Derick Milton, Simiyu
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuchukua hatua kali dhidi ya taasisi zote za serikali ambazo zimeshindwa kulipa madeni yao kwa wakati.
Aidha, amewaagiza wakuu wa wilaya kulichukua suala hilo la madeni ya umeme kwenye taasisi za serikali kama moja ya ajenda zao katika vikao vyao vya kila siku, kwani madeni yao yanaweza kusababisha shirika hilo likashindwa kujiendesha lenyewe.
Amesema hatua ambazo zinachukuliwa kwa sasa bado hazitoshi kwani deni linaendelea kukua.
Naibu Waziri huyo ametoa agizo hilo leo Jumatano Septemba 18, wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Gusuma kilichopo wilayani Bariadi mkoani Simiyu, katika hafla ya kuwasha umeme kwenye kijiji hicho.
“Meneja wa Mkoa endelea kuchukua hatua za kisheria, nimeona tayari umeshaanza kuchukua hatua hizo, lakini hazitoshi deni linazidi kukua endelea kuwachukulia hatua wale wote ambao hawajalipa madeni yao.
“Shirika limepewa jukumu la kusaidiana na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kusambaza umeme katika maeneo yote ambayo bado hayajafikiwa na umeme nchini ifikapo Juni 2021 hivyo ikiwa wateja hawatalipa madeni yao ndani ya muda stahiki, shirika halitafanya kazi kwa ufanisi,” amesema.
Pampja na mambo mengine, amesema kwa sasa shirika hilo linajitegemea lenyewe na halipokei ruzuku tena kutoka serikalini na Wizara ya Nishati haitaki kuona shirika hilo linafikia hatua ya kuomba tena ruzuku ili kujiendesha.