22.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

Naibu Waziri wa Madini Dk. Kiruswa ailekeza GST kufanya Utafiti Longido

Na Mwandishi Wetu, Longido

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST)  imetakiwa kufanya utafiti ili kujua aina za madini yaliyopo katika maeneo yenye shughuli za uchimbaji mdogo wa madini wilaya ya Longido.

Wito huo, umetolewa Juni 4, 2022 na Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa wakati akifunga semina ya siku mbili iliyotolewa kwa wazee wa mila na wataalam wa Wizara ya Madini ikilenga kuwaelimisha masuala mbalimbali yanayohusu Sheria ya Madini, Uchimbaji,  Usimamizi wa Mazingira na Wajibu wa migodi kwa jamii katika maeneo ya uchimbaji wilayani Longido mkoa wa Arusha.

Dk. Kiruswa amesema hayo baada ya kupokea maoni kutoka kwa wazee wa mila, wadau, wafanyabishara na wachimbaji wadogo wa madini kuwa wanachimba kwa kubahatisha.

Amesema GST inatakiwa ifanye utafiti wa kutosha katika wilaya ya Longido hususan katika eneo la Matale yanapochimbwa madini ya Ulanga ili kuondokana na uchimbaji wa kubahatisha.

Amesisitiza kuwa, wanakosa taarifa za kijiolojia ya maeneo hayo ili wachimbe kwa tija.

“Baada ya wao kuwa wamepata elimu na wanajua taratibu zilizopo, ninatoa wito kwa GST wafanye haraka na wafike kufanya utafiti ili kujua kuna aina gani ya madini na ikiwezekana watengeneze ramani ili wananchi waone maeneo yenye rasilimali madini,” amesisitiza.

Pia, semina hiyo imesaidia kutoa uelewa mpana wa shughuli zinazofanyika katika Sekta ya Madini katika masuala ya Sheria, Leseni, Utafiti, Ushirikishwaji wa Watanzania na Wajibu wa Makampuni kwa jamii zinazozunguka migodi.

Vilevile, amesema kuwa elimu hiyo waliyoipata ni hatua muhimu ambayo itasaidia kutekeleza shughuli za madini kwa wale wanaohitaji kuwekeza na ambao wamepata elimu ya  namna gani wanaweza kuomba leseni za uchimbaji, uongezaji thamani madini ya Vito na kusafirisha kwenye masoko ya madini ndani na nje ya nchi na biashara ya madini.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Longido, Nurdin Babu, amewataka wazee wa mila na wadau wa Sekta ya Madini kujitokeza kuwekeza katika biashara ya madini ili kutumia elimu waliyoipata katika mafunzo baada ya kuelimishwa na Wataalamu kutoka Wizara ya Madini.

Semina imetolewa katika wilaya ya Longido na wataalam wa Wizara ya Madini imelenga kuelimisha fursa zilizopo katika Sekta ya Madini, Kanuni na Miongozo mbalimbali ya Taasisi za wizara na Sheria ya Madini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles