24.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 19, 2024

Contact us: [email protected]

Namna ya kumgundua mpenzi atakayekuumiza, asiyejali

CHRISTIAN BWAYA

WANAWAKE wengi hutamani kumpata mwanamume shujaa lakini mwenye mapenzi, mwenye msimamo lakini mwelewa na msikivu, anayejua kupenda lakini hateseki na wivu kupindukia.

Aidha, mapenzi yanapoanza si wanawake wengi hupata hata hisia kwa mbali kuwa wanajiingiza kwenye tanuru la moto. Hisia za mapenzi huwafanya wanawake wengi kuwa vipofu wasioweza kuona dalili za ukatili, usaliti na ubabe.

Baada ya kuoelewa, ndipo wanawake hawa wanapokuja kugundua kuwa walifanya makossa makubwa yanayoweza kugharimu furaha na maisha yao. 

Katika baadhi ya tabia hatari anazoweza kuwa nazo mwanamume, ni pamoja na kujiangalia mwenyewe, kutokufikiria mpenzi wake anatamani nini, tabia zinazoweza kusababisha matatizo makubwa kwenye ndoa. Maswali 12 yafutayo yanaweza kukusaidia kujua ikiwa uko kwenye uhusiano na mwanamume  katili mwenye ubinafsi wa hali ya juu au la. Soma swali kisha chagua namba inayojibu kile anachofanya mpenzi wako.

Mpo kwenye sehemu ya kupata huduma, mhudumu amefanya kitu kinachomkera. Unadhani atafanyaje?

Atamtukana au hata kumpiga kama atakereka zaidi. Ataonesha dharau na atasusia huduma; ataonesha kukasirika lakini hatasusia huduma; ataeleza kutokuridhishwa kwake kwa ustaarabu.

Inapotokea hali ya kutokuelewana kati yenu atafanyaje?

Atanyanyuka na kuondoka; atanipigia kelele au kuongea wakati na mimi ninaongea; atanyamaza na kuzira kwa muda; ataniacha niongee na kunisikiliza.

Mnapojadiliana jambo na ikaonekana anashindwa hoja huwa anafanyaje?

Atakasirika sana. Lazima yeye awe mshindi siku zote; ataniumiza kwa maneno akitaka nijue alivyonikasirikia; anaweza kukasirika lakini ataongea kwa lugha ya kistaarabu; atakubali kushindwa.

Umewahi kuhisi amekusaliti kimapenzi?

Mara nyingi ingawa hakubali; mara nyingi na amekubali nikamsamehe; sijawahi kuona dalili lakini najua anaweza kunisaliti. Nina hakika hawezi kamwe kunisaliti kimapenzi.

Ikiwa amekuomba kitu na umeshindwa kumpa, kitu gani anaweza kukifanya kati ya haya:

Atakasirika na kunishambulia kwa maneno ya kashfa; ataonesha kunipuuza na kuzira kwa siku kadhaa. Atakasirika lakini hatutaacha kuongea.

Ataelewa na kutambua kuwa si mara zote atapata kile anachokitaka.

Unamwonaje mtazamo wake kuhusu tabia ya usiri?

Mambo yake mengi ni ya siri. Nikishika simu yake ni ugomvi. Ananiruhusu nifahamu vitu anavyojua havina umuhimu mkubwa kwenye maisha yake. Hapendi nijue mambo fulani fulani. Anapenda faragha lakini sio msiri kwa mambo ya msingi.

Inapotokea umepata mafanikio kazini, umepanda cheo, umefaulu mtihani au kuna jambo zuri limekupata:

Hatajali na hataonesha furaha; atanipongeza lakini hataichukua muda atasahau; atapongeza kama kuna mtu mwingine amenipongeza; atafurahi na hataacha kuzungumzia kilichotokea.

Unaelezaje tabia yake kuhusu mavazi

Hutumia muda mwingi akifikiria ataonekanaje kimavazi. Anaweza kubadili nguo mara mbili lakini hajali nitavaa nini.

Anatumia fedha nyingi kwenye mavazi hata kama si lazima. Anajali unadhifu wake na wangu; hana muda na mavazi; nguo zake nyingi zinafanana na haimchukui muda kuvaa.

Unamwelezeaje tabia zake kuhusu mambo ya maendeleo kifedha, kijamii au kiuchumi?

Muongo; anapenda kukuza mafanikio yake. Kama humfahamu unaweza kufikiri amefanikiwa lakini kumbe hana lolote;

anapenda kujionesha hata kama kweli amefanikiwa. Msiri, hawezi kuzungumzia mambo yake kwangu huwa nayasikia tu kutoka kwa wengine.

Anaishi maisha ya faragha mara nyingi kuliko kile alichonacho.

Inapotokea umetofautiana na ndugu zake na makosa yao yako wazi:

Atawatetea hata kama anajua ninaumia. Familia yake haiwezi kukosoea; ikiwa anaamini wako sahihi hatajali ninajisikiaje lazima awatetee. Hatahangaika kujua kulikoni. Lazima atapuuza na kutaka nisisumbuliwe na vitu vidogo.

Atatafuta ufumbuzi bila kuniumiza wala kuwaumiza wao. Hapendi kuona mtu anaonewa.

Mpo mahali mnatakiwa kusimama kwenye foleni. Unavyomjua atafanyaje?

Hatajali wengine wanasubiri. Atalazimisha kupita awahi bila kuwaomba aliowakuta

Hatasubiri ila ataomba aliowakuta wamruhusu kupita kwa kusingizia dharura.

Anaweza kusubiri kwenye mstari lakini hataruhusu wengine wenye dharura.

Anaweza kusubiri bila kulalamika au akaamua kuondoka arudi baadae.

Tangu ulipokutana naye kwa mara ya kwanza, unadhani amebadilika?

Ndiyo, amebadilika. Zamani alikuwa mpole na mwelewa sijui amekuwaje siku hizi.

Sijui nisemeje kwa sababu ni kama simfahamu. Mara nyingi ni mtu wa siri.

Hata sijui nisemeje kwa sababu simwelewi;

hajabadilika. Tabia alizokuwa nazo wakati huo bado anazo leo.

Jumlisha alama zote. Ikiwa umepata alama kati ya 12 – 15, mpenzi wako ni mtu katili asiyejali hisia za watu. Tafuta ushauri wa kitaalam. Alama 16 – 24, mpenzi wako ana tabia za ukatili wa wastani ila usizipuuze; alama 25 – 36, ana upungufu unayovumilika; alama 38 – 48 mpenzi wako ni mtu muungwana mwenye utu.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Mawasiliano 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles