30.9 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Namna ya kumfanya mtoto apende kusoma

reading-with-kids

Na CHRISTIAN BWAYA,

KUSOMA si tabia nyepesi kuijenga hususani katika jamii yetu inayotegemea simulizi na mazungumzo kama njia ya kujielimisha.

Tumelelewa katika mazingira yasiyosisitiza umuhimu wa kusoma. Hata hivyo, kusoma ni tabia isiyokwepeka katika ulimwengu huu unaotulazimisha kuyasaka maarifa.

Kadhalika, mafanikio ya mtoto kitaaluma yana uhusiano wa moja kwa moja na utamaduni wa kujisomea. Kwa hivyo, kama kweli tunatamani watoto wetu wawe na tabia ya kujisomea bila kushurutishwa, tunao wajibu mkubwa wa kuwajengea utamaduni huo tangu wangali wadogo. Katika makala haya tunatazama mbinu nne kubwa zinazoweza kuwasaidia watoto wetu kupenda kusoma.

Kuweka mazingira ya kujisomea

Mazingira yanayohamasisha kujisomea ni pamoja na kuhakikisha vitabu vinapatikana nyumbani. Mtoto anapoona vitabu tangu akiwa mdogo huamini kuwa ni sehemu ya maisha yake ya kila siku. Kwa kutambua umuhimu huo, mzazi anashauriwa kukusanya vitabu, magazeti na machapisho mbalimbali na kuyatunza  nyumbani. Sambamba na hilo, tunaweza pia kupunguza muda wa watoto kutazama televisheni. Ni vigumu kudhibiti maudhui ya vipindi vya televisheni lakini tunaweza kudhibiti namna chombo hicho kinavyotumika vyumbani.

Kuwa mfano kwa kusoma

Hatuwezi kumfundisha mtoto tabia ambayo sisi wenyewe hatuna. Kama tunataka mtoto apende kusoma, tunashauriwa sisi wenyewe tujifunze kupenda kusoma. Kwa kawaida, mtoto hujifunza kwa kile anachokiona mzazi akikifanya kuliko anachokisema. Tunapoonekana tukisoma mara kwa mara, ni rahisi mtoto kuiga mazoea hayo.

Aidha, si lazima mzazi kusoma vitabu asivyovipenda kwa lengo la kuigiza tu utamaduni wa kusoma. Kuna magazeti, majarida na vitabu rahisi ambavyo kila mzazi anaweza kuvisoma awapo nyumbani. Vile vile, vipo vitabu vya lazima kiimani, ambavyo kwa hakika hatuwezi kuwa waumini imara bila kuvisoma. Ni vizuri mtoto aone tukivisoma tuwapo nyumbani.

Kumsomea hadithi

Mtoto hawezi kuthamini tu kile anachokiona bila kuona umaana wake katika maisha yake. Kwa kawaida, watoto wadogo wanapenda hadithi zenye visa mbalimbali vinavyowakuza uelewa wao. Kwa hivyo, kumsomea hadithi zinazomvutia kuliko kumsimulia husaidia kutambua thamani ya vitabu.

Kwa mfano; yapo masimulizi mengi katika vitabu vitakatifu tunayoweza kutafuta vitabu vyake na kuwasomea watoto wetu. Mazoea ya kuwasomea hadithi, hata kwa dakika chache kwa siku, mbali na kusaidia kujenga ukaribu na mtoto, yanamfanya mtoto ajenge shauku ya kujua kusoma mwenyewe ili aweze asome hadithi hizo yeye mwenyewe. Anapokua na tabia hii, haitakuwa kazi ngumu kuwa msomaji mzuri wa vitabu atakapokuwa mtu mzima.

Kumpa motisha anapojisomea

Kwa kufanya matatu tuliyoyaona, ni rahisi mtoto kuanza kuiga tabia ya kusoma. Mara anapoanza kuonesha kupenda vitabu, tunahitaji kumpa motisha ili kuiendeleza tabia hiyo. Kwa mfano; anapodai kusomewa hadithi jioni kwa mazoea yaliyoanza kujengeka, motisha ni kutimiza shauku hiyo kwa kumsomea pasipo kutoa visingizio vyovyote.

Kadhalika, badala ya kuwaletea watoto zawadi za pipi na vitu vingine vya kawaida, tunaweza pia kuwaletea vitabu vya hadithi wanazozipenda na kuwasomea. Katika umri mdogo, mazoea haya hujenga tabia imara ya kupenda kujisomea.

Kwa hakika, pamoja na changamoto zake, inawezekana kabisa kuwajenga watoto kuwa wasomaji wazuri. Kilicho muhimu katika yote ni sisi wazazi kuona umuhimu wa kujisomea kwa kuwa mfano wa usomaji wa vitabu tuwapo nyumbani.

Mwandishi ni mwalimu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Anapatikana kwa [email protected], 0754 870 815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles