32.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

Mwongozo wa Kitaifa wa uanzishaji majukwaa ya uwezeshaji wanawake wazinduliwa

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Serikali imezindua Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Uendeshaji Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi wenye lengo la kuleta ufanisi wa utekelezaji wa majukwaa haya ikiwa ni pamoja na kuyafanya yajulikane ngazi zote hapa nchini.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima akikata utepe kuashiria uzinduzi wa Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Uendeshaji Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi, Wilayani Kibaha mkoani Pwani.

Akizungumza katika Uzinduzi wa Mwongozo huo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajima ameitaka jamii kuelimisha Wanawake waone umuhimu wa kujiunga na majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kuanzia ngazi ya kijiji/Mtaa, Kata, Wilaya hadi Taifa, ili yawawezeshe kupata sehemu ya kujadili mambo yao kuhusu ujasiriamali na biashara kwa ujumla.

Pia amezitaka Halmashauri za Wilaya/Manispaa na Majiji ziendelee kutenga fedha za ndani ili kuwawezesha Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu kukopa na hatimaye kuweza kujiendeleza kiuchumi.

Ametoa rai kwa Wanufaika wa Mikopo ya asilimia 10 na mikopo ya Maendeleo ya Wanawake (WDF) inayotolewa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii wahakikishe wanarejesha mikopo hiyo kwa wakati ili iwanufaishe wengine kupata mikopo mapema. 

Vilevile Waziri Dk. Gwajima ameitaka jamii kutoa fursa sawa kwa Wanawake na wanaume kushiriki nafasi za uongozi na maamuzi katika ngazi ya jamii na kuwa sehemu ya maamuzi kwa ustawi wa jamii na Taifa letu.  

“Wanawake na wanaume tuzidi kuungana kupinga ukatili wa kijinsia na kwa watoto kwa kusimamia kurithisha misingi ya maadili mema kwa vizazi vyetu kwani ukatili ni adui wa maendeleo ya kiuchumi.” alisema Waziri Dk. Gwajima. 

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sarah Msafiri amesema kuwa, kupitia Mwongozo huo Mkoa wa Pwani umeanzisha Kampuni ya Go Mama PLC inayofanya shughuli zake ndani ya Mkoa.

Akieleza kuhusu Mwongozo huo Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dk Zainab Chaula amesema Wizara iliona umuhimu wa kuwa na Mwongozo wa Uanzishaji na Uendeshaji Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ili kuwa na ufanisi katika ushiriki wao hususani kwenye shughuli za maendeleo zitakazosaidia kuwakwamua kiuchumi.

Akitoa salamu za Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Zanzibar Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Mariam amesema Wizara itasimamia utekelezwaji wa Mwongozo wa Kitaifa wa Uanzishaji na Uendeshaji Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi ili kuwawezesha Wanawake hasa wajasirimali kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli zao mbalimbali.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wanawake Wafanyabiashara (TWCC) Mwajuma Hamza amesema Chama hicho kimefarijika kuona kuwa Serikali imejipanga ili kuhakikisha inawezesha Wanawake hasa katika kuwakwamua kiuchumi kwa kuweka Miongozo itakayo saidia kuratibu uanzishwaji na Uendeshaji wa Majukwaa hao.

Akizungumza katika uzinduzi wa Mwongozo huo Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, Bein’g Issa amesema Baraza lao limeweka mikakati mbalimbali yani kuwezesha Wanawake Kiuchumi kwa kushirikiana na Wizara walitarubu uanzishwaji wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa ngazi za Vijiji/ Mitaa, Kata, Wilaya na Mkoa.

Ameongeza kuwa uanzishwaji wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi umesaidia kutoa elimu ya ujasiriamali kwa wanawake wajasirimali jumala ya Majukwaa 26 yameamzishwa katika Mikoa ya Tanzania Bara, Majukwaa 151 katika Halmashauri, Majukwaa 1,354 ngazi ya Kata na Majukwaa 1859 katika ngazi ya vijijini/ Mitaa.

“Katika haya yote Mikoa mingi imefanya ubunifu ikiwemo kuanzishwa kwa makampuni, vikundi vya wajasirimali ambapo imesaidia kuwawezesha kiuchumi Wanawake hasa wajasirimali,” alisema Bein’g.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara Wanawake Mkoa wa Pwani, Mariam Ulega ameishukuru Serikali kwa jitihada zake za kuhakikisha inaweka mifumo mizuri ya kuwawezesha Wanawake hasa wajasirimali kupata fursa za kuanzisha biashara na kupata masoko ya bidhaa zao kwa ustawi na maendeleo ya familia na taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles