27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Nape alivyohaha kusaka msamaha wa JPM

ELIZABETH HOMBO – DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli ameelezea namnaMbunge wa Mtama, Nape Nnauye, alivyohangaika kumwomba msamaha, huku akimtumia ujumbe mfupi wa maneno saa nane za usiku.

Mbali na hilo, Rais Magufuli pia ameeleza kuwa mwanasiasa huyo kijana alikwenda hadi kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, Mkurugenzi Mkuu mstaafu wa Idara ya Usalama wa Taifa, Apson Mwang’onda na mke wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere ili wamwombee msamaha.

Hatua ya msamaha huo inakuja ikiwa ni siku chache tangu Rais Magufuli alipotangaza kuwasamehe wabunge wawili wa CCM; January Makamba (Bumbuli) na Wiliam Ngeleja (Sengerema) baada ya kumwomba msamaha.

Makosa ya wabunge hao na ya Nape yanafanana wote wakielezwa kumsema vibaya kiongozi huyo wa nchi kupitia mazungumzo ya simu.

Wanachama wengine ambao nao wanatajwa sauti zao kusikika wakimsema vibaya Rais Magufuli, ni makatibu wakuu wastaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana, Yusuf Makamba na Waziri wa Mambo wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.

Akizungumza jana Ikulu, Dar es Salaam muda mfupi baada ya Nape kumtembelea, Rais Magufuli alieleza bayana kwamba amemsamehe mbunge huyo wa Mtama.

“Na mimi nimeshamsamehe, nimemsamehe kwa dhati, Nape amekuwa hata akiandika ‘message’ nyingi tu, ameshaandika message wakati mwingine hadi saa nane usiku akiomba msamaha.

“Sasa unamwona kabisa huyu mtu anaomba msamaha na leo (jana) kaniomba aje anione na wakati mwingine wasaidizi wangu wamekuwa wakipata hiyo habari.

“Amejaribu kwenda kwa mzee Mangula, amefika hadi kwa mzee Apson na amefika pia hata kwa mama Maria Nyerere, amehangaika kweli, lakini baadaye ni katika hiyo hiyo kwamba sisi tumeumbwa kusamehe na leo umemwona asubuhi amekuja hapa.

“Baadaye nikaona siwezi nikamzuia kumwona, ngoja niache shughuli zangu kwanza nimwone, maana nilikuwa na kikao kingine, amekuja hapa kikubwa anachozungumza anasema ‘naomba baba nisamehe’.

“Kusamehe kunaumiza, lakini nasema kwa dhati kabisa nimemsamehe na ameeleza yaliyokuwa yanamsibu, lakini pia ameeleza baadhi ya watu waliokuwa wanamhubiri, wengine wako kwenye chama, lakini nimesema yote tunasamehe na bado yeye ni kijana mdogo ana ‘future’ nzuri katika maisha yake.

“Mimi nikiendelea kumshikilia kwenye moyo wangu kwanza ni dhambi kubwa kwa Mwenyezi Mungu na tumefundishwa katika maandiko yote tusamehe saba mara sabini, kwa hiyo nimemsamehe na Mungu amsaidie katika shughuli zake, akafanye kazi zake vizuri, akalee mke wake na familia yake, akakitumikie chama na akawatumikie wananchi wa jimbo lake,” alisema Rais Magufuli.

Wakati wakiagana kwa kushikana mikono, Rais Magufuli alimhoji Nape kama alikuwa ana amani huku akicheka. Nape alimjibu kuwa wakati mwingine alikuwa anakosa usingizi na kuamka saa nane usiku, lakini sasa anajisikia raha.  

NAPE

Awali, Nape ambaye alipata kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, alisema anamshukuru sana Rais Magufuli kwa kukubali kuonana naye, kumsikiliza, kumsamehe, kumshauri na kumwelekeza.

“Nimekuja kumwona kama baba yangu, lakini mwenyikiti wa chama changu, Rais wangu, kwa sababu wote mnajua mambo yaliyopita yametokea mengi hapa katikati na mimi kama mtoto wa CCM, kama mwanaye, nimeona ni vizuri nije niongee na baba yangu.

“Nashukuru amenipa fursa ya kuja kumwona, ameniambia amenisamehe na pia amenipa ushauri, kwa kweli kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru sana, amenipa fursa kubwa.

“Hivyo mheshimiwa Rais kama mzee wangu, baba yangu nashukuru sana kwa fursa uliyonipa, lakini kwa kunisikiliza na kunisamehe, lakini pia kwa kunishauri na kunielekeza ninafanyeje huko mbele ninapokwenda,” alisema Nape.

AMBAO HAWAJAOMBA MSAMAHA

Mwishoni mwa wiki hii akizungumza na MTANZANIA, Membe alihoji sababu za yeye kumwomba radhi Rais Magufuli na iwapo gazeti hili limejiridhisha kama wapo waliofanya hivyo.

Kwa upande wa Makamba, yeye alisema hana maoni juu ya hilo.

Kutokana na hilo, wanasiasa hao ambao bado hawajamwomba msamaha Rais Magufuli ni Makamba, Kinana, Membe na Katibu Kata wa Kijiji cha Rondo mkoani Lindi.

JANUARY NA NGELEJA

Wiki iliyopita akizungumza namna January na Ngeleja walivyomwomba msamaha, Rais Magufuli huku akitamka bayana kwamba iwapo wasingeomba msamaha wangepelekwa Kamati ya Siasa ya Kamati Kuu ya CCM na wangepewa adhabu kubwa.

Wakati Rais Magufuli akitoa kauli ya kuwasamehe January na Ngeleja, alisema walimtukana wengi, lakini hao wawili ndio walijitokeza na kumwomba msamaha na kwa kutambua kuwa hao ni vijana, walimgusa na kuamua kuwasamehe.

“Kusamehe huwa si kitu rahisi, lakini tuna wajibu wa kusamehe na saa nyingine kusamehe huwa kunauma, lakini saa nyingine inabidi usamehe.

“Kuna watu fulani walinitukana wee na ‘nika-prove’ (nikathibitisha) kwamba sauti zile ni zao ‘more than one hundred percent’ (zaidi ya asilimia 100), nikawa nakaa nafikiria, nikasema hawa wakipelekwa kwenye Kamati ya Siasa ya Central Committee adhabu itakuwa kubwa.

“Lakini wakajitokeza wawili wakaniomba msamaha, nikawa najiuliza mimi kila siku naomba msamaha kwa Mungu na ile sala ya kuomba utusamehe makosa yetu kama tunavyowasamehe wengine, nikaona hawa waliokuja kuniomba msamaha kutoka kwenye dhamira yao, nisipowasamehe nitabaki na maumivu makubwa kwenye moyo wangu,” alisema.

KUSAMBAA SAUTI

Itakumbukwa kuwa Julai, mwaka huu, sauti zinazodaiwa kuwa ni za January, Nape, Makamba na Kinana zilisambaa katika mitandao mbalimbali ya kijamii.

Pamoja na mambo mengine, walisikika wakizungumzia kuandaa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwa Makamba na Kinana.

Siku chache baadaye, ikasambaa sauti nyingine ya mawasiliano inayodaiwa kuwa ya Nape na Ngeleja, kisha kufuatiwa sauti inayodaiwa kuwa ni ya Membe na Katibu Kata wa Kijiji cha Rondo mkoani Lindi.

Kusambaa kwa sauti hizo kulitanguliwa na tukio la Julai 14, mwaka huu ambalo Makamba na Kinana waliandika taarifa kwa Baraza la Wazee wa CCM wakilalamikia mambo mbalimbali ikiwamo kudhalilishwa kwa mambo ya uongo na mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Waraka huo unaodaiwa kuandaliwa kwa ushirikiano wa Nape na January, pia ulisambazwa katika mitandao ya kijamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles