32.3 C
Dar es Salaam
Saturday, November 30, 2024

Contact us: [email protected]

MWILI WA NDESAMBURO KUZUNGUSHWA MJI MZIMA

*Kuagwa siku mbili, kuzikwa Mbokomu kesho

Na Upendo Mosha,  Moshi


MWILI wa aliyewahi kuwa Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema), unatarajiwa kuagwa leo na maelefu ya wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro na maeneo ya jirani.

Mwili huo utazungushwa kwa gari katika mitaa mbalimbali ya Mji wa Moshi na vitongoji vyake kabla ya kupelekwa katika Uwanja wa Mashujaa, ambako kutafanyika misa ya kitaifa.

Ndesamburo maarufu kwa jina la Ndesapesa hadi umauti unamkuta alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro na amelitumikia jimbo hilo kutoka mwaka 2000 hadi 2015 alipostaafu.

Akizungumzia taratibu za kuagwa mwili wa marehemu, Mwenyekiti wa Kamati ya Mazishi ambaye pia ni Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini, alisema mwili huo utazungushwa mji mzima wa Moshi kwa kutumia gari maalumu, ili kuwapa fursa wananchi wa mji huo na maeneo jirani kumuaga mpendwa wao.

Alisema mwili wa Ndesamburo utatolewa  Hosptali ya Rufaa KCMC leo saa 4:00 asubuhi  na msafara wake utazunguka mzunguko wa YMCA kuelekea katikati ya mji.

“Mwili utaondoka KCMC saa nne asubuhi, utapita barabara ya KCMC, utakuja mpaka kwenye mzunguko wa YMCA, halafu utashika barabara ya njia mbili, kisha utakwenda hadi Msikiti wa Riadha (Mbuyuni) na kupita barabara ya Sokoni, tutaunganisha barabara ya Mawenzi inayopita polisi,” alisema Selasini.

Alisema baada ya kupita barabara hizo utarudi karibu na mnara wa saa uliopo karibu na Benki ya CRDB.

 “Halafu tutapita barabara ya Nakumatti, kisha barabara ya kiwanda cha kukoboa kahawa…baada ya hapo tutaingia viwanja vya majengo na shughuli zitaanza kama ratiba yetu ilivyo,”alisema.

Alisema baada ya mwili huo kuwasili katika viwanja hivyo, viongozi mbalimbali wa dini, kisiasa na Serikali  watashiriki katika ibada ya kumuaga Ndesamburo kwa kumwombea dua na kumfanyia ibada maalumu.

“Tunategemea viongozi mbalimbali wa dini zote watashiriki, tayari wamethibitisha kuhudhuria.

Baada ya ibada hiyo, viongozi watapewa nafasi ya kuzungumza baadae itasomwa historia ya marehemu,” alisema.

Alisema baada ya hatua hiyo, wananchi na viongozi mbalimbali watapewa nafasi ya kutoa heshima za mwisho, kisha mwili wa marehemu Ndesamburo utapelekwa nyumbani kwake Mbokomu kwa ajili  ya maziko.

Alisema baada ya mkesha wa maombolezo ambao utafanyika nyumbani kwake mwili wa marehemu Ndesamburo, kesho upelekwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) Usharika wa Kiboriloni kwa ajili ya misa ya mazishi.

“Baada ya kuagwa Majengo, mwili utapelekwa nyumbani kwake Mbokomu, kutakuwa na mkesha wa  maombolezo na siku ya Jumanne (kesho),  sala ya maziko itafanyika katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kasikazini, Usharika wa Kiboriloni  na baadae mwili utarejeshwa nyumbani kwake kwa ajili ya maziko,” alisema Selasini.

Alisema. “Tunaamini wakazi wa Moshi na maeneo mbalimbali kutoka nje ya mkoa wetu, watatuunga mkono nasi hatutaki kuingia mgogoro katika shughuli hii ya kumuaga mzee wetu,”alisema.

Naye Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Gholugwa, alisema mazishi ya Ndesamburo yatafanyika kwa siku mbili mfululizo.

Alisema siku ya kwanza, itakuwa  kwa ajili ya kumbukizi ya maisha yake na siku inayofuata itakuwa mazishi, huku ikikadiriwa watu zaidi ya 4,000 wanatarajiwa kushiriki.

Alisema mpaka sasa viongozi mbalimbali wa Chadema wakiongozwa na Mwenyekiti,  Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Vincent Mashinji na wabunge wamewasili Moshi.

 

LOWASSA NA SUMAYE

 

Waziri Mkuu  wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa na Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani wako nyumbani kwa marehemu Ndesamburo.

 

MAANDALIZI

 

Katika hatua nyingine, maandalizi katika Uwanja wa Mashujaa yameendelea usiku kucha wa kumkia jana.

Viongozi wa chama hicho wakiongozwa na Mbowe, jana walitembelea eneo hilo kwa ajili ya kujionea shughuli inavyoendelea.

Makada wa chama cha Chadema wameanza kutundika bendera za chama hicho katika barabara zote ambazo mwili wa mwanasiasa huyo mkongwe utapitishwa.

Marehemu Ndesamburo alifariki Mei mosi, mwaka huu akiwa ofisini kwake akiendelea na majukumu yake ya kila siku.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles