23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Mwili wa Leticia Nyerere kuwasili kesho

Leticia-Nyerere-256x300MAULI MUYENJWA NA ESTHER MNYIKA, DAR ES SALAAM

MWILI wa marehemu Leticia Nyerere unatarajiwa kusafirishwa kutoka Marekani kuja nchini kesho kwa ajili ya mazishi yaliyopangwa kufanyika katika Kijiji cha Butiama mkoani Mara.

Akizungumza na MTANZANIA jana, John Shibuda ambaye ni msemaji wa familia ya Musobi Mageni, alisema kuwa mwili wa marehemu Leticia utasafirishwa kutoka Marekani alipofariki dunia na baadaye utaagwa katika nyumba ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere, Msasani jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa.

“Mwili wa marehemu unatarajiwa kusafirishwa kuelekea Musoma siku ya Ijumaa kwa ajili ya mazishi na suala lililokuwa limechelewesha ni pamoja na kupatikana haraka cheti cha kifo nchini Marekani,” alisema Shibuda.

Naye Waziri Mkuu Kasimu Majaliwa aliyekwenda kutoa salamu za pole nyumbani kwa Mwalimu Nyerere, Msasani, aliwaasa ndugu na jamaa wa marehemu kuendelea kumwombea marehemu huku akisisitiza kuwa Leticia alikuwa ni mchapakazi wakati alipokuwa ni mbunge.

 

CHADEMA YAMLILIA

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Leticia aliyewahi kuwa mbunge wake katika Bunge lililopita.

Taarifa ya Chadema iliyosainiwa na ofisa habari wa chama hicho, Tumaini Makene ilisema: “Tunatoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki katika wakati huu mgumu wa kuondokewa na mpendwa wao.

“Mwenyezi Mungu awatie moyo wa ujasiri na subira katika wakati huu mgumu wa majonzi ya msiba huo.”

Taarifa hiyo ya Chadema ilisema kama chama watamkumbuka Leticia kwa mchango na ushiriki wake wakati wote alipokuwa mwanachama wao huku akiwa miongoni mwa watu waliopata fursa za kuwa wabunge kupitia chama hicho.

Leticia ambaye alikuwa mbunge wa viti maalumu katika Bunge la 10, alifariki dunia Januari 9 mwaka huu katika Hospitali ya Doctors Community iliyopo MaryLand nchini Marekani ambako alikuwa amelazwa tangu mwishoni mwa mwaka jana akitibiwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua.

Aliolewa na mtoto wa Baba wa Taifa, Madaraka Nyerere mwaka 1996 na kufanikiwa kupata watoto watatu ingawa baadaye walitengana na kuhamia nchini Marekani ambako alichukua uraia na kuishi kabla ya kurejea nchini ambapo mwaka 2010 aliteuliwa na Chadema kuwa mbunge wa viti maalum kwa miaka mitano.

Msemaji wa familia ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema juzi kuwa mwili wa marehemu Leticia unatarajiwa kusafirishwa kutoka nchini Marekani kwa ajili ya maziko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles