23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mzumbe waja na mwarobaini wa ndoa za utotoni

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Prof. William Mwegoha, leo Agosti 10, 2022 amezindua programu maalumu ya elimu na ufuatiliaji kimtandao “TOKOMEZA” pamoja na mwongozo wa mafunzo kwa Maafisa Ustawi wa Jamii, ambao utawasaidia katika kushughulikia changamoto ya ndoa za utotoni ambazo zimekuwa na madhara makubwa ya kiafya kwa watoto. 

Dk. Seraphina Bakta, Mratibu wa Mradi wa Utafiti kuhusu changamoto za kiafya zitokanazo na Ndoa za Utotoni, akiwasilisha matokeo ya Utafiti wakati wa Warsha na wadau. 

Uzinduzi huo umefanyika Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi Kuu Morogoro wakati wa kufunga warsha ya wadau ya uwasilishaji wa matokeo ya utafiti kuhusu Changamoto za ki-Afya zitokanazo na Ndoa za Utotoni nchini Tanzania, uliofanywa na Chuo Kikuu Mzumbe Kitivo cha Sheria kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Antwerp cha Ubelgiji, kupitia mradi wa VLIR UOS.

Programu hiyo imelenga kuongeza uwelewa wa Maaafisa Ustawi wa Jamii kuhusu masuala ya sheria na miongozo iliyopo katika kushughulikia changamoto za ndoa za utotoni, pamoja na kufuatilia kwa karibu matukio ya ndoa za utotoni pindi yanapojitokeza, ili kuripotiwa na kushughulikiwa na Mamlaka zinazohusika kwa wakati. 

Akihitimisha Warsha hiyo, Prof. Mwegoha amewashukuru wadau wa Maendeleo Serikali ya Ubelgiji, na wadau wengine wa ndani walioshiriki kufanikisha utafiti huo, ambao umelenga kutatua changamoto za ndoa za utotoni na madhara ya kiafya yatokanayo na ndoa hizo kwa watoto, ambazo kwa sehemu kubwa zinahusisha jamii ya watoto na familia masikini, wengi wao wakiishi vijijini. 

Ameahidi Chuo Kikuu Mzumbe, kuendelea kushirikiana kwa karibu na wadau wa mradi huo katika kuhakikisha matokeo ya utafiti huo yanakuwa na mwendelezo, na matokeo ya utafiti yanawafikia wadau wote muhimu, kama sehemu ya kuendelea kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la ndoa za utotoni ambazo zimekuwa zikikatisha ndoto wa watoto wengi katika jamii zetu.

“Chuo Kikuu Mzumbe kupitia mradi huu tunaahidi kuendelea kufuatilia kwa karibu na kutoa ushirikiano kwa wadau wetu wote wa ndani na nje, ili kuhakikisha tunakuwa sehemu ya kutatua changamoto za ndoa za utotoni na madhara yanayoambatana nayo,” amesisitiza

Baadhi ya washiriki wa Warsha waliwa katika picha ya pamoja. 

Akizungumza wakati wa kumkaribisha Mgeni Rasmi, Mratibu wa Mradi huo ambaye pia ni Mtiva wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu Mzumbe, Dk. Seraphina Bakta, amesema mradi huo ulianza mwaka 2020 na umehitimishwa mwaka huu kwa utafiti uliofanywa mkoani Dodoma na kuhusisha Wilaya mbili.

Amesema matokeo ya Utafiti huo yamepelekea kuanzishwa kwa Programu maalumu ya kimtandao ambayo wadau wataitumia kupata elimu ya sheria na kuripoti matukio mbalimbali ya ndoa za utotoni kwa wakati, ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa na Mamlaka husika.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Mwegoha, akizungumza na washiriki wa Warsha ya  uwasilishaji wa matokeo ya utafiti kuhusu Changamoto za ki-Afya zitokanazo na Ndoa za Utotoni nchini Tanzania, iliyofanyika Chuo Kikuu Mzumbe, Morogoro.

Aidha, mbali na programu hiyo, pia wameandaa mwongozo wa mafunzo ambao utatumiwa na Maafisa Ustawi wa Jamii na Maendeleo katika kutoa elimu  ya sheria kwa walengwa.

Ameahidi matokeo ya utafiti huo kuchapishwa katika majarida mbalimbali, pamoja kuanzisha mijadala ya kitaaluma na kisekta,  kwa kuhusisha wadau wote muhimu wa ndani, ili kuhakikisha matokeo ya Utafiti yanaleta matokeo chanya kwa jamii katika kukabiliana na changamoto ya madhara ya kiafya yatokanayo na ndoa za utotoni.

Warsha hiyo imehudhuriwa na wadau mbalimbali zikiwemo Taasisi za Serikali, Mashirika yasiyo ya Kiserikali “NGO’s,” Maafisa Maendeleo ya Jamii, Wanasheria,  na wawakilishi  kutoka Chuo cha Antwerp Ubelgiji. 

Prof. Wouter Vandenhole, Kaimu Mtiva wa Kitivo cha Sheria na Maendeleo ya Utafiti cha Antwerp nchini Ubelgiji, akichangia jambo wakati wa Warsha.
- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles