27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 16, 2024

Contact us: [email protected]

Naibu Spika asaidia shule ya msingi aliyosoma Rugwe

NAIBU SPIKA5Na KENNETH NGELESI, RUNGWE

NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ametoa msaada wa Sh milioni tano kwa Shule ya Msingi Mabonde iliyopo mjini Tukuyu wilayani Rungwe, Mkoa wa Mbeya.

Dk. Tulia alitoa msaada huo jana baada ya kuridhishwa na mchanganuo wa matumizi ya fedha kama hizo alizotoa shuleni hapo Februari mwaka huu, alipotembea shule hiyo aliyosoma kuanzia mwaka 1984 hadi 1990.

Akizungumza na walimu, wanafunzi na wajumbe wa kamati ya shule hiyo katika viwanja vya shule hiyo, Dk. Tulia alipongeza kamati ya shule pamoja na uongozi wa shule ulio chini ya Mwalimu Mkuu, Aswile Mwaisaka, kwa usimamizi mzuri wa fedha alizotoa awali kwa ajili ya ukarabati wa vyumba vitatu vya madarasa na shimo la choo.

“Ni kawaida yangu kutembelea na kukagua kile nilichokitoa kama kimefanya kazi iliyokusudiwa. Kwa kweli nimeridhishwa na mchanganuo wa matumizi ya fedha nilizotoa awali.

“Kwa hiyo, nitaongeza tena Sh milioni tano kwani katika taarifa yenu mmeonyesha kuwa kuna fedha mmechukua katika mfuko wa shule ili kukamilisha kazi iliyokuwa ikifanyika.

“Kitendo cha kutumia fedha vizuri, kinaonyesha ni kwa jinsi gani mnavyothamini michango ya wahisani, ndiyo maana nalazimika kuwapa fedha nyingine,” alisema Dk. Tulia.

Pamoja na kutoa kiasi hicho cha fedha, aliwataka pia walimu waendelee kutoa elimu bora itakayowasaidia watoto hao.

Pia, aliwataka wanafunzi hao wasome kwa bidii kwani hadi sasa hawajui watakuwa na madaraka gani pindi watakapokuwa wamehitimu masomo yao.

“Someni kwa bidii na pia toeni ushirikiano kwa walimu wenu kwa sababu bila kufanya hivyo, hamuwezi kufanikiwa kimaisha,” alisema.

Awali, akisoma taarifa ya shule hiyo, Mwalimu Mwaisaka alimshukuru Naibu Spika kwa kukumbuka shule aliyosoma na kusaidia kutatua changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Pia, aliahidi kutumia vizuri fedha zilizotolewa na Naibu Spika kama alivyofanya katika fedha alizotoa awali.

Katika ziara yake wilayani Rungwe, Dk. Tulia alitoa msaada wa mifuko 100 ya saruji kwa kikundi cha Karasha Kikoba kilichoko Kata ya Kiwira kinachofyatua matofali.

Pia, alitembelea Shule ya Msingi Mchanganyiko Katumba II kukagua matumizI ya fedha alizotoa Februari mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles