Renatha Kipaka -Bukoba
WAZIRI wa Ulinzi, Dk. Hussein Mwinyi, ameahidi kufidia wananchi waliotakiwa kupisha eneo la Kambi ya Jeshi ya Kaboya iliyoko Kata Mayondwe wilayani Muleba mkoani Kagera.
Alisema hayo alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari mkoani Kagera baada ya kutembelea eneo la Kaboya ambalo lilikuwa likikaliwa na watu tangu mwaka 2014.
Dk. Mwinyi alisema katika eneo hilo la kambi ya jeshi wananchi wachache walibaki bila kupatiwa fidia na kuanza makazi mapya.
Wakati huo huo, Dk. Mwinyi alisema katika ziara ya Kanda ya Ziwa amekutana na changamoto ya uhalifu Ziwa Victoria.
“Lengo kuu la ziara yangu nikutaka kukutana na wananchi wanaoishi Kaboya ili kuona namna watakavyolipwa fidia,” alisema Dk. Mwinyi.
Awali Mkuu wa Mkoa Kagera, Brigedia Jenerali Marco Gaguti, alisema mkoa huo uko salama pamoja na kuwa mpaka wa Tanzania na Uganda unahitaji kuongezewa ulinzi. Gaguti alisema ulinzi huo utaongeza ufanisi wa shughuli za kilimo kwa kufikia masoko kwa nchi ambazo wamepakana kama Sudan Kusini.