TASNIA ya mitindo imebeba maisha ya watu ndani yake, kuna watu wanaipa heshima kubwa sekta hiyo kwa sababu imewapa maisha, imewapa umaarufu unaofanya waishi vyema hapa duniani. Haijalishi nafasi waliyonayo sasa hivi waliitafuta vipi ila hata siku moja huwezi kuona wanaichezea kazi hiyo.
Kuichezea tasnia ya mitindo siyo lazima uwadharau waasisi wake, hata kitendo cha kutafuta umaarufu kwa kigezo cha mitindo kwa kujifanya modo ambaye unakiuka misingi, tamaduni na taratibu za tasnia hiyo unakuwa unaidharau tasnia na kuwakosea mamodo wenye heshima zao.
Licha ya kuwa mchekeshaji ambaye muda mwingi huendekeza utani, Idris Sultan moja katika ya posti zake kwenye mitandao ya kijamii wiki hii aliandika ujumbe mujarabu sana ambao umenigusa na kuwagusa watu wote wanaohusika na tasnia ya mitindo nchini kufuatia kuibuka kwa watu wengi wanaotumia kivuli cha mitindo kupitisha uhuni wao.
Mshindi huyo wa shindano la Big Brother mwaka 2014, aliwashukia wanamitindo wachanga wakike ambao wamekuwa wakiitumia mitandao ya kijamii vibaya kwa kuweka picha za utupu wakitumia kigezo uamitindo.
Idris aliiendelea kutoa somo kwa mamodo chipukizi ambao wanapiga picha zinazoacha sehemu kubwa za miili yao kwa kuwauliza lengo lao ni nini haswa mpaka kuingia studio au kwenye fukwe na kupiga picha hizo chafu zinazopakaza matope tasnia ya mitindo,
Kufanya hivyo ni kutangaza brandi gani? Je ni kutangaza mataulo, vumbi au majani, kampuni gani kubwa itawekeza fedha zake kwa mtu ambaye tayari heshima yake kwenye jamii imeshuka? Hakuna.
Hapo ndipo niliposhawishika kuandika andiko hili ambalo ni kama nyundo ya kugongelea msumari wa Idris kwa mamodo chipukizi ambao kiukweli wanaivunjia heshima tasnia ya mitindo kwani kiuhalisia modo si kuacha mwili wazi.
Kwa maana hiyo endapo modo chipukizi atatumia njia hiyo kujipatia umaarufu anakuwa anaivunjia heshima tasnia hiyo hali kadharika anakuwa anawakosea wanamitindo wanaoishi kupitia kazi hiyo, wote wanaonekana wahuni ilhali si kweli.
Mbona wanamitindo kama Flaviana Matata, Herieth Paul, Niler, Lorraine Pascale, Millen Magese, Maggie Vampire, Dax, Lota, Calisah na wengine wengi hawafanyi hiyo michezo, iweje wewe utumie kivuli cha mitindo katika kukamilisha adhma yako mbaya.
Ni lazima suala hili la watu kuichafua tasnia ya mitindo kwa kuleta michongo ambayo si ya kimitindo tuikemee kwa nguvu zote, tunahitaji wanamitindo ambao tutawatambua kwa kazi zao nzuri na siyo kwa matukio ya kuweka picha za utupu kwenye mitandao ya kijamii.