23.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

NAIBU WAZIRI AMUONYA MWEKEZAJI PANGANI


Na OSCAR ASSENGA-PANGANI

NAIBU Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Jumaa Aweso, ametishia kutompa ushirikiano mwekezaji wa Kampuni ya Amboni Plantation anayejishughulisha na kilimo cha mkonge iwapo hatabadilika na kusaidia miradi ya maendeleo kwenye vijiji na vitongoji vinavyomzunguka.

Aweso ambaye pia ni Mbunge wa Pangani (CCM), aliyasema hayo juzi wakati wa ziara yake ya kutembelea Kituo cha Afya cha Mwera na kuona mradi wa ujenzi wa baadhi ya majengo ulivyokwama baada ya mwekezaji huyo kugoma kutoa sehemu ya ardhi yake.

Pamoja na mambo mengine, naibu waziri huyo alikagua ujenzi wa sehemu ya upasuaji na ukarabati wa miundombinu iliyopo katika kituo hicho cha afya.

“Kitendo cha mwekezaji huyo kushindwa kuwathamini wananchi na kushindwa kushiriki kwenye shughuli za kijamii ikiwamo kuchangia miradi inayotekelezwa kwenye kata hiyo ikiwamo elimu, afya na miundombinu, kinakwenda kinyume na taratibu za uwekezaji huo.

“Kwa hiyo, nasema mwekezaji ambaye amewekeza kwenye kata hii na amechukua eneo kubwa la ardhi ambayo ni mali ya Watanzania waliopo kwenye eneo hili na akagoma kushiriki shughuli za maendeleo, sitampa ushirikiano.

“Ni jambo la ajabu kwa mwekezaji huyu na haiingii akilini kwa kitendo chake cha kukataa kutoa sehemu ya ardhi yake kwa ajili ya ujenzi wa jengo la upasuaji.

“Nakumbuka mwaka jana aliyekuwa Naibu Waziri wa Tamisemi ambaye sasa ni Waziri wa Wizara hiyo, Seleman Jafo, alimwagiza mwekezaji huyo atoe ushirikiano na kuwa mstari wa mbele kusaidia miradi ya kijamii, lakini nashangaa mpaka leo amekuwa akisuasua, hii ni aibu na dharau kwa Serikali.

“Wakati mwekezaji huyo anayafanya hayo, ieleweke kwamba ni utaratibu wa kawaida kwa mwekezaji kuhakikisha wananchi wananufaika kupitia uwepo wake, jambo ambalo kwa mwekezaji wetu halifanyiki,” alisema Aweso.

Awali, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Juma Mfanga, alisema wameshindwa kuendelea na ujenzi wa majengo baada ya mwekezaji huyo kugoma kutoa sehemu ya ardhi yake.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Issa, alisema ujenzi wa majengo hayo utakamilika Mei 30, mwaka huu badala ya Machi 30, mwaka huu kama ilivyokuwa imepangwa awali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles