25.5 C
Dar es Salaam
Wednesday, December 11, 2024

Contact us: [email protected]

Mwili wa marehemu wazikwa na kuku tumboni

Pg 2

Na Kadama Malunde, Shinyanga
KATIKA hali isiyokuwa ya kawaida, mwili wa Benadetha Steven (35), aliyefariki dunia juzi umefanyiwa matambiko ya kimila baada ya kupasuliwa na wembe ukiwa kaburini na kuingiziwa kuku ndani ya tumbo lake ikiwa ni ishara ya kuondoa mkosi.
Tukio hilo lilitokea juzi katika Mtaa wa Mapinduzi wakati waombolezaji wakiwa hatua ya mwisho ya kumzika marehemu.
Lakini ghafla alijitokeza ndugu wa marehemu mwanamke kuwazuia waombolezaji, huku mwenyewe akiingia kaburini na kufungua sanduku na kuanza kuchana tumbo la marehemu aliyekuwa akisumbuliwa kwa muda mrefu na uvimbe tumboni.
Mashuhuda wa tukio hilo, walisema mwanamke huyo ambaye hakutaka kujitambulisha jina kabila la Mkurya, aliupasua mwili wa marehemu kwa kutumia wembe kisha kuchinja kifaranga cha kuku na kuumwagia damu baadaye kufunika jeneza na kuruhusu maziko.
Walisema kabla ya tukio hilo, kulitokea mabishano kati ya waombolezaji na ndugu wakitaka matambiko hayo yafanyike Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga alikokuwa akitibiwa.
“Mgogoro ulianzia nyumbani hata kabla ya kwenda makaburini, wakati mazishi yanaendelea ndipo ndugu mmoja wa marehemu akaingia kaburini akiwa amevaa mipira ya mkononi (glovu), akiwa na wembe na boksi dogo lililokuwa na kifaranga cha kuku na kuzuia waombolezaji wasitupe udongo kaburini.
“Ndugu huyo wa marehemu mwenye jinsia ya kike, aliingia kaburini baada ya mchungaji kumaliza ibada ya mazishi na kuruhusu mwili wa marehemu ufukiwe ndipo akaanza kuuchana kwa wembe, akachinja kuku kisha kummwagia damu na kumwingiza kuku huyo kwenye tumbo la marehemu, akafunika jeneza na ndugu wakaendelea na mazishi,” alieleza mmoja wa mashuhuda, Sijali Jumanne.
Jumanne alisema ndugu wa marehemu waliamua kufanya hivyo wakiamini wanaondoa mkosi ili kifo kama hicho kinachotokana na uvimbe tumboni kisitokee tena kwenye ukoo wao.
Mwenyekiti wa Mtaa wa Mapinduzi, Ayubu Daniel, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na kuongeza kuwa baada ya tukio alitoa taarifa polisi ambapo ndugu hao wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi.
Hata hivyo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ndala, Dickson Venance, alisema marehemu alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu na kwamba siku moja kabla ya mazishi kulikuwa na mgogoro juu ya mazishi ya mwanamke huyo ambaye aliolewa bila kulipiwa mahari.
“Kabla ya mazishi nilisuluhisha mgogoro, ndugu wa marehemu walikuwa wanataka mahari ya Sh milioni moja, kukawa na mvutano, wakakubaliana Sh 100,000, ndugu wa mwanaume wakachangishana wakakubaliana kuzika, sikuwepo wakati wa mazishi lakini nashangaa leo yamekuwa hayo,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, amethibitisha tukio hilo na kusema uchunguzi unafanyika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles