26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mwinshehe achaguliwa Mwenyekiti mpya wa CCM Pwani

Na Gustafu Haule,Pwani

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Pwani kimemchagua, Mwinshehe Mlao kuwa Mwenyekiti mpya wa chama hicho atakayeongoza kwa muda wa miaka mitano ijayo.

Mlao ameibuka mshindi katika uchaguzi uliofanyika Novemba 21, 2022 Mjini Kibaha ambapo katika nafasi hiyo wagombea walikuwa wanne akiwemo, Imani Madega, Farida Mgomi na Shaibu Mtawa.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (MNEC), Mohamed Mchengerwa (kulia) akisalimiana na wajumbe wa mkutano Mkuu wa Mkoa wa Pwani.

Hata hivyo, upinzani mkubwa ulikuwa Kati ya Mwinshehe Mlao na Farida Mgomi ambapo katika uchaguzi huo nafasi yao ilirudiwa kupigiwa kura mara mbili kwakuwa kikanuni mshindi wa kwanza alipaswa kupata kura zaidi ya nusu.

Msimamizi wa uchaguzi huo,amesema kuwa uchaguzi wa awali wa nafasi hiyo ulikuwa na wapiga kura 841 lakini kura zilizoharibika ni nane na kura halali 833 ambapo Mlao alipata kura 392 na Farida Mgomi alipata kura 367 wakati Imani Madega alipata kura 61 na Shaibu Mtawa kura 13.

Matokeo hayo yalipelekea uchaguzi msimamizi wa uchaguzi kufuata kanuni na hivyo uchaguzi kurudiwa kwa wagombea wawili akiwemo Mwinshehe Mlao na Farida Mgomi ambapo Mlao aliibuka mshindi kwa kupata kura 479 dhidi ya Mgomi aliyepata kura 341 Kati ya wapiga kura 824 huku kura nne zikiharibika na kubaki kura halali 820.

Aidha, Mlao amerudi katika nafasi hiyo baada ya kukaa benchi miaka mitano kwakuwa tayari alikuwa mwenyekiti wa CCM ndani ya Mkoa wa Pwani kwa muda wa miaka 10 na hatimaye nafasi yake kuchukuliwa na Ramadhani Maneno mwaka 2017.

Msimamizi wa uchaguzi huo, Zainabu Telack ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, amesema amemtangaza Mlao kwakuwa ndiye mshindi halali na amepata kura nyingi zaidi ya wagombea wengine.

“Kwa Mamlaka niliyopewa nachukua nafasi hii kumtangaza ndugu Mwinshehe Mlao kuwa mwenyekiti mpya wa CCM Mkoa wa Pwani kwakuwa ndiye mshindi halali na aliyepata kura nyingi zaidi  ya wengine,” amesema Telack.

Aidha ,katika nafasi ya mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC), Telack amemtangaza Mohamedi Mchengerwa ambaye ni Waziri wa Michezo,Sanaa na Utamaduni kuwa mshindi wa nafasi hiyo.

Amesema, Mchengerwa ameibuka kidedea baada ya kupata kura 762 kati ya kura halali 828  dhidi ya wapinzani wake akiwemo, Baraka Dau ambaye ni Mbunge Mstaafu wa Jimbo la Mafia aliyepata kura 38 na Mohamed Muga aliyepata kura 5.

Akizungumza Mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi Mlao amesema kuwa anawashukuru wajumbe kwa kumuamini na kumpa kura nyingi zilizosababisha kuwa mshindi wa nafasi hiyo.

Mlao,amesema kuwa ushindi wake imetokana na imani na wajumbe na kwamba kikubwa anachoenda kukifanya ni kuwarudishia imani wana CCM wa Mkoa wa Pwani katika kujenga na kuimarisha chama ili kiweze kushika dola zaidi katika chaguzi zijazo.

“Ninawashukuru sana wajumbe wote wa mkutano huu kwa kunichagua lakini lazima tujue tunakazi kubwa ya kufanya ndani ya Mkoa wetu hasa katika kuwaunganisha wanachama pamoja na hata kuhakikisha chama chetu kinasimama imara,”amesema Mlao.

Mlao amesema atahakikisha miradi yote iliyoanzishwa na watangulizi wake anakwenda kuisimamia ili hiweze kukamilika na hivyo kukifanya chama kiwe na miradi itakayosaidia kuendesha chama.

Naye Mchengerwa akizungumza na Waandishi wa habari baada ya ushindi wake, amewashukuru wajumbe kwa kumchagua huku akisema  atahakikisha anashirikiana na viongozi wanzake katika kufanya yale yote yenye kuleta tija kwa chama na Taifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles