24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

NANI KUIBUKA MSHINDI WA URAIS UFARANSA LEO?

Emmanuel Macron (kushoto) na Marine Le Pen (kulia)

 

 

PARIS, Ufaransa

WAPIGAKURA nchini Ufaransa wanatarajiwa kuamua leo nani atakuwa rais wao baada ya kumalizika utawala wa Rais Francois Hollande wa miaka mitano. Hollande anaondoka madarakani baada ya kukataa kutetea nafasi yake katika muhula wa pili.

Zoezi la uchaguzi wa mwaka huu limekuwa la kusisimua ambapo jumla ya wagombea 11 wamejitokeza kwenye kinyang’anyiro cha urais nchini Ufaransa huku wakiwasilisha mikakati yao ili wachaguliwe.

Kampeni za uchaguzi zilitia fora. Wagombea walichuana kwa hoja na kufafanua mambo mbalimbali ambayo watawafanyia wapigakura endapo watachaguliwa.

Wagombea kutoka mrengo wa kulia, Marine Le Pen na mwenzake mwenye misimamo mikali, Jean-Luc Melenchon, wamekosoa Jumuiya ya Ulaya na kwamba ikiwa watachaguliwa suala hili litakuwa kwenye ajenda zao za awali kabisa.

Kura za maoni zinaonesha kuwa uchaguzi wa mwaka huu utakuwa mgumu na wenye ushindani, huku takribani asilimia 30 ya wapiga kura wakiwa hawajaamua watamchagua nani.

Wadadisi wa mambo wanasema uchaguzi wa mwaka huu ni moja kati ya chaguzi ambazo hazitabiriki kwa kiwango kikubwa na kwamba mdahalo huu ulikuwa ni nafasi ya mwisho kwa wagombea hawa kuongea na taifa.

Marine Le Pen na Emmanuel Macron, ndio wagombea wanaoonekana kupewa sana nafasi ya kushinda kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi na kwamba huenda wakachuana wao wawili kwenye duru ya pili mwezi Mei.

Hata hivyo, wagombea wengine, Francois Fillon na mwenzake Jean-Luc Melechon, nao wameongeza umaarufu wao hivi karibuni na kuwakaribia Le Pen na Macron.

Vita ya Le Pen na Macron

Kwa mujibu wa utafiti wa maoni uliofanywa na shirika la Elabe kwa niaba ya kituo cha Televisheni cha BFM, mgombea anayewakilisha siasa za mrengo wa kati, Emmanuel Macron, anatarajiwa kushinda kwa kupata asilimia 24 ya kura, wakati mgombea wa chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, Marine Le Pen, anatazamiwa kufikia asilimia 21.5 ya kura.

Ndiyo kusema mchuano mkali utakuwa baina ya wagombea hao, ambapo mmojawapo anaweza kutangazwa mshindi na kurithi mikoba ya Rais Hollande.

Mgombea wa chama cha kihafidhina Francois Fillon, anafuatia katika nafasi ya tatu kwa kukadiriwa kupata asilimia 20 ya kura. Naye kiongozi mwenye mrengo wa kushoto, Jean- Luc Melenchon, alishika mkia kwa kupata asilimia 19.5 kwenye matokeo hayo ya utafiti.

Aidha, utafiti huo unaonyesha kuwa Macron mwenye umri wa miaka 39, anatabiriwa kushinda katika duru ya pili kwa kupata asilimia 65, wakati mshindani wake mkuu, Marine Le Pen, anatazamiwa kupata asilimia 35 ya kura. 

Hata hivyo, utafiti mwingine wa kura za maoni unaonyesha ikiwa Melenchon atafanikiwa kuingia katika raundi ya pili ataweza kuwashinda Le Pen na Fillon kwa urahisi lakini atapitwa na Macron.

Utafiti mwingine umeonyesha wapiga kura ambao bado hawajakata shauri wanafikia asilimia 40. Hata hivyo, inapasa kutilia maanani kwamba utafiti huo wa shirika la Elabe ulifanyika kabla ya kutokea mashambulio ya kigaidi ya mjini Paris ambapo polisi mmoja aliuawa na wengine wawili walijeruhiwa.

Hata hivyo, mgombea wa chama cha mrengo mkali wa kulia, Marine Le Pen, ameendeleza shutuma kali na kupinga sera ya uhamiaji ya Umoja wa Ulaya na kusisitiza kuwa endapo atachaguliwa kushika madaraka ya Ufaransa atahakikisha anawavua uraia wahamiaji wote nchini humo.

Mwanasiasa huyo ametajwa mara kadhaa kubwa mbaguzi kutokana na matamshi yake pamoja na mwenendo wa siasa ambazo zilisababisha bunge la Ulaya kumwondolea kinga ya kutoshtakiwa.

Le Pen aliwaambia waandishi wa habari kwamba, ugaidi ni vita inayowalenga wananchi na nchi yao yote ya Ufaransa.  Amesema Ufaransa haina budi kushinda vita hiyo.

Mwanasiasa huyo ametamka kwamba, itikadi kali ya Kisalafi hazina haki ya kuwapo nchini Ufaransa na zinapaswa kupigwa marufuku. Mwanasiasa huyo wa mrengo mkali wa kulia ametaka wale wanaohubiri chuki wafukuzwe nchini Ufaransa na misikiti yao ifungwe.

Naye mgombea, Emmanuel Macron, ameshauri kuwapo utulivu badala ya kuwachanganya watu kwa kuitumia kadhia ya ugaidi. Macron aliwaambia waandishi wa habari kwamba lengo la magaidi ni kuiyumbisha Ufaransa wakati ambapo wananchi wake wanauchagua mustakabali wao.

Uchaguzi chini ya ulinzi mkali

Kutokana na tukio la kigaidi lililotokea kwenye Kitongoji cha Champs Elysees nchini humo, Serikali ya Ufaransa imechukua hatua kali za usalama ili uchaguzi wa urais ufanyike katika hali ya utulivu, ulinzi na usalama wa kutosha.

Uamuzi huo umechukuliwa baada ya mkutano wa Baraza la Ulinzi lililokutana juzi asubuhi chini ya uenyekiti wa Francois Hollande.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Bernard Cazeneuve, hakuna kitakachozuia uchaguzi kufanyika. Alibainisha kuwa polisi zaidi ya 50,000 na kitengo kingine cha polisi kitakachosaidiwa na askari 7,000 wa kikosi cha ulinzi kitatumika kuimarisha usalama kwa ajili ya uchaguzi katika vituo vya kupigia kura 60,000.

Naye Waziri wa Mambo ya Ndani, Matthias Fekl, ametoa agizo kwa mameya wa miji kwamba kila kiongozi wa kituo cha kupigia kura anatakiwa kuwa na namba ya simu ya moja kwa moja kwa vikosi vya usalama.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles