26.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Mzee wa miaka 95 aliyeombwa rushwa na polisi kumuona Magufuli

Abdallah Amiri-Igunga

MKAZI wa Kijiji cha Isakamaliwa Wilaya ya Igunga mkoani Tabora, Ngaka Mataluma (95) na viongozi wa CCM wa kata hiyo, wamepanga kuanza safari ya kwenda kuonana Rais Dk. John Magufuli ili kushinikiza askari polisi sita wanaodaiwa kumuomba rushwa wachukuliwa hatua za kisheria.

AskAri hao, ambao wanadaiwa kuomba na kupokea rushwa ya Sh milioni 8 kutoka kwa Matalamu, hawajachukuliwa hatua zozote na wakubwa zao, licha ya ushahidi kuwapo.

Akizungumza na MTANZANIA nyumbani kwake mjini hapa juzi kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Isakamaliwa Simon Makolo, alisema wamefikia uamuzi huo baada ya kuona vyombo vya dola vimeshindwa kuchukua hatua stahiki.

Alisema wamepanga kuanza safari ya kuonana na Rais Dk. Magufuli wakati wowote kuanzia sasa ili kufikisha kilio chao.

 “Wananchi wa Isakamaliwa, tumekuwa tukijiuliza juu ya ukimya uliopo wa askari hawa na viongozi wawili wa Serikali ya Kijiji cha Isakamaliwa, wanaotuhumiwa kuomba na kupokea rushwa ya shilingi milioni nane kutoka kwa Mataluma kutofikishwa mahakamani.

“Hali imesababisha Mataluma na viongozi wenzangu, tujipange kwa safari ya kwenda kuonana na rais, tukiamini atatusaidia jambo hili ili haki itendeke,”alisema

Alisema amekuwa akisumbuliwa na wananchi na Mataluma mwenyewe kutokana na kesi hiyo kutofikishwa mahakamani tangu Juni 12, mwaka huu, lilipotokea tukio hilo.

Alisema yeye na viongozi wengine, walitoa maelezo yao kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) na jeshi la polisi.

Alisema katika safari hiyo, Mataluma atafuatana na  Mwenyekiti wa CCM tawi la Isakamaliwa, Nkwabi Galishi na mkazi wa kijiji hicho, Jilunga Mwangali, viongozi wawili, mmoja wa serikali ya kijiji na mmoja wa chama ambaye ni katibu wa tawi  na mfanyabiashara aliyenunua ng’ombe 11.

Alisema pamoja na hatua hiyo, Mataluma amekuwa akisumbuliwa na mfanyabiashara Kashinje Mhela aliyenunua ng’ombe wake 11 ambao alilazimishwa na polisi hao akitaka arudishwe fedha zake Sh milioni  8.

“Ukimwangalia yule mzee Mataluma amezeeka kweli kweli, sasa anasumbuliwa na huyu mfanyabiashara arudishiwe fedha zake shilingi milioni 8 ambazo zinadaiwa kuchukuliwa na hawa askari. Anaishi maisha ya hofu kila kukicha, jambo hili lazima lipate ufumbuzi,”alisema.

UHAMISHO

Pamoja na kilio cha Mataluma, kuna taarifa za uhakika kutoka vyanzo vya jeshi la polisi Igunga, kuwa askari wamehamishwa vituo vingine vya kazi katika wilaya za Sikonge, Uyui na Nzega.

Inaelezwa Inspekta Frank Matiku (36) ambaye aliongoza askari hao kwa kile kichodaiwa rushwa, amehamishiwa Wilaya ya Sikonge kuwa Mkuu wa Upelelezi Msaidizi, PC Raphael Maloji (31) na Koplo Paulo Bushishi (49), wanahamishiwa Wilaya ya Uyui, DC Lucas Nyoni (31), PC Lome Laizer (39) na Koplo Charles Zacharia (45), wamehamishiwa Wilaya ya Nzega.

Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo alipoulizwa juu uhamisho huo jana, alisema yeye hajapata taarifa yoyote.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Barnabas Mwakalukwa alipoulizwa alisema  hana taarifa hizo.

“Umezipata taarifa hizi wapi, mimi ndio naingia Tabora, nitafuatilia,” alisema Mwakalukwa.

Hivi karibuni, Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tabora, Chaulo Mussa alisema wanasubiri askari hao wafukuzwe kazi  na mwajiri wao ili wawafikishe mahakamani.

Juni 12, mwaka huu katika Kijiji cha Isakamaliwa, askari hao na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Zahanati, Juma Mwagala na Ofisa Mtendaji wa Kijiji chicho, Edward Kitenya walituhumiwa kuomba na kupokea rushwa ya  milioni 8 kutoka kwa Mataluma, wakimtuhumu kujihusisha na vitendo vya upigaji ramli chonganishi, kumiliki nyara za serikali, zikiwamo ngozi ya kenge na bunduki aina ya gobole.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,206FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles