26.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 28, 2023

Contact us: [email protected]

Mzee wa upako afunguka

Lusekelo
Anthony Lusekelo

 

MCHUNGAJI wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo Kibangu, Anthony Lusekelo, ameibuka na kuzungumzia uongozi wa Rais John Magufuli na sababu zilizochangia jina la Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kutawala Mkutano Mkuu maalumu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) uliomalizika Dodoma mwishoni mwa wiki.

Akizungumza na waandishi wa habari   Dar es Salaam jana, Mchungaji Lusekelo, maarufu kama ‘Mzee wa upako’, alisema ilikuwa ni vigumu kumalizika   mkutano huo wa CCM pasipo kutaja jina la Lowassa kwa kuwa ndiye alikuwa tishio katika Uchaguzi Mkuu uliomalizika Oktoba mwaka jana.

“Lowassa ni tishio ….hivyo ilikuwa ni ngumu kukwepa kutaja jina lake katika mkutano huo maalumu wa CCM ambao Magufuli alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa tano wa chama hicho,” alisema Lusekelo.

Katika mkutano mkuu huo, viongozi mbalimbali wa chama hicho walionekana kupagawa na kutaja jina la Lowassa kwa kumpiga vijembe kila walipokuwa wakizungumza.

Lowassa alijiengua CCM katika kipindi cha uteuzi baada ya jina lake kukatwa likiwa kwenye ngazi ya Kamati Kuu.

Alijiunga na Chadema na kuteuliwa kugombea urais akiungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kumpa wakati mgumu mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli.

Lusekelo alisema kuondoka kwa Lowassa kulisababisha kutokea mpasuko wa fikra ndani na nje ya CCM, jambo lililosababisha kuondoka kwa makada wengi wa kawaida na waliokuwa na vyeo.

“Ndani ya CCM kulitokea makundi ambayo yaliibua mpasuko hivyo tutumie muda wa sasa kuyafukia ili kila mmoja aanze kuchapa kazi.

“Huu ni mwaka wa kuponya majeraha yaliyotokana na uchaguzi huo hivyo tutumie muda huu kujenga utaifa na si kuendelea kupigana vijembe.

“Nasema hivyo kwa sababu naona hawa makada wanaorudi kwenye vyama vya awali kama Chadema na CCM wanaishia kupigana vijembe tu na kuendeleza majadiliano yasiyokuwa na msingi.

“Huu ni wakati wa kujenga umoja wetu kwa sababu amani ikitoweka itakuwa balaa kama ilivyo Sudan Kusini hivi sasa… na ninaamini nchi hiyo haitaweza kurejea tena kwenye amani hivi karibuni itakuwa kama Somalia. Naomba Watanzania tusifike huko,” alisema mchngaji huyo.

Alisema madaraka ni chanzo kikuu cha   vita katika nchi nyingi za Afrika, hivyo Tanzania inatakiwa kujifunza kutoka huko ili isiingie kwenye machafuko ya namna hiyo.

Pamoja na mambo mengine, alisifia uongozi wa Rais Magufuli akisema   wanaomwita kuwa ni dikteta uchwara hawajui maana yake.

“Watanzania wampe muda wa mwaka mmoja tu wataona mafanikio yake kwa sababu ni kiongozi mtekelezaji, kila kona ya nchi sasa kazi zinafanyika, ameijenga taswira nzuri ya Tanzania,” alisema.

Kiongozi huyo wa kiroho pia alizungumzia malalamiko ya wapinzani dhidi ya uongozi wa Rais Magufuli ikiwamo kupiga marufuku mikutano ya siasa.

Alisema hiyo inatokana na udhaifu uliopo kwenye Katiba ya mwaka 1977 inayotumika sasa.

“IGP anateuliwa na Rais, na Rais mwenyewe ndiye Amiri Jeshi Mkuu,  sasa hapo tutarajie nini lazima wamweshimu kwa kila kitu.

“Wataendelea kulalamika hivi hivi hadi ile Katiba ya Warioba itakaporudi na kumpunguzia Rais madaraka kama ilivyokuwa imetamka,” alisema mchungaji huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
579,000SubscribersSubscribe

Latest Articles