23.6 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 10, 2024

Contact us: [email protected]

Naibu Meya Kinondoni ashtukia mchezo sanduku la maoni kituo cha afya Tandale

Na Winfrida Mtoi, Mtanzania Digital

Naibu Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Michael Urio amefanya ziara katika kituo cha afya cha Kata ya Tandale kuona utoaji wa huduma na kubaini changamoto mbalimbali, ikiwamo masanduku ya maoni ya wananchi hatofunguliwa kwa wakati.

Urio ambaye Diwani wa Kata ya Kunduchi, amefanya ziara hiyo leo Agosti 26,2024 ikiwa ya kwanza tangu alipochaguliwa katika nafasi hiyo wiki iliyopota.

Alipofika katika kituo hicho cha afya, alipokelewa na Mganga Mfawidhi, Dk. Wilfred Barinzigo ambaye alimueleza changamoto mbalimbali, lakini akahitaji kufungua pia sanduku la maoni ya wananchi kujua walichoandika.

Hata hivyo alishindwa kusoma kilichopo ndani ya masanduku hayo baada ya ufunguo kukosekana ikidaiwa anayeutunza hakuwepo eneo hilo.

Kutokana na hali hiyo, Naibu Meya huyo amemuagiza Diwani wa Kata ya Tandale, Abdallah Said ‘Chief’ kuweka sanduku binafsi ili apate maoni ya wananchi.

“Haya masanduku ya hamuyafungui ndio maana leo natafuta funguo zake hazipatikani. Daktari ni lazima kufuatilia wananchi wanataka nini na si kwa Tandale tu, ni lazima kufuatilia malalamiko na maoni ya wananchi.

Kama mimi nimekuja hapa nilitamani nipate kuona maoni ya wananchi kupitia masanduku tuliyoyaweka lakini naona hayajafunguliwa miezi kadhaa. Mheshimiwa Diwani na wewe sio vibaya hata ukaongeza sanduku lingine la maoni hata ukasema ni la Diwani, ukawa unapitia ukajua wananchi wanahitaji nini,” amesisitiza Naibu Meya Urio.

Aidha ameahidi kuhamasisha kuhakikisha changamoto ya ufinyu eneo na udogo wa wodi ya wazazi vinatatuliwa kutokana na mchakato huo kuanza.

Amesema atazungumza na Meya na Mkurugenzi wa Kinondoni ili kupata eneo wanalohitaji kwa ajili ya upanuzi wa kituo hicho cha afya.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Tandale, Dk. Barinzigo, amesema wanahudumia watu 1000 kwa siku sawa na 30,000 kwa mwezi hivyo kutokana na baadhi ya changamoto hasa ufinyu wa wodi ya wazazi wanalazimika kuwapa rufaa wengine kwenda vituo vingine vya afya.

Dk. Barinzigo amesema wanatoa huduma zote zinazohitajika kwa wagonjwa wa nje na ndani na lengo lao ni kutaka kupunguza msongamano katika hospitali kubwa endapo watapata eneo kubwa la kuongeza majengo na huduma.

Katika hatua nyingine Urio alifanya ziara kwenye mradi ujenzi wa shule ya Sekondari ya Abbas Tarimba na kubaini mkandarasi hayupo kazini kwa muda mrefu ambapo aliahidi kushughulikia changamoto hiyo ili madarasa yakamilike kwa wakati na kupokea wanafunzi Januari mwakani.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Tandale, Chief amemshukuru Naibu Meya huyo kwa kufanya ziara katika kata yake na kuahidi kuweka sanduku la maoni ndani ya wiki moja kama alivyomuagiza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles