HIVI karibuni Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa amesema anajutia kitendo chake cha kuliingiza taifa katika ubinafsishaji wa rasilimali bila ya kujiandaa kikamilifu na mabadiliko hayo wakati wa Kongamano la Kigoda cha Mwalimu Nyerere lililofanyika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).
Katika kujuta huko alisema, “Kukosekana kuundwa mfumo mzuri wa udhibiti kumesababisha kuwepo kwa watu waliotumia fursa hiyo kwa maendeleo yao binafsi na si kwa Taifa.
“Kwenye uongozi wangu kitu ambacho mpaka sasa ninajutia ni kuanzisha sera ya ubinafsishaji na kushindwa kuweka mfumo au chombo cha kuudhibiti.
“Nilifanya kosa lakini hatuwezi kusema ubinafsishaji haufai kwa sababu ulisaidia kuleta mabadiliko na kuongeza uzalishaji katika mashirika yaliyokuwa yameshindwa kuendeshwa na serikali.”
Lakini ni kitu gani kilichosababisha kuwepo kwa udhaifu huo, hili ni jambo ambalo linahitaji rejea ya jinsi alivyokuwa anaongoza kwa jazba juu ya rushwa katika hotuba zake wakati anapiga kampeni za kutafuta uongozi wa juu wa Taifa mwaka 1995. “Rushwa, rushwa, rushwa…nitapambana na tatizo hili bila woga na wala sitamwonea haya mtu yeyote…”
Lakini vile vile kuna haja ya kutafakari maneno haya katika hotuba yake Mzee Mkapa kwa wananchi wake Oktoba 31, 2003: “… Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alitufundisha, Kupanga ni Kuchagua’. Maana yake ni kuwa kila uamuzi tunaoufanya una gharama yake na kwa kweli gharama za aina mbili. Utekelezaji wa uamuzi una gharama. Hiyo ni gharama ya kwanza. Lakini ipo pia gharama itokanayo na hasara ya kutoamua vinginevyo.
“Nitatoa mfano, ukiwa na Sh 10,000 unaweza kwa hiari yako kuamua kununua shati, chakula, mbegu za kupanda shambani. Ukiamua kununua shati, ipo gharama ya kukosa suruali na gharama ya kukosa mbegu. Katika istilahi za uchumi gharama hiyo inaitwa “Gharama ya Hiari”, au kwa Kiingereza, “Opportunity Cost”. Kiserikali, kwa mfano tukiamua kutenga Sh bilioni 1.8 kila mwezi kujenga barabara, fedha hizo haziwezi tena kutumika kununulia dawa. Gharama ya hiari ya kujenga barabara ni kuacha kununua dawa au kitu kingine.
“Kwa hiari yetu, tangu wakati wa Serikali ya Awamu ya Pili, Serikali ya Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi, tulifanya tathmini ya hali na mwelekeo wa uchumi wetu. Tulifanya hivyo kwenye chama tawala, tukaandaa mwelekeo wa sera za CCM katika miaka ya 2000 hadi 2010. Na kwa vile kwa msingi wa mwelekeo huo na Ilani ya Uchaguzi iliyotokana na mwelekeo huo, ninyi wananchi mmetupa ridhaa ya kuongoza nchi, basi mwelekeo huo kwa sasa ndio mwelekeo wa taifa letu.
“Tathimini ya hali na mwelekeo wa uchumi wetu ilitufikisha mahali ikabidi tuamue la kufanya, kwa kuzingatia hali halisi ya uchumi nchini na mazingira mapya duniani. Uchaguzi ulikuwa wazi. Ama tuendelee na uchumi hodhi wa dola wa sekta ya umma, au tukaribishe sekta binafsi ili taratibu igeuke kuwa injini ya uchumi wa Tanzania.
Tukaamua kukaribisha sekta binafsi. Kama uamuzi mwingine wowote, huu pia una gharama zake za kuweka mazingira mazuri kwa uwekezaji binafsi na gharama za hiari ya kuachia yale tunayodhani yana manufaa katika uchumi uliohodhiwa na dola… Tukaamua pia kubinafsisha mashirika ya umma. Uamuzi huo nao una gharama zake. Maana, tunaachia kilichokuwa chetu, na pengine kwa uchungu…
“Kupanga ni Kuchagua. Tulishachagua kukaribisha sekta binafsi, ya ndani na nje, na tulishaamua kubinafsisha mashirika ya umma. Uchaguzi huo ulikuwa hiari na kama nilivyosema, kila hiari ina gharama zake. Si busara leo kudhani maamuzi hayo hayana gharama. Dunia ambamo maamuzi hayana gharama, au yana bima dhidi ya hasara zozote, si dunia ya hali halisi; ni dunia ya kusadikika…”
Kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere maana halisi ya ‘Kupanga ni Kuchagua’ ni kuhimiza umakini zaidi katika kupanga matumizi ya Pato la Taifa ili kutoa kipaumbele (priority) kwa mambo muhimu zaidi kwa taifa. Dhana hii ilikuwa ni sehemu imani ya Mwalimu kwamba “Ni heri maskini huru kuliko tajiri mtumwa”.
Kwa mara ya kwanza Mwalimu alitoa dhana ya “Kupanga ni Kuchagua” katika Mkutano Mkuu wa TANU Mei 28, 1969. Azimio la Arusha lilikuwa na miaka mitatu wakati CCM ilikuwa haijaundwa.
Katika hotuba yake ilichapishwa kama kijarida, Mwalimu alizindua “Mpango wa Pili wa Maendeleo wa miaka mitano”. “Nia yangu jioni hii ni kutilia mkazo mambo fulani fulani ambayo naamini yanahitaji kutiliwa mkazo, hasa yale yasiyopendeza…” alisema Mwalimu na kutaja nia ya TANU kuhakikisha wanachi wote wanapata mahitaji muhimu manne. Alitaja mahitaji hayo kuwa ni chakula bora, mavazi bora, malazi bora na elimu.
“Lakini ingawa mpango wa pili ni bora kuliko ule wa kwanza, kuna jambo moja ambalo ni sawa kwa mipango yote. Kuweka mpango maana yake ni kuamua jinsi ya kutumia raslimali iliyo haba: maana yake ni kuchagua kutimiza baadhi tu ya shughuli nyingi na zote nzuri,” Mwalimu alidokeza.
“Kuna mambo mengi sana yanayohitajika sana Tanzania lakini ambayo hayakutiwa katika mpango huu. Kila mjumbe katika mkutano huu anaweza kutoa orodha ndefu ya mambo yanayofaa kufanyika katika wilaya au kijiji chake, lakini ambayo hayatafanyika katika muda wa miaka mitano ijayo, hata kama kila kazi iliyotajwa katika mpango huu ikitekelezwa…” aliasa Mwalimu na kuhitimisha: “Hatuna budi kuchagua baina ya mambo mengi mazuri, si baina ya mambo mazuri na mambo mabaya; maana kupanga ni kuchagua.”
Katika mazingira hayo inawezekana Mzee Ben hakuielewa vyema dhana ya kupanga ni kuchangua kutokana na tofauti inayojionesha katika ufafanuzi wa Mwalimu Nyerere na aliotoa yeye.
Aidha ni katika kipindi chake cha uongozi dhana ya kujenga ufahari ilipamba moto na matanuzi ya kawa yanaumuka kutokana na kuanzishwa kwa makampuni hadi yaliyosemekana kuanzia ndani ya Ikulu.
Katika mazingira hayo ni kwamba alisema Hayati Baba wa Taifa hakuwa anapinga na mwenendo mzima wa ujasiriamali inaweza kuelezwa kuwa hata hiyo dhana hakuielewa vizuri na hivyo akawa amejenga dhana ya ujasiri wa mali ulioifanya nchi kujiweka uchi mbele ya makuwadi wa uliberali mambo leo na hivyo jasho la wavuja jasho kuvunwa na wavuna jasho katika mazingira yaliyo endelevu.