvisimamia vyombo vya habari, alikwenda pale Clouds Media Group kuwapa pole viongozi na wafanyakazi, kutokana na tukio hilo. Akasema kwamba Serikali inalaani vikali kitendo hicho. Akaahidi kufanya uchunguzi na tayari alikuwa ameunda kamati ya kufanya hivyo.

Sitaki kurudia yaliyotamkwa na Rais John Magufuli, muda mchache baadaye alipokuwa kwenye sherehe ya kuweka jiwe la kumbukumbu ya ujenzi wa barabara za juu pale makutano ya barabara za Sam Nuyoma/Nelson Mandela na Morogoro. Waliosikia wamesikia.

Nape alikuwa amekanwa. Wenye akili wakajua kwamba kibarua cha Waziri Nape kilikuwa shakani. Kwa hiyo, tangazo la asubuhi ya Machi 23, 2017 halikuwa la kushitua kwamba Nape Nnauye si Waziri wa Habari tena.

Wako wanaomlaumu kwamba alifanya kosa kuitisha mkutano na waandishi wa habari siku hiyo hiyo. Hakuna aliyejua atasema nini lakini inaelekea vyombo vya dola vilikuwa vinajua aliyotaka kuyasema, huenda yalikuwa ni mambo mazito ambayo yangebadili upepo wa siasa nchini.

Kwa hiyo wakachukua hatua za kumdhibiti. Njia mojawapo walimwamuru mwenye Hoteli ya Protea, pale Oyster Bay, amfungie mlango Nape, asifanye mkutano na wanahabari hotelini mwake.

Kama hiyo ilikuwa haitoshi, wakatumwa askari na makachero, kuhakikisha kwamba Nape haingii hotelini hapo kwa vyovyote vile na labda ndilo lililomfanya askari yule kumnyooshea bastola Nape alipokaidi na kutaka kuingia hotelini.

Nape si mhalifu, Nape ni kiongozi katika chama tawala, kwanini polisi waende na silaha? Tulitazame suala hili kwa upande mwingine. Nape amevuliwa cheo cha uwaziri. Nape bado ni kiongozi wa umma ni Mbunge wa CCM Jimbo la Mtama, hiyo ilitosha kumpa heshima.

Lakini Nape pia ni raia wa Tanzania ana haki ya kukutana na watu au kikundi chochote, ana haki ya kikatiba ya kutoa maoni ilimradi tu havunji sheria.

Nape hakuitisha mkutano wa hadhara, kwa hiyo hakuhitaji kuwaomba polisi wampe ulinzi, alikuwa ameomba kwa mwenye hoteli kutumia ukumbi wa ndani akutane na wanahabari. Nani alilipia ukumbi, si suala la mjadala hapa. Ila tuwaulize jeshi la polisi, Je, watalipa gharama za ukumbi?

Kilichoendelea pale nje ya Kanisa la St. Peters Oyster Bay, baada ya Nape kukataliwa kuingia hotelini, sote tuliona kwenye luninga.

Tunachohoji hapa, Je, ni kosa mtu akifukuzwa kazi kusema ya moyoni? Kumbukeni Nape ni ‘Public figure’ na alitaka kusafisha hali ya hewa kwa sababu kulikuwa na taharuki; kwanza katika vyombo vya habari na kule jimboni kwake Mtama pamoja na Mkoa wa Lindi kwa jumla.

Nape kama mwanasiasa mpevu, asingeweza kukaa kimya, kwa kuwa alijua kwamba watu watakuwa na shauku ya kutaka kujua nini kimemsibu kijana wao. Katika hali hii, asingeweza kusubiri eti atafakari!

Kwa vitimbi na vituko alivyofanyiwa Nape mpambanaji na kada wa CCM, vimemfanya aonekane shujaa wa kutetea ukweli kama alivyokuwa Horace Kolimba aliyetamka mambo ambayo wakubwa zake hawakutaka kuyasikia kwamba chama chao kilikuwa kimepoteza mwelekeo.

Ni viongozi wachache ndani ya CCM ambao wanaweza kusimamia kile wanachoamini. Swali ni Je, Nape atabaki salama kwenye chama hicho? Ametofautiana na Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM. Naweka maneno ya akiba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles