23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NAIONA SAFARI YA MWISHO YA YANGA 

Na ZAINAB IDDY



MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao pia ni wawakilishi pekee kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, Yanga, wamepangwa kucheza dhidi ya MC Alger ya Algeria kwenye mechi ya mchujo, kabla ya kuingia kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo.


Yanga imepata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho, baada ya kutolewa kwenye raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Zanaco, ambapo kwenye mechi ya kwanza wakiwa nyumbani walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Wazambia hao kabla ya kulazimishwa sare ya bila kufungana kwenye mechi ya marudiano, hivyo kutolewa kwa bao la ugenini.


Kwa kanuni za Shirikisho la Soka Afrika (CAF), timu zote zilizotolewa kwenye hatua hiyo ya Ligi ya Mabingwa, zinapata fursa ya kucheza hatua ya mtoano kwenye Kombe la Shirikisho na kupitia droo yao iliyochezeshwa Jumanne ya wiki iliyopita, Yanga itaanza nyumbani Aprili 7, 8 au 9, kabla ya kurudiana nchini Algeria Aprili 14 hadi 16.


Yanga kupangwa na timu zinazotoka ukanda wa Kaskazini mwa Afrika, itakuwa ni mara ya 16 na mara 15 ilizocheza haijawahi kuwatoa kwenye mashindano yoyote yale wanapokutana, lakini wakiwa wameshinda mara mbili tu wakiwa nyumbani kuanzia mwaka 1982.
Hapa ndipo ninapoiona safari ya mwisho ya Yanga kimataifa, kwani licha ya rekodi isiyoridhisha waliyonayo kwa Waarabu, Mouloudia Club d'Alger  wengi hupenda kuiita MC Alger si timu ya kubeza ukizingatia na maandalizi ya zimamoto waliyonayo Wanajangwani hao mwaka huu. 

MC Alger ilianzisha mwaka 1921, ikijulikana kama Mouloudia Chaabia d'Alger na baadaye mwaka 1977 ikaanza kujulikana kama Mouloudia Petroliers d'Alger na ilipofikia mwaka 1986, ikabadilishwa tena jina na kuanza kujulikana kama Mouloudia Club d'Alger.

MC Algeria ndiyo klabu ya kwanza kushinda kombe la michuano ya kimataifa, baada ya kubeba ubingwa wa Klabu Bingwa ambayo sasa ndiyo Ligi ya Mabingwa Afrika.

Hii ni moja ya klabu yenye mafanikio zaidi nchini humo, licha ya kwamba kuna klabu nyingine kubwa na maarufu kama JS Kabylie, USM Alger na ES Setif kwani imeshinda makombe saba nchini kwao yakiwa ni ya ligi, lakini ikinyakua pia makombe saba tena katika mashindano mengine.

Katika kipindi hiki, MC Alger inaonekana kuamua kurejesha heshima yake, baada ya kuonyesha kiwango bora kwenye ligi ya nchini kwao, wakiwa nafasi ya nne kabla ya mchezo wao wa jana (Jumapili) dhidi ya JS Kabylie.

Kwenye mechi za kimataifa timu hiyo imeonyesha uwezo mkubwa, tofauti na Yanga wanaonyesha wazi msimu huu si wa kwao na hivyo kutakiwa kujipanga upya mwakani, iwapo kama watatetea taji lao la ligi au lile la Kombe la FA.

Ingawa Yanga wanaweza kujipa moja kuwa mpira ni dakika 90, lakini pia mpira unadunda, mbele ya wapinzani wao wanatakiwa kufanya kazi ya ziada ili waweze kusonga mbele kwa jinsi wenzao walivyoonekana kujiandaa.

Yanga wanapaswa kuwa makini na kama maandalizi basi yawe bora, lazima wajiandae hasa na lazima wawe jasiri kwa kutaka kufanya vema kwa kuwa hakuna kinachowezekana, lakini haitakuwa rahisi kwao kupenya mbele ya Waarabu hao, jambo ambalo ni wazi safari ya Yanga kimataifa inaweza kufika ukingoni pindi watakapokutana nao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles