28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NAPAMBANA KUWAINUA WANAWAKE NMB – GLADNESS

Na ASHA BANI


LEO Tanzania imeungana na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Katika makala haya, nimekutana na mwanamke ambaye kwa namna moja ama nyingine naweza kusema kuwa amepata mafanikio aliyoyatumia katika kuwanyanyua wanawake wenzake.

Si mwengine bali ni Gladness Deogratias (33), Mkuu wa Idara ya Fedha za Kigeni katika Benki ya NMB.

Gladness ameweza kuelezea mafanikio yake na changamoto alizozipata hadi kufikia hapo alipo huku akitaka wanawake wengine nchini kuiga mfano wake na kutokata tamaa katika maisha ili kuonja mafanikio.

Anasema kwa kuhakikisha hilo na kutaka kuona wanawake wanafanikiwa, mwaka jana alianzisha Forum ya wanawake katika benki hiyo yeye akiwa ni mwenyekiti.

Anasema lengo la Forum ndani ya NMB ni kuhakikisha wanawake wanashika nafasi za juu ya uongozi ndani ya benki kwa kufanya nao kazi na kuwafundisha mbinu mbalimbali za mafanikio.

Anasema yeye tayari ameshafika ngazi ya juu hivyo ni lazima ahakikishe anawasaidia wanawake wengine ili wafikie alipo.

“Ni lazima kuwasaidia wanawake kuweza kuingia katika ushindani na ni lazima kutengeneza sera ili kuweza kushindana na ikifanyika hivyo na kuonekana kuwa na mafanikio, benki nyingine zitaiga hivyo, kiwango cha wanawake katika kwenye benki kuwa na uamuzi kitakuwa kikubwa,” anasema Gladness.

Anasema kutokana na Forum hiyo, NMB imekuwa na mkakati kabambe wa kuwapo kwa usawa wa 50 kwa 50 hasa kwa kuanza na wanafunzi wanaofika kufanya mafunzo ‘field’anawasimamia na kuhakikisha wanawake wanafanya vizuri na hata wengine kuwapatia ajira za moja kwa moja.

Anasema atahakikisha kunakuwapo usawa wa kijinsia katika benki hiyo kwa maana ya kuwa na uwiano mzuri kwa wanaume na wanamke katika nguvu kazi yao.

 “NMB inaamini si tu usawa bali haki na ni jambo sahihi katika jamii, lakini pia ni suala la biashara katika mafanikio.’’

Anaeleza kuwa alipofika katika benki hiyo, mwaka 2014 aliona hilo mapema kwa kuangalia namba ya wanawake katika ngazi za juu hivyo ni lazima kupambana kuwainua.

Akizungumzia kuhusu changamoto zinazozuia wanawake kuendelea na njia zake za utatuzi, anasema kuna mipango kadhaa ambayo mashirika yanaweza kufanya ili kuwainua ikiwa ni pamoja  na kuwaondolea vikwazo kwa kuajiri walengwa, kuwa na sera za kazi na likizo ambazo ni rahisi na zinazoangalia jinsia.

Kuwa na mpango wa kusaidia wanawake kupata ujuzi na uzoefu na kuwapo kwa mpango maalumu wa mafunzo ya uongozi kwa wanawake ambao utalenga kuwawezesha pia.

Gladness pia alizungumzia jinsi ya kuwashirikisha wanawaume katika kusaidia kushiriki usawa wa jinsia sehemu za kazi katika jamii.

“Wanaume ni watu muhimu katika kuziba pengo la usawa wa jinsia, hapa kuna kitu kinaitwa ‘upendeleo bila kujijua’ ambacho kipo hivyo tukiwajumuisha wanaume pamoja itasaidia kuweka hali hiyo wazi,’’anasema Gladness.

Anasema inabidi kuongeza wajibu wao katika kuingiza masuala ya jinsia na kuleta mkakati wa utekelezaji.

Anasema katika kuhakikisha si tu wanawake wa benki ndio wanatakiwa kufanikiwa bali Forum ya wanawake NMB inatoa fursa ya kusaidia vikundi vingine vya wajasiariamali wanawake.

Anasema kwa kupitia vikundi vidogo vidogo vya wajasiriamali huwa wanawasapoti mikopo na kutolea mfano kikundi cha akina mama kilichopo Zanzibar cha Ushindi Women.

Anaeleza kuwa na mwendelezo wa programu hiyo nchi nzima lengo ni kumfanya mwanamke awe bora zaidi katika familia kwa kutafuta na kusaidia familia yake.   

Historia yake

Amezaliwa miaka 33 iliyopita na amesoma katika Shule ya Msingi Chang’ombe mwaka 1996.

Alifanikiwa kufaulu na kujiunga Shule ya Sekondari Kifungilo mwaka 1997 – 2000.

Baada ya hapo alifanikiwa kupata nafasi ya masomo kupitia International School of Tanganyika na kujifunza masomo ya saikolojia.

Mwaka 2005-2006 alijiunga na Chuo Kikuu cha Nottimghan Uingereza na kuchukua BA ya masuala ya biashara.

“Baada ya kumaliza chuo niliomba kufanya kazi katika benki kubwa ya LEHAM international Eropean Bank na niliomba kama graduate program ambayo nilikaa hapo kuanzia 2006 hadi 2008 ulipotokea mtikisiko wa kidunia nikarudi nyumbani Tanzania,” anasema Gladness.

Anasema akiwa hapa nchini aliwahi kufanya kazi katika benki ya ABC na baadaye kujiunga na  NMB hadi hapa alipo sasa na kuendeleza wanawake wenzake.

Ameolewa na ana watoto watatu – mmoja wa kike na wawili wa kiume.

Gladness pia anawakumbusha akina mama wote nchini hasa wale ambao wapo katika kutafuta kipato kwa njia ya ajira au biashara kutenga muda wao wa kazi sambamba na muda wa kuhudumia familia.

Anasema amekuwa akijitahidi kugawanya muda wa familia na kazi za watoto na kuwahudumia watoto wake kwa upendo.

Anasema huwa anatoka kazini na kuwahi nyumbani kwa ajili ya kuangalia familia na nyakati za asubuhi ni lazima aamke asubuhi na mapema kwa ajili ya kuwaandaa watoto wake kwenda shule.

Anasema siku ya Jumapili anatenga muda wa kwenda kumuabudu Mungu na familia yake ikiwa ni pamoja na kuingoza familia hiyo katika njia inayompendeza Mungu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles