29.2 C
Dar es Salaam
Thursday, September 19, 2024

Contact us: [email protected]

Nape ahimiza watoa huduma za mawasiliano kuwekeza kwenye miundombinu

Na Esther Mnyika Mtanzania Digital

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia, Nape Nnauye ametoa rai kwa watoa huduma za mawasiliano kuendelea kuwekeza kwenye miundombinu inayowezesha kufikisha huduma kwa watumiaji wa mwisho ambao ni wananchi kwani uwekezaji bado ni kubwa na linahitaji uwekezaji wa pamoja kufikia malengo ya Taifa.

Nape amebainisha hayo leo Septemba 25, jijini Dar es Salaam wakati wa hafla ya utiaji saini wa hati ya maridhiano na hati ya mkataba wa nyongeza kwenye miundombinu ya mkongo wa mawasiliano na Teknolojia ya Habari na Umoja wa watoa Huduma za Mawasiliano (Consortium of Telco Operators) ambao unajumuisha Kampuni ya Airtel Tanzania, Honora Tanzania (Tigo) na Kampuni ya Vodacom Tanzania.

Amesema anamshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa namna mbavyo amekuwa akiipa sekta ya TEHAMA kipaumbele katika kuhakikisha kuwa inakuwa wezeshi na inachochea ukuaji wa uchumi kwa nchi.

“Leo hii tumeshuhudia utiaji saini wa Hati ya Maridhiano na Hati ya Mkataba wa nyongeza kati ya Wizara ninayoiongoza na Consortium of Telco Operators ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo yake aliyotoa kuhusu kuhakikisha Wizara na Consortium inafanyia kazi changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa makubaliano yaliyoingiwa,” amesema Nnauye.

Amesema anawapongeza wote kwa namna mbavyo wameweza kushirikiana na Serikali na kuhakikisha kuwa changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mkataba zimetatuliwa kwa kuzingatia maslahi ya pande zote mbili.

Waziri huyo amefafanya kuwa Oktoba, 4, 2011 Serikali kupitia iliyokuwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia iliingia makubaliano ya miaka 30 na Umoja wa Watoa Huduma za Mawasiliano uliokuwa unajumuisha kampuni ya Celtel Tanzania LTD (Airtel), MIC Tanzania LTD (Tigo) na Zanzibar Telecom LTD (Zantel).

Mkataba huo ulihusu ujenzi wa mkongo wa mawasiliano (Optic Fibre Cable Network) wenye njia 48 katika maeneo yaliyokuwa hayajafikiwa na Mkongo wa Taifa (missing links).

Ameeleza kuwa dhamira ya serikali ya kuingia mkataba na umoja huo ilikuwa ni kuongeza kasi ya kuyafikia maeneo yasiyokuwa na huduma za mawasiliano nchini kupitia jitihada za pamoja na Sekta Binafsi za ujenzi wa mkongo.

Amesema utekelezaji wa mkataba ulikumbwa na changamoto mbalimbali ambazo zilipelekea pande zote mbili kukutana, kujadiliana na hatimaye kufikia muafaka.

Amesema utiaji saini wa hati ya maridhiano ambapo Consortium imeridhia kutoa fedha taslimu Dola za Marekani milioni 20 sawa na Sh bilioni 50 kwa kipindi cha miaka mitano ikiwa ni malipo ya matumizi ya njia za miundombinu hiyo tangu ilipojengwa hadi sasa pamoja na kufanya uwekezaji wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 13 sawa na Sh bilioni 32.5.

Aidha, wameshuhudia utiaji saini wa hati ya mkataba wa nyongeza ambapo Kampuni ya Vodacom Tanzania imekuwa sehemu ya Conosrtium, hatua inayoonyesha ushirikiano uliopo kati ya sekta binafsi katika kufikisha huduma za mawasiliano kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.

“Matokeo chanya ya majadiliano haya yatawezesha Consortium kukabidhi kwa serikali miundombinu ya Mkongo wa Mawasiliano wenye urefu wa takribani kilomita 3,000,”amesema Nape.

Ameongeza kuwa hivi karibuni walishuhudia utiaji saini mradi wa kujenga minara mipya 758 ili kuongeza na kupanua wigo wa mawasiliano ambayo itawafaidisha zaidi ya Watanzania milioni nane kote nchini.

Amesema Serikali imepunguza gharama za kuweka miundombinu ya mkongo kutoka Dola za Marekani 1,000 hadi 100 ili kuharikisha ufikishaji wa mawasiliano bora kwa wananchi na imeongeza uwezo wa Mkongo wa Taifa kutoka kwenye uwezo wa 200Gbps hadi kufikia 800Gbps na inaendelea na upanuzi huo kufikia kiwango cha 2000Gbps sawa na 2Tbps.

Nnauye amesema wanaendelea na ujenzi wa Mkongo wa Taifa ambao unatarajia kufikia Wilaya 99 kati ya 139 ifikapo mwezi Machi, mwakani lengo likiwa ni kufikia wilaya zote 139 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2024.

Amesema kuimarisha sekta ya TEHEMA na Mawasiliano itasaidia kuleta maendeleo ya uchumi, kukuza biashara na kuongeza matumizi ya kidigitali katika kuimarisha sekta za kijamii.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles