RAMADHAN HASSAN,DODOMA
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson ametoa Sh. milioni moja kwa ajili ya kuichangia Klabu ya mpira wa miguu ya Yanga huku akitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa kuichangia timu hiyo.
Dk Tulia ametoa mchango huo leo Mei 28, ofisini kwake bungeni jijini Dodoma kwa kuukabidhi kwa viongozi ambao ni wabunge wapenzi wa Yanga wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya kuhamasisha michango ya timu hiyo, Anthony Mavunde.
Wabunge wengine waliokuwepo katika kupokea mchango huo ambao ni wapenzi wa Yanga ni Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini-CCM), Vanance Mwamoto (Kilolo-CCM), Mohamed Mchengerwa (Rufiji-CCM) na Mussa Ntimizi (Igalula-CCM).
Akizungumza kabla ya kukabidhi mchango huo, Dk.Tulia amesema aliahidi kuichangia timu hiyo na sasa anatimiza ahadi yake.
“Niliahidi kuchangia Yanga na nimekabidhi Sh. milioni moja na ninawaomba sana Watanzania kuwachangia Yanga kwani wanahitaji sana michango.”amesema Dk Tulia.
Aidha ametoa wito kwa Watanzania kujitokeza Juni 15, 2019 katika shughuli iliyoandaliwa na Yanga ambayo imepewa jina la ‘Kubwa Kuliko’ itakayofanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee.
Akipokea mchango huo kwa niaba ya kamati ya hamasa na michango ya Yanga, Mavunde amemshukuru Dk Tulia kwa kutekeleza ahadi aliyoahidi kwa kuishi maneno yake.
“Sisi sio ombamba ila ni wanachama wanaichangia Yanga na Juni 15, 2019 katika tukio la Kubwa Kuliko nchi itakwenda kutikisika,” amesema Mavunde ambaye ni Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana