WASANII wa kizazi kipya hapa nchini wanaounda kundi la Navy Kenzo, Nahreel na Haika, juzi walipagawisha mashabiki katika bonanza la kuhamasisha upatikanaji wa huduma za uzazi wa mpango Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam.
Mbali na wasanii hao, wasanii wengine ambao walikuwa kivutio kwa mashabiki ni pamoja na Mwasiti, Barnaba na kundi la vichekesho la ‘Vituko Show’ ambapo bonanza hilo lilifanyika kwenye viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, likisimamiwa na ‘Marie Stopes Tanzania’.
Katika tamasha hilo kulikuwa na viongozi mbalimbali wa Serikari wakishirikiana na zaidi ya vijana 1,000 kutoka vikundi mbalimbali vya uhamasishaji.
Akizungumza katika bonanza hilo, Mkurungezi Mkuu wa Marie Stopes Tanzania, Anil Tambay, alisema: “Hiki ni kizazi kikubwa zaidi cha vijana katika hisoria ya Tanzania, asilimia 54 ya Watanzania wapo chini ya umri wa miaka 20. Mafanikio yao ni maendeleo ya uchumi wa Tanzania, lakini kuna wakati matarajio ya vijana yanaharibiwa au wakati mwingine yanaishia pabaya kutokana na mimba zisizotarajiwa, ila uzazi wa mpango ni silaha ambayo vijana wanaweza kuitumia kupangilia maisha yao,” alisema Tambay.