MZEE MWINYI ATAMANI JPM AONGOZE MILELE

0
449
Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, akiswali pamoja na waumini wakati wa swala ya Eid El Fitr iliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana. Picha John Dande.
Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, akiswali pamoja na waumini wakati wa swala ya Eid El Fitr iliyofanyika kimkoa katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam jana. Picha John Dande.

NA VERONICA ROMWALD–DAR ES SALAAM

RAIS Mstaafu  Ali Hassan Mwinyi amesema kama si matakwa ya Katiba   ya nchi, uongozi wa Rais John Magufuli ulipaswa kuendelea kuwapo miaka yote.

Alisema laiti ingelikuwa Katiba iliyopo haikufupisha muda wa uongozi wa rais,  angeshauri Rais Dk Magufuli awe  Rais wa Tanzania wa siku zote.

Alikuwa akizungumza   katika Viwanja vya Mnazi Mmoja  Dar es Salaam jana,    alipokuwa akitoa salamu za Eid El Fitri.

Mzee Mwinyi alisema mambo anayoyafanya Rais Dk Magufuli ni mazuri na yanalipeleka Taifa mbele.

Hii ni mara ya pili kwa kiongozi huyo kutamka hadharani namna anavyokunwa na utawala wa sasa wa Rais Magufuli.

Mwinyi alisema   Magufuli ameweza kufanya mambo mengi mazuri kwa kipindi kifupi kuliko yaliyowahi kufanywa na watangulizi wake akiwamo yeye (Mwinyi).

Katika kauli yake ya jana, Mzee Mwinyi alisema Rais Magufuli amefanikiwa kulipeleka Taifa mahali pazuri na amerejesha nidhamu katika maeneo mbalimbali ya kazi nchini.

“Nchi imetulia, leo mnakwenda madukani, hospitali, ofisini unapata huduma nzuri.

“Hayo ndiyo tuliyoyataka, kupata Serikali itakayokuwa na watumishi ambao watawatumikia watu na hivyo ndivyo inavyofanyika sasa kwa sababu tumempata kiongozi tuliyenaye leo (Rais Magufuli),” alisema na kuongeza:

“Huyu kiongozi ni wa kumuenzi sana, ni wa kumsaidia sana, ni wa kumsifu sana… si kumsifu kwa uongo, uongo, ni kumsifu kwa kazi nzuri anayoifanya si kwa manufaa yake bali kwa manufaa ya Watanzania wote pamoja na mimi niliyesimama hapa.

“Raia anataka nini tena baada ya haya?  Analindwa, anashughulikiwa, anayoyataka raia ndiyo anayoyataka Rais wetu… lakini kwa kuwa tuna Katiba basi twende na Katiba yetu.

“Husia wangu kwenu Watanzania wote, tumtii na kumsaidia Rais wetu ili mambo yaende vizuri kama yalivyo sasa.  Wazee wanasema hivi.  ‘kidole kimoja hakivunji chawa’. Tumsaidie ili mambo yaende hivi kama yanavyokwenda”.

Akizungumzia alipokutana na Rais Dk. Magufuli Ikulu baada ya mwaka mmoja wa uongozi wake, alisema yako baadhi ya maeneo ambayo aliyafanya kwa mafanikio makubwa ikilinganishwa na wakati uliopita.

Aliyataja baadhi ya maeneo hayo kuwa ni mapambano dhidi ya rushwa akisema hatua zilizochukuliwa katika   mwaka mmoja zimedhihirisha kasi kubwa ya kukabiliana na tatizo hilo ikilinganishwa na wakati uliopita.

“Rushwa ilikuwapo tangu enzi ya Hayati Mwalimu Nyerere … aliipondaponda kabisa lakini hakuimaliza, na sote tuliosalia ni hivyo hivyo, kila mmoja amefanya kwa kiasi chake, lakini Rais Magufuli kwa mwaka mmoja ameleta ‘surnami’, nafurahi sana,” alisema Alhaji Mwinyi.

Eneo jingine ni kuimarisha utendaji kazi Serikalini akisema  hatua zilizochukuliwa na Serikali ya sasa zimeongeza kasi.

Aliwataka  viongozi na wananchi kuunga mkono juhudi hizo.

“Tuliobaki tumsaidie, tumsaidie kwa kumuombea dua, tumsaidie kurekebisha kwa kusema ukweli pale ambako watu wanapotosha.

“Tusiwaache watu wakapata nafasi ya kuongea uongo, kila mtu anaweza kuwa anasema kutokana na nia yake na lengo lake, lakini hakuna asiyejua kuwa kazi aliyoifanya mwenzetu ni nzuri nzuri, nzuri ya ajabu,” alisisitiza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here