Na Mwandishi Wetu, Longido
NAIBU Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa amepiga marufuku wachimbaji wa madini kuchimba kiholela bila kuzingatia utaalamu wa kuchimba, kwani hali hiyo hupelekea vifo vya watu kwa kufukiwa na vifusi.
“Nimepata taarifa hapa kulishatokea vifo vya watu kwa kufukiwa na vifusi, udongo wa hapa ni tifutifu. Naomba mzingatie uchimbaji wa kitaalam, acheni uchimbaji wa njia za asili,” amesema Dk. Kiruswa.
Dk. Kiruswa ametoa agizo hilo leo Januari 28, 2022 alipokuwa kwenye muendelezo wa ziara ya kikazi wilayani Longido mkoani Arusha.
Ni baada ya kutembelea migodi ya madini ya vito aina ya Sunstone na Quartz yanayochimbwa na Kampuni ya Loorukudita ya Mwekezaji mzawa iliyopo Kijiji cha Matale A katika Tarafa ya Engarenaibor.
Amesema, eneo hilo limebainika kufanya uchimbaji ambao ni hatari kwa usalama wa wananchi ikiwemo kimazingira na kuonekana watu kuingia kiholela kujichimbia madini bila kufuata taratibu za Serikali na kijijini ambapo amesema hali hiyo ni kama wizi wa madini.
“Uchimbaji huu wa kiholela unatokana na ukosefu wa elimu, hivyo naagiza Tume ya Madini kufika hapa kutoa elimu kwa jamii,” amesema Dk. Kiruswa.
Dk. Kiruswa ameeleza kuwa imebainika watu wanajimilikisha maeneo na kuanza kuchimba bila kufanya utafiti hivyo amewataka STAMICO kufanya utafiti wilayani humo ili kubaini madini mbalimbali yanayotajwa kupatikana katika maeneo hayo.
“Wilaya hii inaongoza kwa madini mbalimbali mkoani Arusha, hivyo naomba wafike kutafiti kama ni kweli na wazawa tumieni fursa za uwekezaji kwa kumiliki vitalu vya uchimbaji na kuacha kuilaumu Serikali inavyotoa vibali kwa watu kutoka nje ya wilaya, kwani kila mtanzania anayo haki ya kuwekeza popote nchini ilimradi afuate taratibu za kisheria,” amesema Dk. Kiruswa.
Akielezea hali ya mgodi huo, Afisa Tarafa wa Engarenaibor, Isaya Samweli, amesema Kata ya Matale machimbo bubu ya migodi yamekuwa mengi, hivyo wilaya ilishatoa maelekezo kusitishwa kwa machimbo yote yanayoendelea kinyume na Sheria.
Mmiliki wa Mgodi wa Loorukudita, Paulo Lekoole amesema alianza uzalishaji Mwaka 2019 kwa njia za asili bila kutafuta kibali na alidai kuwa alikuwa akifanya utafiti na kijiji kilimpatia ekari 4 lakini baadaye alitafuta leseni na wizara ikampatia ekari tisa.
Amesema katika uzalishaji wa madini hatumii upigaji wa baruti bali huchimba kwa kutindua na kutumia skaveta na amefanikiwa kuzalisha tani mbili za madini hayo yakiwa na rangi tatu ambayo ni Moon stone, Kijani na Rangi ya karoti( Double Colors) lakini kazi za mikono hazizalishi kwa ubora.
“Afisa anayesimamia shughuli za Madini Tarafa ya Engarenaibor, Baza Meshack amesema Mwaka 2019 mgodi ulizalisha kwa kasi na migogoro iliibuka kwani watu walikuwa wakiingia usiku kwenye machimbo kinyume na Sheria lakini pia ni hatari kufanya shughuli za uchimbaji usiku, hivyo tulisitisha uchimbaji wa usiku,” amesema Meshack.
Hata hivyo, amesema kuna watu waliojitokeza na kuanzisha uchimbaji nje ya mgodi huo ambapo walifanikiwa kuwadhibiti lakini wakaendelea kuchimba kwa siri na baadaye kuna mtu aliangukiwa na kifusi na kuumia sehemu ya kiuno.
“Katika kufanya tathimini ya madini yaliyochimbwa kwenye mgodi huo Mwaka 2021 Mwezi Julai hadi Desemba walipata kilo 14,271 thamani yake ikiwa ni Sh milioni 109.2, mraba wa serikali ikiwa ni Sh milioni 5.7 na ada ya ukaguzi ikiwa Sh milioni, moja,” amesema Meshack.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Nurdin Babu amesema, kipaumbele cha kwanza ni kuzingatia usalama wa wakazi wa wilaya hiyo na kuwataka kuepuka tabia ya utoroshaji wa madini na kupelekea serikali kukosa mapato.
Naye, Kamishna wa Madini  kutoka Wizara ya Madini, Dk. Abdulrahman Mwanga amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za watuy wanaovamia maeneo hayo na kufanya uchimbaji kiholela kinyume na Taratibu za Nchi.