CHUO Kikuu cha Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam, kinatarajia kuanza kuwajengea uwezo wajasiriamali wa viwanda vidogo ili kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuiendeleza sekta hiyo na kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo.
Hayo yalisemwa mwishoni mwa wiki na Kaimu Makamu wa Chuo hicho, Profesa Josephat Itika, wakati wa mahafali ya 14 ambapo alisema kwa sasa kampasi hiyo inaandaa miradi mbalimbali ya ushauri na kozi fupi kwa kushirikiana na chuo cha Stellenbosch cha Afrika Kusini tayari kuanza kwa mpango huo mwakani.
Alisema pia kampasi itashirikiana na Shirika la Kimataifa la Kuendeleza Viwanda (UNIDO), kutoa mchango wake kwa jamii na Serikali katika kuimarisha viwanda hivyo viweze kuzalisha, kuongeza thamani na kutoa ajira.
Katika mahafali hayo, Mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta, aliwatunuku shahada mbalimbali za uzamili wahitimu na kutoa zawadi kwa wahadhiri waliofanya tafiti na kutoa machapisho mbalimbali kwa ajili ya kufundishia.
Pia wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao walitambuliwa.
“Tunafanya hivi kama moja ya njia za kutekeleza sera ya taifa ya kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025,” alisema.
Alifafanua kwamba, mpango huo utafuata miongozo ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi na kuwataka wataalamu katika vyuo watumie taaluma zao kubuni miradi inayolenga kulikomboa taifa.