27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Namungo FC ilivyosukwa kwa TPL

Zainab Dddy

NAMUNGO FC ni moja ya timu ngeni katika Ligi Kuu Tanzania Bara(TPL), baada ya ku­panda daraja msimu uliopita, ikitokea Ligi Daraja la Kwanza(FDL).

Timu hiyo yenye mskani yake Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi, ilikuwa ya kwanza kufuzu kushiriki Ligi Kuu msimu ujao wa 2019-20.

Katika ushiriki wake huo wa Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita, iliweka rekodi ya kumaliza ligi huku ikipoteza mchezo mmoja pekee.

Ilipanda daraja hadi Ligi Kuu, baada ya kukusanya pointi 42 huku ikiwa imesaliwa na michezo miwili mkononi na alama 42.

Kupata nafasi kwa Namungo Ligi Kuu, kumeongeza changamoto ya ushindani, hasa kutokana na mikakati ambayo timu hiyo imejiwekea katika kinyang’anyiro hicho kitakachoanza kutimua vumbi Agosti 23 mwaka huu.

MTANZANIA , limezungumza na Mwenyekiti wa Klabu ya Namungo, Hassan Zidadu.

Zidadu anabainisha mikakati yao katika ushiriki wao wa Ligi Kuu msimu ujao ambao ni wa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa klabu yake hiyo.

Mikakati hiyo ni pamoja na usajili uliofanywa na klabu hiyo katika dirisha kubwa la usajili.

KIKOSI KILIVYOSUKWA

Zidadu anasema katika kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu, waliamua kufanya usajili kulingana na matakwa ya kocha wao.

Anasema wamesajili wachezaji 23 na kuacha nafasi saba, ambazo zitazibwa kipindi cha dirisha dogo la usajili kama kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.

“Tuliowasajili kwa upande wa wachezaji wazawa ni Adamu Oseja, Lucas Chembeja, Mizar Kristom, Ally Korosho, Jukumu Kibanda, Faisal Mganga, Hamisi Mgunya,Paul Ngalema na Carlos Protus.

“Wengine ni John Mbise, Daniel Joram, Lukas Kikoti na Selemani Bwenzi, wakati washambuliji tutakuwa na Reliants Lusajo, Abeid Athumani, John Kelvin, Hashim Manyanya, Hamisi Nyenye, Ben Silvester na Jamal Dulaz”, anawataja.

Zidadu anasema mbali na wazawa Namungo pia imesajili wachezaji saba kutoka nje ya Tanzania, anawataja kuwa ni Nurdin Barola, Sure Piere Leopard, Sina Jerome, Bigirimana Blaise, Steve Nzigamasabo, Yusuph Aduhidy na Stiven Duwa,

BENCHI LA UFUNDI LABORESHWA

Zidadu anasema kuwa, walilazimika kuachana na kocha Bakar Malima ‘Jembe Ulaya’ baada ya kocha wao mkuu raia wa Burundi, Thierry Hitimana kutaka afanye kazi na kocha mwenye uwezo sawa na yeye, ili hata kama itatokea dharura atabeba majukumu bila tatizo.

“Katika hilo tulimpa jukumu la kumtafuta kocha anayehitaji kufanya nae kazi ndipo alipotuletea jina la Okoko Godfrey ambaye ni raia wa Rwanda

“Tuliyempa mkataba wa mwaka mmoja lakini pia tukamuongeza na Emmanuel Kingu ambaye atakuwa na jukumu la kuwafundisha makipa,”anasema.

MAANDALIZI

Zidadu anaeleza kuwa kikosi chao kilianza mawindo ya Ligi Kuu Julai 6 mwaka huu mjini Lindi lakini baadae wakarejea kujichimbia Ruangwa ambako ndiko maskani ya Namungo.

“Katika kambi yetu ya Ruangwa, mbali ya mazoezi timu imepata nafasi ya kucheza mechi za kirafiki si chini ya tano.

Pia tunatarajia kucheza michezo mingine ya kirafiki za na timu imara zinazoshiriki Ligi Kuu.

“Timu yetu ilianza mechi za kirafiki kwa kucheza na Aigle Noir ya Burundi ambapo tulishinda mabao 3-1, tukacheza na Lindi Kombaini waliotuchapa 1-0, kabla ya kurudiana nao na kulipa kisasi kwa kuwatandika mabao 5-0,”anasema Zidadu.

Anakumbuka mechi nyingine ya kirafiki ambayo kikosi chake kimekwishacheza kuwa ni dhidi ya Kombaini ya Kilwa ambayo walioshinda mabao 14-1.

Zizadu anafuchua kwamba pia wana mpango wa kukipiga na Polisi Tanzania ambayo itashiriki Ligi Kuu msimu wa 2019/20, baada ya kupanda daraja.

MATARAJIO

Anataraja malengo ya Namungo katika Ligi Kuu kuwa ni kuleta ushindani wa maana kwa kila timu watakayokutana nayo kama zilivyowahi kufanya Mbeya City, msimu wa kwanza baada ya kupanda daraja na KMC, ili wamalize ligi katika nafasi nne za juu.

“Katika kuhakikisha malengo tuliyoyaweka yanatimia, tulianza na kumbakisha kocha Hitimana ambaye kwetu ana viwango vya juu katika ufundishaji.

“Mbali ya kumbakisha, tumetoa nafasi ya kusajili mchezaji yoyote atakayemuhitaji pamoja na kupendekeza upya benchi lake la ufundi, vyote hivyo tumekamilisha.

“Uongozi kwa nafasi zetu, kilichobaki ni kocha kutuaminisha kile ambacho tayari tunacho kwenye vichwa kuwa ana uwezo wa kutimiza malengo yaliowekwa,”anasema.

KOCHA ACHIMBA MKWARA

Kwa upande wake kocha Hitimana anasema kuwa walijipanga kupanda TPL ndio maana wamefanikiwa hivyo hawatakuwa na hofu pale watakapokutana na changamoto mpya za ligi hiyo.

“Tumejipanga ndio maana tulipanda Daraja, ni wakati wetu sasa kuonyesha kwamba hatukubahatisha kupanda, hivyo hao wanaojiita vigogo wasitarajie kupata mteremko kutoka kwetu.

“Iwe Simba iwe Yanga hatuna hofu nazo kwa kuwa zote tumecheza nazo na hakuna kikosi ambacho kimebahatika kupata matokeo kirahisi hasa tukiwa katika uwanja wetu wa nyumbani.

“Jambo hili nasema kwa kujiamini kwa sababu nina kikosi bora kinachoweza kupambana na mpinzani yeyote na kumshinda,”anajitapa Hitimana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles